MOURINHO ASIMIKWA RASMI DARAJANI, AMWAGA SERA ZA KUMTOA NYOKA PANGONI


Rasmi darajani, amesisitiza hajawahi kuwa na bifu na Abramovich, ataka kumrejesha John Terry uwanjani, awataka wachezaji kucheza kwa uzalendo mkubwa.
Kocha aliyejaliwa  kuwa na maneno mia kidogo, Mreno Jose Mourinho leo hii ametambulishwa rasmi kuwa kocha mpya wa wazee wa darajani, klabu ya Chelsea.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mourinho ambaye miaka ya nyuma akiwa na Chelsea alikuwa anajiita “The Speacial one” kwa tafsiri isiyo rasmi,  akimaanisha mtu maalumu, leo hii ametoa kali ya mwaka baada ya kubadili jina hilo na kujiita “The Happy One” kwa tafsiri isiyo rasmi unaweza kusema “Mtu mwenye furaha pekee”.
Mreno huyo ambaye ametokea klabu ya Real Madridi ya Hispania leo mchana ametambulishwa jijini London na kujibu maswali mengi kutoka kwa wanahabari waliohitaji kujua mambo mengi kutoka kwake likiwemo suala la uhusiano na bosi wake Abramovich.
Mourinho ambaye miaka ya nyuma alitimuliwa na mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich baada ya kushindwa kuelewana, leo hii amesema kipindi cha nyuma alikuwa na mahusiano mazuri na bosi wake, endapo wangekuwa na mahusiano mabaya asingerejea kwa mara ya pili darajani.
Akiongea na wanahabari wapatao 250 leo katika uwanja wa Stamford Bridge, aliulizwa kama ataendelea kujiita “The Special one”, kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 kwa sasa alisema “I am the Happy One” na kumalizia maneno yake kwa kusema “nina furaha sana”.
Mourinho alisema ” Mambo mengi sana yametokea katika maisha yangu ya kufundisha soka na kazi yangu miaka tisa iliyopita, lakini ni mtu yule yule, nina moyo uleule, nina hisia zile zile za kupenda mpira na kazi yangu, lakini kwa sasa ni mtu mwingine kabisa baada ya kurudi nyumbani Chelsea, nina furaha sana”.
Mourinho amewataka wachezaji wake kujituma zaidi na kuongeza kuwa klabu ni muhimu kuliko wao, kwani isingekuwepo wao pia wasingekuwepo.

Post a Comment

Previous Post Next Post