Ifuatayo in Taarifa kwa vyombo vya habari kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Nzega (CCM) Hamisi Andrea Kigwangalla, M.D
Bungeni, Dodoma, Mei 1, 2013.
Nawasalimu kwa heshima na taadhima.
Napenda kutumia fursa hii kutoa taarifa kwa wanahabari na umma kwa
ujumla kufuatia habari iliyotoka leo mapema asubuhi kwenye gazeti la
Sauti ya watu Tanzania Daima, toleo Na.3071 na kuzua mjadala mkubwa na
mzito kwenye jamii pamoja na kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na
hadhi, heshima na uadilifu wangu kwenye jamii nikiwa kama kiongozi wa
umma. Niwape pole wale wote walioguswa na kushughulishwa na jambo hili,
haswa familia yangu, ndugu, marafiki na wananchi wa Nzega; ambao siku
zote wanaamini sana katika uadilifu wangu na namna ninavyosimamia
misingi ya haki, sheria na uzalendo.
Nimesikitishwa sana na habari hii hususan kwa kuwa ilichapishwa bila
kunipa fursa ya kueleza kwa mapana uhusika wangu. Niwapongeze gazeti la
Nipashe kwa kupuuza uzushi huu mara baada ya kunipigia na kueleza upande
wangu wa hadithi.
Kumekuwa na wimbi kubwa la baadhi ya watu kwenye baadhi ya vyombo vya
habari kuandika habari za uongo kwa maslahi maovu ya kuwachafua
wanasiasa na watu wengine. Watanzania sote tubadilike na tukatae tabia
za kutumika vibaya namna hii, maana ni hatari kwa ustawi wa weledi, na
kwa umoja na mshkamano wa kitaifa. Ukishaandika jambo ambalo litamchafua
mwenziyo, hata kama utamsafisha kiasi gani ni wazi hautokuwa na uhakika
kuwa utawafikia wale wale waliosoma zile za jana za kumchafua – hivyo
ni jambo la kawaida kabisa kuanza kwanza kwa kuwa na uhakika kabisa na
habari kabla ya kuiandika.
Mfano mwaka 2010 tu mara baada ya kuteuliwa nilizushiwa kashfa ya
uongo kabisa inayohusiana na Uraia wangu na gazeti moja maarufu la kila
siku na mengine yakaweka kwenye ukurasa wa mbele kabisa kwamba
Kigwangalla ni Mrundi; hawakusema ni mrundi wa wapi, toka lini ama
kivipi, walisema ni mrundi tu! Basi hata kusema shaka yao inaanzia wapi
hawakusema. Kwa kuwa vyombo vya dola vilinisafisha na kupelekea kushinda
mapingamizi yote yaliyowekwa na washindani wangu kisiasa, niliamua
kudharau na kusema yatapita tu na yatasahaulika.
Pia gazeti lingine likaandika kwamba kampuni ya Kigwangalla ni
miongoni mwa makampuni yaliyowahi kufaidika na ‘stimulus package’ baada
ya mdororo wa uchumi mwaka 2008. Gazeti hata halikutaja kampuni ya
Kigwangalla ni ipi, inaitwaje, Kigwangalla ana hisa kiasi gani,
anaendesha kampuni hiyo ama la, na kampuni hiyo imepewa sh ngapi kutoka
benki kuu, na je imepewa pesa hizo kwa nyaraka zipi na zenye namba gani?
Na je pesa hizo imepewa kihalali ama imepitia mlango wa nyuma? Kama
imezipata pesa hizo kinyume na utaratibu, basi kuna ushahidi gani! Kwa
kuwa yalikuwa mambo ya uongo na uzushi niliamua kudharau na kuacha kama
ilivyo.
Gazeti lingine la kila siku liliwahi tena kuandika ‘Kigwangalla
atajwa kufadhili mgomo wa madaktari’ na liliweka hadithi hii kwenye
ukurasa wake wa mbele kabisa. Halikusema amefadhili sh ngapi? Amempa
nani? Zimeenda kufanya nini fedha hizo? Kwa kuwa lilikuwa ni jambo la
uongo, pia nilidharau na kuacha lipite. Mwaka jana Novemba pia gazeti
lingine liliandika habari na kuweka picha yangu na ya Ndg. Hussein
Bashe, na katikati yetu picha ya bastola, na kusema ‘Kigwangalla na
Bashe na vita ya bastola Nzega’, na humo ndani kueleza kuwa Kigwangalla
na Bashe wanyoosheana bastola wakati wakirudisha fomu za kugombea ujumbe
wa NEC. Na kuna mengine mengi: yale ya rushwa ya vitumbua n.k.
Yote haya kwa ujumla wake yalikuwa ni mambo ya uongo na yasiyo na
chembe ya ukweli hata kidogo. Mara zote nimekuwa nikiyadharau na kuongea
na wahariri wa vyombo husika vya habari kwa namna inayoashiria urafiki
na weledi wa kushirikiana na kufanya kazi pamoja na si vinginevyo;
ushauri ambao niliupata mwaka 2009 kutoka kwa moja ya wanasheria wa
kampuni yangu (wa kampuni ya Marando, Mnyele & Co. Advocates),
wakili nguli Mzee Mabere Nyaucho Marando, ambaye alisema ‘wasamehe tu
hawa gazeti la Sauti Huru maana ni vema kujenga marafiki wengi zaidi na
media kwa kuwa wewe ni kijana, kuliko kujenga maadui – na niliwasamehe
bila gharama yoyote ile’. Mzee Marando hakukosea, ila ukweli ni kwamba
ukifanya hivyo utaona patatulia kwa muda na baada ya hapo pataibuka tena
jambo lingine la ukurasa wa mbele linaloandikwa bila ukweli wowote ule!
Imekuwa wimbo wa kawaida kwenye baadhi ya media houses! Kufanya kazi
kwa maslahi ya watu fulani ama chama fulani, misingi ya weledi ya
uandishi haipo! Cha muhimu ni maelekezo ama utashi wa anayetoa chochote.
Jambo moja kubwa nililojifunza kutokana na yote haya ni kwamba, jambo
likiishaandikwa kwenye media halifutiki kwenye bongo za watu, hata muda
ukipita namna gani! Leo hii kila siku haya mambo yamekuwa yakirudiwa
rudiwa kwenye mitandao ya kijamii hata baada ya kuyatolea ufafanuzi wa
kina. Nimefika mahali nimeona niachane na passive ways za kushughulika
na media ili kuweka sawa kumbukumbu zangu mbele ya umma wa watanzania.
Ya ukweli: ni kweli kwamba ninamiliki hisa kwenye kampuni ya Emergent
Africa Ltd. Nina hisa 40% na mke wangu Dr. Bayoum Kigwangalla anamiliki
hisa 11%. Sijihusishi na kuendesha biashara hii kama mtendaji wa kila
siku – kampuni ina watumishi wake sehemu mbalimbali. Ni kweli kwamba
kampuni ina mradi wa kujenga chuo cha afya Nzega (International
Institute for Health Tabora), eneo la uchama, na ni kweli imepewa orodha
ndefu ya vitu ilivyosamehewa kodi na serikali kwa kuwa ni vitu/vifaa
vya mtaji (deemed capital goods). Ni kweli kwamba kampuni imewahi
kuingiza nchini kontena moja lenye vifaa vichache sana katika
vinavyotajwa kwenye habari ile, na vingi kati ya hivyo vipo aidha kwenye
stoo ya kampuni iliyopo Nzega ama ya Dar es salaam, Kigamboni. Kwa kuwa
vipo, wanahabari wanakaribishwa kwenda kuvitazama vitu hivi kama
wanapenda.
Ya uongo: Si kweli kwamba nina hisa 78% na mke wangu Dr. Bayoum
Kigwangalla ana hisa 22% – ni uongo. Si kweli kwamba kampuni imeagiza
vitu na kuvipitisha bandarini na forodhani kwa msamaha kwa nia ya kuuza
na hivyo kuiibia serikali kwa njia ya kukwepa kodi. Si kweli kwamba
kampuni ya Emergent Africa Ltd imeingiza vifaa vyote ambavyo imepewa
msamaha, kama habari inavyotaka kuwaaminisha waTanzania. Sijawahi kuuza
bidhaa zozote zile za kampuni hii zilizoingizwa nchini kwa njia ya
msamaha wa kodi. Kampuni ya Emergent Africa Ltd haina mradi wa kuuza
tiles na hivyo haijawahi kufanya biashara hiyo.
Ingekuwa ni dhambi kubwa kama kweli ningekuwa naviuza vifaa hivi bila
kuvilipia kodi. Na kama ningekuwa sina mradi genuine wa ujenzi wa chuo
na labda nimetumia vibaya nafasi yangu ya ubunge kujipatia msamaha ili
kurahisisha biashara zangu basi ningeanza kwa kuuza cement (ambayo ni
bidhaa inayokimbia sana sokoni na kampuni yangu imepewa msamaha wa
karibu tani 5000 – lakini sijawahi kuutumia msamaha huu kununua hata
mfuko mmoja wa cement!). Ama ningeingiza mabati/vigae vya kuezekea
(ambavyo pia vinakimbia sana sokoni kwa kuwa watu wengi wanajenga –
lakini sijaingiza hata kigae kimoja!), ama ningeingiza malori 4, Nissan
Navara pick up 4, Mitsubishi Canter 2, Landcruiser Hardtop 4( ambazo
zinatumika sana kwenye utalii na hata kwenye barabara za vumbi) kwa
msamaha – lakini sijaingiza hata gari moja kati ya haya, kinyume na
habari hii ya Tanzania Daima inavyotaka kuuaminisha umma! Kuonesha
uadilifu nitaeleza hapa mfano mmoja kwamba mnamo Novemba mwaka jana
nilinunua gari moja SUV aina ya Nissan Patrol (T934 CDB) na nimeilipia
kodi zote bila msamaha japokuwa ningeweza kutumia msamaha wa kodi
kununua na kuingiza moja ya magari yaliyopo kwenye msamaha huu wa
kampuni ambayo mimi ni major shareholder. Pia nina ujenzi wa nyumba ya
kuishi Nzega, Tabora na Dar es salaam katika hatua mbalimbali: ningeweza
kutumia msamaha huu wa kodi wa kampuni yangu ili kujipatia unafuu
kwenye manunuzi ya vifaa mbalimbali vya ujenzi kama cement, vigae ama
mabati, lakini sijawahi kufanya hivyo hata siku moja!
Kuwa na hisa kwenye kampuni inayofanya biashara halali siyo dhambi.
Kupata msamaha wa kodi siyo dhambi. Dhambi ingekuwa kuviuza baada ya
kupata msamaha. Kama kuna mtu anaamini kuwa kuna vifaa vimeuzwa na
kampuni yangu, kati ya hivi vilivyoingizwa nchini kwa msamaha,
anakaribishwa kuleta uthibitisho wa nyaraka za mauzo (cash sale
receipts, tax invoice ya mauzo, pay-in slip ya benki ya malipo, delivery
note, ama receipt yoyote ile ya kampuni hii inayoashiria kuwa mauzo
yamefanyika) ili niweze kufuatilia kujua ni nani aliyeuza na kwa nini
alifanya hivyo ili niweze kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yake ikiwa
ni pamoja na kumpeleka mbele ya vyombo vya sheria.
Msamaha wa vifaa hivi ni kwa ajili ya Ujenzi wa Chuo Cha Afya Nzega
(kitakachoitwa International Institute for Health Tabora), ambacho
nilikianza kwa fedha zangu mpaka pale kilipofikia na sasa tunasubiria
majibu ya benki ya maombi yetu ya mkopo ndipo tuendelee. Na msamaha huo
upo na hautotumika kwa mambo mengine ya binafsi kama nilivyoeleza hapo
juu kwenye ununuzi wa gari langu binafsi la kutembelea na ujenzi wa
nyumba yangu binafsi ya kuishi Nzega, Tabora ama Dar es salaam (ambako
ninajenga).
Watanzania tuache kushabikia uongo. Kufanya hivyo kunaziba mianya ya
ukweli kutamalaki. Tuache kutazama mambo kwa macho ya wivu, husda na
majungu. Tusimame kwenye misingi ya ukweli daima. Nchi hii itaendelezwa
na watu wenye kuchukua maamuzi thabiti na hatua za maksudi za kuleta
mabadiliko – kama miradi ya namna hii (ya chuo cha afya Nzega kule!).
Nchi yetu bado ina watu waaminifu na waadilifu na tunaamini tutafanikiwa
kuwadhibiti walio waovu. Hata siku moja kweli haijawahi kushindwa vita
na uongo. Si kila mtu aliyeko kwenye uongozi ndani ya CCM basi ni
fisadi, watu wazuri na wasafi wapo pia. Tusimuangalie kila mtu kwa sura
ya ‘ufisadi’ na ‘ubadhirifu’ tu! Tuaminiane jamani. Tusifedheheshane na
kukatishana tamaa. Safari kuelekea mapinduzi ya maisha ya watanzania
kiuchumi na kijamii bado ni ndefu lakini tutafika. Tufanyeni kazi.
Taarifa hii nimeiandika na kuitoa mimi mwenyewe, Hamisi Andrea
Kigwangalla, M.D., Mbunge, Jimbo la Nzega. (simu yangu ya kiganjani ni
0782636963 na email yangu ni hkigwangalla@gmail.com, website: http://www.hamisikigwangalla.com )
إرسال تعليق