Maggid Mjengwa: Kama Mahiga, nakubaliana na njia ya Warioba ya Serikali tatu

Picture

 
Balozi, Mahiga
Ndugu zangu,

Gazeti la Mwananchi leo Jumapili, mbali ya habari nyingine kemkem, lilibeba habari iliyonivutia kuisoma kwanza;” Dk Mahiga asema Katiba Mpya ni heshima”- (Mwananchi, Jumapili, Juni 9, 2013).

Balozi  Augustine Mahiga ambaye ni Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UN nchini Somalia  anizungumzia Rasimu ya Katiba kama jitihada za ubunifu katika kufikia mwafaka  wa mazungumzo  kuhusiana na kero za Muungano.

Balozi Mahiga anasema, kuwa ingawa Serikali Tatu zina gharama zake, lakini, kisiasa ina manufaa yake kutokana na mijadala ya muda mrefu kuhusiana na muundo wa Muungano. Balozi Mahiga anazidi kunukuliwa akisema, kuwa iwapo Rasimu hiyo itapitishwa na Watanzania, ni wazi kwamba  Tanzania itakuwa imerekebisha kasoro za Muungano unaotimiza miaka 50 mwakani, kwa njia ya mazungumzo. ( Mwananchi, Jumapili, Juni 9, 2013, Uk 2)

Ndugu zangu,

Balozi Mahiga ameongea mengi mengine kuhusiana na Katiba, lakini, kwa mtazamo wangu, hayo ya juu yana uzito mkubwa sana. Ni maneno yaliyojaa hekima na busara nyingi kutoka kwa Mtanzania na 

Mwanadiplomasia mzoefu. Mahiga kwenye mazungumzo yake ametanguliza maslahi  mapana na ya muda mrefu ya taifa.

Nakubaliana na Balozi Mahiga kwenye usahihi wa njia ya Jaji Warioba na Tume yake kuhusiana na Serikali Tatu.

Maana, njia ni ile ile tuliyokuwa tukihangaika kuifuata huku kukiwa na kero nyingi za njiani. Ni kwa vile njia ilikuwa nyembamba mno. Alichofanya Warioba na Tume yake ni kuipanua ili hata malori yaweze kupita.

Katiba Mpya ina maana pia ya Mabadiliko Makubwa. Ninachokiona mimi ni hofu ya mabadiliko kwa baadhi yetu. Na kwa wengine ni hofu inayotokana na sababu binafsi  zenye kuambatana na kupoteza fursa hata nafasi za kimamlaka katika mabadiliko yanayokuja. Hivyo, ni sababu za  kibinafsi zaidi nap engine hata kimakundi.

Ni hulka ya mwanadamu pia kuogopa mabadiliko yanapotokea. Hata kwenye nyumba yako tu. Siku ukirudi nyumbani ukakuta mfanyakazi wako wa ndani kapangua fenicha na kuziweka katika utaratibu mpya , basi, utaanza kwanza kuyaogopa mabadiliko yale. Na huenda akili yako isitulie pia.  Kidogo kidogo utaanza kuyazoea.

Hili la Serikali Tatu kwa historia tu inabidi tupumue kwa akina Jaji Warioba kuja na ubunifu huu. Maana, imekuwa ni kero sugu iliyoundiwa hata Wizara. Hatuwezi kuendelea na hali hiyo mwaka hadi mwaka.

Maana, hata mimi binafsi, ningeulizwa mwaka 2000 juu ya muundo wa Muungano, basi, chaguo langu la kwanza lilikuwa Serikali Moja, pili, Serikali Mbili na tatu Serikali Tatu.

Lakini, miaka 13 baadae, na kwa kusoma alama za nyakati. Ukiniuliza leo swali hilo jibu langu liko wazi kabisa, kuwa tuwe na Serikali Tatu; Ya Muungano, Zanzibar na Tanzania Bara ( Tanganyika). Na hii si heshima tu tutakayoipata kimataifa, bali, itachangia kwa watu wa pande mbili hizi za Muungano kuheshimiana na kushirikiana zaidi.

Na tusisahu historia, kuwa Kamati ya Jaji Robert Kissanga mwaka 2000 ilikuja na mapendekezo kama haya ya Serikali Tatu. Nakumbuka Rais Mkapa pale Diamond Jubilee akiongea na Wazee wa Dar es Salaam alionyesha dhahiri kuwa Serikali haikuyapenda mapendekezo yake. 

Kukawa na hata mjadala kama Kamati inaweza kuja na mapendekezo au la, maana, ikasemwa kuwa ya Kissanga haikuwa Tume. Na Mkapa akawashambulia pia wanahabari kwa kutaka kuishinikiza Serikali kuyakubali mapendekezo hayo. Kitu ambacho hakiwezekani, maana, Serikali hata siku moja haiwezi kushinikizwa na wanahabari kama haikubaliani na inachoshinikizwa nacho. Lakini huo ulikuwa ni mwaka 2000, na sasa ni 2013. Wakati umebadilika.

Naam, na tuendane na wakati unaobadilika. Tuwe na ujasiri wa kuzipa mgongo fikra za ukale.

Maagid Mjengwa,
Iringa.
0754 678 252
 

Post a Comment

Previous Post Next Post