Marekani kutoa msaada wa kijeshi kwa waasi wa Syria


Waasi nchini Syria
Marekani imetangaza rasmi kuwa itatoa msaada wa kijeshi kwa waasi nchini Syria baada ya uchunguzi wao kuonesha kuwa majeshi ya rais Bashar Al Assad yamekuwa yakitumia silaha za kemikali dhidi ya waasi hao.

Mshauri wa rais Barrack Obama, Ben Rhodes amesema Washington DC inakadiria kuwa kati ya watu 100 na 150 wameuawa baada ya kushambuliwa na silaha hizo za kemikali na majeshi ya serikali.

Serikali ya Syria kwa upande wake imekanusha madai hayo ya Marekani na kusema kuwa sio ya kweli na kuungwa mkono na nchi ya Urusi ambayo ni mshirika wa karibu wa rais Assad.

Katibu Mkuu wa Majeshi ya Kujihami ya nchi za Magharibi Anders Fogh Rasmussen kwa upande wake, ameitaka serikali ya Syria kuruhusu Umoja wa Mataifa kwenda nchini humo na kufanya uchunguzi wa matumizi hayo ya silaha za kemikali.

Uingereza pia kupitia Waziri wake wa Mambo ya nje William Hague imesema kuwa London imeafikiana na uchunguzi huo wa Marekani na suluhu la haraka linastahili kuchukuliwa ili kumaliza mzozo wa Syria.

Marekani sasa inataka marufuku ya angaa kuwekwa nchini humo hali ambayo serikali ya Ufaransa kupitia msemaji wa Wizara ya mambo ya nje Philippe Lalliot anasema haitakuwa rahisi kutokana na China na Urusi kuendelea kutumia kura zao za veto katika Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupinga azimio lolote dhidi ya Syria.

Awali, rais Obama alikuwa ameionya serikali ya Syria kutotumia silaha hizo za kemikali kwa kile alichosema ikiwa ingefanya hivyo itakuwa imevuka mstari mwekundu.

Hadi sasa, haijafahamika wazi ni msaada upi ambao Marekani watatoa kwa waasi hao wa upinzani huku wachambuzi wa maswala ya usalama wakisema huenda rais Obama akawapa waasi hao silaha za kisasa, vifaa vya mawasiliano na ndege za kivita.


Tangazo hili la Marekani linakuja siku moja baada ya Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu kutangaza kuwa zaidi ya watu elfu 93 wameuawa wakiwemo watoto 6,500 kutokana na machafuko yanayoendelea katika taifa hilo.

Kiongozi wa tume hiyo Navi Pillay amesema kuwa idadi ya maafa huenda ni kubwa na pia itaendelea kuongezeka ikiwa machafuko yataendelea na suluhu kutopatikana.

Aidha, UN inasema kuwa watoto nchini Syria wanatumiwa kama ngao katika mapigano hayo kati ya majeshi ya serikali na waasi wa upinzani.

Post a Comment

Previous Post Next Post