Kwa mara nyingine, Tanzania yetu imeshuhudia tukio la kigaidi
lililopelekea vifo vya watu wasio na hatia. Jumamosi iliyopita, wakazi
wa jiji la Arusha walikumbwa na janga la kigaidi baada ya bomu kurushwa
katika mkutano wa kampeni za CHADEMA kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani.
Kwa hesabu za haraka, tukio hilo la kigaidi ni la pili kutokea jijini
Arusha kwa siku za hivi karibuni, na la tatu tukijumuisha na lile la
mauaji ya Padre Evaristus Mushi huko Zanzibar.
Cha kusikitisha ni kwamba hadi wakati ninaandika makala hii, haki
haijatendeka kwani licha ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa
WATUHUMIWA wawili, mmoja kwa tukio la Zanzibar, na mwingine kwa tukio la
kanisani Arusha, mwenendo wa kesi hizo na hisia miongoni mwa wananchi
mbalimbali unaleta hisia hiyo ya haki kutotendeka na/au kuonekana
imetendeka.
Lakini hata kama haki ingekuwa imetendeka katika matukio hayo mawili ya
mwanzo, ukweli kwamba leo hii tunaongelea tukio jingine la kigaidi
unamaanisha kitu kimoja tu: taasisi zetu za usalama zimezidiwa uwezo wa
kukabiliana na tishio hilo linaloonekana kuzidi kukua la ugaidi.
Niliwahi kuandika huko nyuma kuhusu mapungufu kadhaa katika taasisi zetu
za usalama ambayo ninaamini kuwa yalipelekea taifa letu kushuhudia
majanga hayo.
Na kama nilivyobashiri, japo niliomba Mungu aepushie mbali, kwamba
pasipo hatua za haraka tunaweza kushuhudia vitendo vya kigaidi
vikiendelea, kwa bahati mbaya (au makusudi?) mwishoni mwa wiki tumeona
bayana mwendelezo wa matukio hayo.
Na japo nisingependa iwe hivyo, kuna uwezekano wa hali hiyo kuendelea
kwa sababu tuliowakabidhi dhamana ya kupambana na ugaidi wameshindwa
jukumu hilo muhimu.
Lakini kwa upande mwingine, tukizungumzia ugaidi, hisia za haraka
zinaweza kuelekezwa kwa kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Usalama wa
CHADEMA, Wilfred Lwakatare, ambaye licha ya kuachiwa kwa dhamana na
mahakama, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai ameonyesha nia ya kupinga
dhamana hiyo akitaka kiongozi huyo wa CHADEMA arejeshwe rumande.
Labda msomaji unaweza kujiuliza kama mie, hivi kipaumbele cha taifa letu
kwa sasa ni kuendeleza kesi hiyo ‘ya kisiasa’ au kukabiliana na
matishio halisi ya ugaidi ambayo tayari yameshapoteza maisha ya
Watanzania wenzetu?
Haihitaji upeo mkubwa wa kufikiri kubaini kuwa kesi inayomkabili
Lwakatare ni ya kisiasa zaidi, na ambayo kimsingi inapaswa kufutwa kwa
sababu baadhi ya wabunge wa CCM wameshaitolea hukumu kwamba sio tu
Lwakatare ni gaidi bali pia CHADEMA ni chama cha kigaidi.
Tukiweka kando ‘ishu’ ya Lwakatare na tuhuma za CCM kuwa CHADEMA ni
chama cha kigaidi, binafsi nina maswali kadhaa ambayo labda kwa kuyaweka
hadharani yanaweza sio tu kutupatia majibu lakini pia kuamsha tafakuri
mpya kuhusu hatma ya nchi yetu kiusalama.
Baada ya matukio ya tukio la ugaidi huko Zanzibar na hatimaye Arusha,
baadhi ya wananchi tulishauri viongozi husika serikali wawajibishwe. Hao
ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, Inspekta
Jenerali wa Polisi Said Mwema, na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa
Taifa, Rashid Othman. Swali: kwanini hadi sasa linatokea tukio la tatu
la kigaidi viongozi hao hawajawajibishwi?
Katika hili, ni vigumu kukwepa kumtupia lawama Rais Jakaya Kikwete kwani
yeye ndiye aliyewateua na pia ndiye mwenye mamlaka ya kuwawajibisha,
tukiamini kuwa watendaji hao wamegoma kujiwajibisha wenyewe. Je itakuwa
makosa kuhisi kuwa Rais Kikwete bado ana imani nao licha ya mapungufu
yao ya wazi ya kiutendaji kazi?
Kwa vile watendaji hao wamegoma kuwajibika, na Rais haelekei kuwa na
mpango wa kuwawajibisha, na kibaya zaidi, tayari kumeshatokea matukio
matatu ya kigaidi, kwanini tusihisi kuwa usalama wa nchi yetu unazidi
kuwa hatarini kwa sababu hakuna jitihada zozote za makusudi za
kuhakikisha kuwa matukio ya ugaidi sio tu yanazuiwa bali yanakomeshwa
kabisa?
Lakini pia tukio hilo la majuzi huko Arusha limekuja wakati Tanzania ipo
kwenye ‘vita ya maneno’ na Rwanda kufuatia ushauri (wa nia njema tu) wa
Rais Kikwete kwa Rwanda kuwa itafute suluhu na waasi wa kundi la FDLR
ambao wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994-5.
Pamoja na kuafikiana na ushauri wa Rais Kikwete, lakini hivi nchi yetu
haionekani ‘kituko’ kwa ‘kujifanya washauri wa amani na usalama wa
Wanyarwanda’ ilhali sie wenyewe tunaishi kwa hofu ya matukio ya ugaidi
ambayo hayana dalili ya kutotokea tena?
Kadhalika, nchi yetu imeamua kwa nia nzuri tu kuunga jitihada za Umoja
wa Mataifa kusaka amani huko DRC. Lakini, pamoja na nina hiyo nzuri,
hatuonekani ‘watu wa ajabu’ kwa kuelekeza nguvu zetu kusaka amani huko
ilhali kwa mujibu wa matukio ya hivi karibuni, magaidi ‘wapo huru’ kuua
Watanzania at will (watakavyo)?
Kingine kilichonikera sana ni ukweli kuwa lilipotokea tukio la ugaidi
kanisani huko Arusha, tuliambiwa kuwa Rais Kikwete ameamua kukatisha
ziara yake huko Falme za Kiarabu ili kuja kuwafariji wahanga wa tukio
hilo. Muda huu ninapoandika makala hii, Rais yupo hapa Uingereza
kuhudhuria mkutano wa G8.
Hivi kuna sababu zozote zinazomfanya Rais asirejee huko nyumbani kutoka
na tukio hili? Je tukio la ugaidi kwenye mkutano wa CHADEMA huko Arusha
lina umuhimu mdogo kuliko lile la kanisani ambalo lilimlazimu Rais
kuahirisha ziara yake (japo kuna wanaodai alikuwa ameshamaliza ziara
hiyo)?
Majuzi, akiongelea tukio hilo la ugaidi, Rais alidai, (namnukuu), “Mimi
siamini kuwa Watanzania au wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi
cha kufanyiana matendo ya unyama wa aina hii. Naamini kuwa hiki ni
kitendo cha mtu au watu wasioitakia mema nchi yetu, watu ambao
wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki miongoni mwa raia, au
makundi ya raia, ili nchi yetu iingie kwenye machafuko makubwa.”
Swali, je Kikwete haamini hivyo kutokana na hisia zake tu au ndio
taarifa za kiusalama anazopatiwa kila siku zinavyomweleza? Lakini hata
kama ni sahihi Rais kuamini hivyo, hivi kauli za Mwigulu Nchemba ambaye
kuna ushahidi wa video unaomwonyesha akiwaambia wananchi waliokuwa
wakimsikiliza kuwa wasipoichagua CCM watakufa na baada ya siku moja
tangia atoe kauli hiyo kweli watu waliuawa kwa bomu?
Lakini pengine katika kuonyesha ‘ombwe’ la kiuongozi katika serikali ya
Kikwete, wakati Rais anasema hayo, tamko la serikali lililotolewa na
Waziri William Lukuvi linahitimisha kuwa, (namnukuu), “Katika siku za
karibuni, zimekuwepo jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa,
makundi ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki kwa raia dhidi ya
vijana wetu wa Jeshi la Polisi, kuwafanya raia wawachukie askari,
kuwafanya raia wasiwaamini askari, kuwafanya raia wasiwape ushirikiano
askari na hatimaye kuwa na taifa ambalo halitawaliki.”
Sasa hapo tumwamini Rais Kikwete anadai haamini kuwa Watanzania au
wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya
unyama wa aina hii, au Waziri Lukuvi ambaye anasema kwa hakika kuwa
matukio ya ugaidi kama hilo la majuzi huko Arusha ni matokeo ya jitihada
za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi ya kijamii na watu
binafsi kupandikiza chuki kwa raia dhidi ya polisi?
Lakini wakati jeshi la polisi likitangaza tume ya kuchunguza tukio hilo
Arusha na kutangaza zawadi ya shilingi milioni 100 kwa atakayetoa
taarifa kuhusu wahusika, tumeshuhudia dhihaka kubwa ikifanywa na Spika
wa Bunge Anne Makinda kwa kutoona umuhimu wa kuahirisha bunge angalau
kwa siku moja kwa heshima ya Watanzania wenzetu waliokufa au kujeruhiwa
katika tukio hilo.
Inaelezwa kuwa Spika Makinda ameshindwa japo kumtumia SMS Mwenyekiti wa
CHADEMA (Taifa) Freeman Mbowe kwa janga hilo (lakini Rais Kikwete anadai
haamini kama kuna chuki baina ya wafuasi wa vyama vya siasa).
La kuchukiza zaidi ni ‘uhuni mkubwa’ uliofanywa na Katibu Mwenezi wa CCM
Nape Nnauye ambaye amenukuliwa akidai kuwa inawezekana CHADEMA
wanahusika na tukio hilo la kigaidi. Hii ni zaidi ya chuki ya kisiasa
(ambayo Bosi wa Nape, Rais Kikwete, anaamini kuwa ipo); huu ni unyama wa
hali ya juu. Kuna haja gani ya jeshi la polisi kuunda timu ya uchunguzi
au kupoteza fedha za umma kwa dau hilo la shilingi milioni 100 ilhali
tayari akina Nape wanawajua wahusika?
Nimalizie makala hii kwa swali hili, kwanini IGP Mwema adai jeshi la
polisi litamchunguza Mwigulu kwa kauli yake kuwa wananchi wasipoichagua
CCM watakufa (na kweli kesho yake baadhi wakauawa au kujeruhiwa kwa
bomu) lakini YUPO HURU HADI MUDA HUU ilhali Lwakatare alikamatwa kwa
tuhuma ‘nyepesi tu’ na sasa jitihada zinafanywa arejeshwe rumande baada
ya kupewa dhamana?
Sio tu kuwa tunaelekea kubaya bali tumeshafika kubaya. Rais Kikwete
alisisitiza hivi karibuni kuwa nchi haijamshinda. Je, kwa mwenendo huu
wa magaidi kuangamiza maisha wanavyotaka tusemeje?
http://www.chahali.com/2013/06/makala-yangu-ktk-raia-mwema-toleo-la_21.html?utm_source=feedburner&utm_medium=feed&utm_campaign=Feed%3A+chahali%2FQwqK+%28Kulikoni+Ughaibuni%29
إرسال تعليق