Amani Makungu amepata mrithi |
Na Salum Vuai, Zanzibar,
CHAMA cha Soka Zanzibar, kimepata Rais mpya kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika leo katika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Aliyefanikiwa kukalia kiti hicho, ni Ravia Idarous Faina (42), aliyewabwaga wapinzani wake wawili, kwa kuzoa kura 37 kati ya 53 zilizopigwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa ZFA.
Abdallah Juma Mohammed, Mwanasheria wa chama hicho, yeye alipata kura 16, huku mwanafunzi anayetarajia kuhitimu digrii ya sheria katika Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu hivi karibuni, Rajab Ali Rajab akishindwa kupata hata kura moja.
Uchaguzi huo uliitishwa kufuatia kujiuzulu kwa Amani Ibrahim Makungu mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, baada ya kukiongoza chama hicho kwa miezi saba tu.
Makungu pia alichukua nafasi hiyo kupitia uchaguzi mdogo uliofanyika Juni 30, 2012, baada ya kuachia ngazi kwa Ali Ferej Tamim, aliyekaa madarakani kwa zaidi ya miongo miwili.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa chama hicho Gulam Abdallah Rashid, Rais huyo mpya aliwashukuru wote waliomchagua na waliomnyima kura, na kusema ushindi huo ni wa kila anayelitakia mema ZFA na soka la Zanzibar.
Alisema, kila uchaguzi unakuwa na mambo yake, pamoja na wagombea kubebwa na watu wanaowaunga mkono, lakini mwisho mshindi anakuwa mmoja, hivyo wapiga kura wanapaswa kuvunja kambi zao ili kuimarisha chama na kufanya kazi kwa matakwa ya Wazanzibari.
Aliahidi kuongoza kwa kufuata katiba na kanuni zinazotawala mpira wa miguu Zanzibar , na kusema hatakaribisha nafasi ya uongozi au utendaji isiyotajwa ndani ya katiba.
Aidha, alisema kwa wakati wote akiwa madarakani, atahakikisha chama kinakuwa na sauti ya pamoja na kuvunja mgawanyiko kati ya Unguja na Pemba ( UFA na PFA) yaani Unguja Football Association na Pemba Football Association kama wengi walivyoanza kubatiza
Post a Comment