Na Mwandishi Wetu
KWELI asiye na adabu hakosi sababu ya kuharibu, mwenye mdomo mchafu ni ada yake kutoa neno chafu, mwanamuziki chipukizi, Omar Faraji Nyembo ‘Ommy Dimpoz’, amedhihirisha kuwa ana kiwango cha juu sana cha dharau kwa kumdhihaki na kumtusi mtu aliyetangulia mbele za haki.
Utamaduni wetu Tanzania na kama ilivyo kwa mafundisho ya dini kupitia vitabu vinne vitakatifu, Torati, Zaburi, Injili na Kuran, fundisho ni kwamba mja aliyepoteza maisha hakashifiwi, hasimangwi, hahukumiwi, isipokuwa huhifadhiwa kwa heshima kisha kuombewa salama na amani mbele ya Mungu.
Ommy Dimpoz, kijana ambaye ni mwaka jana tu alikuwa ‘anawanga’ huku na huko mikono nyuma akiomba msaada wa kimuziki, hivi sasa anajiona ameota meno ya juu kuweza kung’ata, kiburi hicho kimempa uthubutu wa kumtusi Mfalme wa Freestyle, marehemu Albert Kenneth Mangwea ‘Ngwair’.
Thamani ya Ngwair na namna alivyozikwa kwa heshima hajaviona, badala yake akatusi kuwa Mfalme wa Freestyle alikufa maskini ndiyo maana mazishi yake yalikuwa ya kuungaunga michango ya wadau.
Kifo cha Ngwair, kilivuta makundi mbalimbali kushiriki kwa hali na mali kuchangia na kumzika, taifa lilizizima mkoa kwa mkoa, mguso huo wa kitaifa aliokuwa nao mwanamuziki huyo, Ommy hakuuona, isipokuwa akanena: “Sitaki kufa maskini kama Ngwair.”
Akimweleza mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, Juni 10 (Jumatatu) na Juni 11, mwaka huu (Jumanne), Ommy alidhihaki hata ushiriki wa wanamuziki waliosimamisha shughuli zao kwa muda kisha kuungana na kushikamana kuhakikisha Ngwair anazikwa kwa heshima.
“Sitaki nikifa yatokee kama ya Ngwair, amekufa Afrika Kusini, hata kuusafirisha mwili kuuleta Tanzania imebidi mpaka watu wachangie, ile ni aibu sana,” alisema Ommy kwa dharau.
JUMANNE (JUNI 11)
Kutokana na uzito wa maneno ambayo Ommy aliyatamka kuhusu Ngwair, siku iliyofuata (Jumanne), mwandishi wetu alimpigia simu kumuuliza kama maelezo hayo ya kashfa aliyatoa akiwa amelewa au la?
Ommy kwa kujiamini, alijibu kwamba alichokisema kuhusu Ngwair ni ukweli kwa asilimia 100.
MWANDISHI: Nakushauri kama mdogo wangu, siku nyingine usirudie kutamka maneno hayo ni mabaya sana kwa mtu aliyekufa.
OMMY: Sijaongea neno baya, nimesema ukweli wasanii hatutakiwi kufa maskini.
MWANDISHI: Wewe unaona mtu akichangiwa baada ya kufa ndiyo kipimo cha umaskini?
OMMY: Kuna mambo mengi ambayo yangefanyika kabla ya kuchangiwa lakini Ngwair alishindwa kuyafanya.
MWANDISHI: Sasa Ngwair angefanya nini wakati yeye ameshakufa?
OMMY: Kuna mambo yangefanyika, mfano kusafirisha mwili kutoka Afrika Kusini.
MWANDISHI: Sasa Ngwair angejisafirisha mwenyewe?
OMMY: Nachosema mimi ni kwamba wasanii hatutakiwi kufa maskini.
MWANDISHI: Sikiliza Ommy, hata mabilionea wakubwa huwa wanachangiwa. Mtu kuchangiwa siyo kashfa wala aibu kama unavyotaka kulionesha tukio la Ngwair. Marehemu Steven Kanumba alikuwa anatembelea Toyota Lexus V8, mbona alipokufa kila kitu alifanyiwa? Ni jambo la kawaida.
OMMY: Ngwair alikuwa na ‘stresi’ za maisha ndiyo maana alikuwa anakula unga.
MWANDISHI: Ulishawahi kumwona Ngwair akitumia unga?
OMMY: Kwanza nakusikia unanirekodi, sijui una malengo gani.
MANENO YA KASHFA MLIMANI CITY
Juni 8, mwaka huu, katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, wakati wa utoaji wa Tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) mwaka 2012-2013, Ommy Dimpoz alizungumza maneno ya kashfa ambayo moja kwa moja yalitafsiriwa ni dongo kwa Ngwair.
Baada ya kutangazwa mshindi wa kipengele cha Video Bora ya Mwaka na kukabidhiwa tuzo yake, Ommy alibwabwaja: “Jamani tumechoka kuzika wasanii maskini wenye majina makubwa.”
Japo hakutaja jina la yule aliyekuwa anamzungumzia, tafsiri ya wengi ni kwamba Ommy alikuwa anamzungumzia Ngwair kwa sababu ndiye staa aliyekuwa amezikwa kishindo cha siku moja tu kabla ya usiku huo wa tuzo. Ngwair alizikwa Alhamisi, tuzo Jumamosi.
“Huyu dogo ana nyodo sana, sasa haya ni maneno gani ya kuzungumza? Hapa anamzungumzia Ngwair, ila anapaswa kujua kwamba yeye bado msanii mdogo sana kumlinganisha na Ngwair,” alisema mtangazaji mmoja kwa masikitiko.
MAPOZI NI KAWAIDA YAKE, ATIMULIWA KIGOMA ALL STARS
Ndani ya Kampuni ya Kigoma All Stars, awali Ommy alikuwa mmoja wa wajumbe kwenye bodi ya wakurugenzi lakini hivi karibuni alitimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Peter Msechu.
Chanzo chetu makini ndani ya Kigoma All Stars, kimetonya kuwa Ommy alionesha tabia mbaya dhidi ya wasanii wenzake wanaounda kampuni hiyo, hivyo hakukuwa na jinsi zaidi ya kumtimua ujumbe wa bodi na kumuweka Msechu.
“Alikuwa ameshakuwa kero. Unajua pale Kigoma All Stars wote ni mastaa lakini yeye anajiona yupo juu ya wote. Tunaitisha vikao hatokei, tunakwenda kufanya shoo hatokei, tunamuona hana umoja na sisi na hatufai.
“Uamuzi wa kwanza ulikuwa ni kumtimua kabisa ili asiwepo kabisa kwenye kampuni yetu, maana siyo lazima kila mtu mwenye asili ya Kigoma awepo Kigoma All Stars. Baadaye kwa busara za mlezi wa kampuni yetu, Zitto Kabwe ndiyo tukamuondoa kwenye bodi.
“Tumembakiza kwenye kampuni kama mwanahisa wa kawaida tukiwa tunampima. Akiendelea kuleta mapozi yake, hatutamvumilia, tutamfukuza moja kwa moja,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kiliongeza, ndani ya Kigoma All Stars kuna wasanii wakubwa kama Nasibu Abdul ‘Diamond’, Ali Kiba, Mwasiti Almasi, Sunday Mangu ‘Linex’, Banana Zorro na wengineo lakini hawaringi, isipokuwa Ommy ndiye fungakazi kwa maringo.
Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), vilevile Waziri Kivuli wa Fedha na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alipoulizwa kuhusu Ommy kutimuliwa kwenye bodi, alikiri hilo kufanyika.
“Ni kweli kuna mabadiliko kwenye bodi, wanamuziki wenyewe kwa sababu ndiyo wanahisa, waliamua kumuondoa Ommy Dimpoz na nafasi yake akawekwa Peter Msechu,” alisema Zitto.
Kuhusu kutimuliwa kwenye bodi Kigoma All Stars, Ommy hakutaka kuzungumza chochote, badala yake alijikanyagakanyaga.
OMMY NA NYIMBO TATU
Ommy anajiita super handsome, mapozi, kampuni yake anaiitwa Pozi Kwa Pozi, majina hayo yanatosha kueleza sababu kwa nini amemdhihaki Ngwair na haelewani na wasanii wenzake.
Ndiyo kwanza ana nyimbo tatu tu, Nai Nai (alisaidiwa sana na Ali Kiba), Baadaye na Me & You (amesaidiwa sana na Vanessa Mdee) lakini amekuwa wa migogoro na mbwembwe nyingi dhidi ya wasanii wenzake.
Alishawahi kurushiana maneno kwenye vyombo vya habari na mwanamuziki Cyril Kamikaze, baadaye akaingia kwenye gogoro zito na mwana Hip Hop wa Nako 2 Nako Soldier, Isaac Waziri Makuto ‘Lord Eyez’.
Kuhusu Lord Eyez ambaye ni memba wa Familia ya Weusi, alidai alimuibia taa, power windows, vioo na vifaa vingine vya gari lake lakini kesi ilipofika mahakamani, Ommy hakwenda kutoa ushahidi.
Ommy alishindwa kutoa ushahidi lakini kabla yake alitangaza katika vyombo vya habari kuwa Lord Eyez ni mwizi na kwamba alimwibia vifaa vya gari lake, zaidi ya hapo alikusanya watu wakampa kipigo memba huyo wa Weusi kisha wakampeleka polisi ambako aliwekwa lupango
HABARI KUTOKA GLOBALPUBLISHERS.INFO
SOMA ALICHOJIBU OMMY DIMPOZ HAPA
http://rashidijuma.blogspot.com/2013/06/ommy-dimpoz-aeleza-sababu-ya-global.html
http://rashidijuma.blogspot.com/2013/06/ommy-dimpoz-aeleza-sababu-ya-global.html
إرسال تعليق