SERIKALI NA FIFA ZIMEIUMBUA TFF, ANGETILEH IOMBE RADHI SERIKALI!

Mh Amos Makalla (kushoto ) akiwa na Angetileh Oseah

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) limeliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanza upya mchakato wake wa Uchaguzi Mkuu baada ya kubaini mambo kadhaa lilipokuja kusilikiza malalamiko ya baadhi ya wagombea wa uchaguzi huo.
Uamuzi huo wa Fifa ni kama ulikuwa ukitabiriwa na wadau wengi wa michezo nchini kutokana na madudu yaliyofanywa na Kamati ya Uchaguzi na ile ya Rufaa ya TFF, kiasi cha baadhi ya wagombea kuamua kupeleka malalamiko yao Fifa baada ya kutokuwa na chombo chenye mamlaka mengine hapa nchini.
Mvutano ulizidi kupamba moto baada ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuingilia kati.
Kutokana na hali hiyo, serikali ilipitia upya malalamiko hayo ambayo yalilenga kubatilisha uamuzi wa TFF kuendesha uchaguzi huo kwa kutumia marekebisho ya katiba yaliyofanyika mwaka 2012 kwa njia ya waraka uliosambazwa kwenye mikoa yote wanachama wa TFF.
Tofauti na katiba inavyosema kwamba, ili marekebisho ya katiba yafanyike, ni lazima mkutano mkuu ukae, TFF ilipitisha marekebisho hayo bila ya mkutano mkuu kukaa kwa maelezo kwamba hawana fedha za kuendesha mkutano huo.
Serikali iliagiza kutotumiwa kwa katika hiyo ya mwaka 2012, hapo ndipo palipoibuka malumbano kati ya Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mh. Amos Makalla na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah.
Angetile ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari alikuwa akijibizana wazi wazi na Mh. Makalla huku akijua kwamba kinachofanywa na waziri huyo ni maagizo ya mabosi wake ambao ni waziri husika, Dr Fenella Mukangara na serikali kwa ujumla.
Hatukupenda majibizano hayo kwa kuzingatia vitu viwili, kwanza, TFF ipo chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, hivyo kuendeleza malumbano kwa Angetile na Mh. Makalla hakukuwa na manufaa ya kukuza soka la Tanzania.
Ni malumbano ambayo Angetile hakupaswa kuyapa nafasi kwa kuwa serikali ndiyo inayoratibu kila kitu kinachohusu michezo nchini na hata uamuzi wa kuipiga ‘stop’ katiba ya 2012 lilikuwa jambo sahihi ambalo hata Fifa waliliona baadaye.

ANGETILEH ALIKUWA AKIBISHANA NA SERIKALI
Angetileh alipokuwa akilumbana na kujibizana na Mh. Makalla tunadhani alisahahu kwamba Makalla anafanya kazi chini ya serikali ya Rais Jakaya Kikwete, hivyo kupingana na kujibizana na mtu kama huyo ni sawa na kujibizana na serikali iliyo chini ya Mh. Kikwete.
Kama chombo cha habari, www.shaffihdauda.com tunadhani Angetile atakuwa amejifunza kutokana na jambo hili na kwa kuzingatia taaluma yake anapaswa kuviomba radhi vyombo vya habari, kwani wadau wa soka walikuwa wakimtazama Angetileh kwa macho mawili kwanza akiwa kama katibu mkuu wa TFF pili akiwa kama mwandishi ‘ Senior ‘ wa habari za michezo.
Kitendo kile kilitoa picha mbaya kwa waandishi wa habari karibu wote, hasa wanaondika habari za michezo. Tunasisitiza hii haikuwa picha nzuri kwa taaluma.
Hakukuwa na haja ya Angetile kubishana na Mh. Makalla kama angekuwa anafahamu anayebishana naye ni naibu waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ambayo kimsingi hata yeye Angetile, Mh. Makalla ni kama bosi wake.
Hatujuhi ilipopatikana nguvu ya Angetile kubishana na Mh. Makalla huku akimdharau naibu waziri huyo kwa kusema hata akienda wizarani atazungumza na waziri husika na siyo msaidizi wake.
Hoja ya kwamba, Mh. Makalla alikuwa akiegemea upande mmoja haikuwa na mashiko kwani uamuzi wa kutotumia katiba ya mwaka 2012, ulipata pia baraka za Mh. Dr Mukangara na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

MSIMAMO WETU
Tunaamini kwamba, Angetile ni binadamu kama walivyo binadamu wengine hivyo atakuwa amebaini kosa alilofanya katika jambo hili hivyo kutorudia tena endapo hali kama hii itajitokeza hapo baadaye (kama atabaki madarakani).
Tutaendelea kusimamia haki katika michezo bila kupindisha ukweli na kamwe hatuwezi kuzifanyia kazi kelele za watu wengine ambao kwa namna moja au nyingine hawana nia nzuri na soka la Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post