Dar. Siku moja baada ya Simba kumwongezea mkataba Amri Kiemba, klabu hiyo ya Msimbazi inatarajia kumpiga bei kiungo huyo mwenye kiwango kilichosimama kwenye mstari kwa timu ya Wydad Ac Casablanca ya Morocco.
Mpango wa kumuuza Kiemba umekuja baada ya mashushushu wa timu hiyo ya Morocco kuridhishwa na kiwango alichoonyesha wakati akiichezea Taifa Stars dhidi ya Morocco katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia mwakani.
Katika mchezo huo, Stars ilifungwa mabao 2-1, huku Kiemba akifunga bao nzuri la kufutia machozi kwa kiki ya mwendo mrefu nje ya boksi la hatari.
Zakaria Hanspope, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Simba, aliithibitishia Mwananchi jana kuwa, mazungumzo ya awali ya kuuzwa kwa kiungo huyo aliyewahi kucheza Yanga yako hatua za mwisho kukamilika.
“Ni kweli, mazungumzo ya awali yameshafanyika kati ya Simba na uongozi wa Wydad Ac Casablanca, leo tunamalizia tulipofikia,” alisema Hanspope.
“Niko Morocco kufanya mazungumzo ya mwisho na uongozi wa Wydad Casablanca, natumaini tutafikia mahala pazuri Mungu akijalia,” alisema Hanspope.
Mmoja wa vigogo wa Kundi la Friends of Simba ndiyo aliyeushtua uongozi juu ya mpango huo, ambao nao waliharakisha kumsainisha mkataba mpya kabla ya kumuuza. Juzi, Simba ilimsainisha Kiemba mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh35 mil.
إرسال تعليق