MGAWANYO WA MKOA WA MBEYA WAJIELEKEZA KUVUTIA KIMAKABILA


Mnyukano wa ugawaji wa mkoa wa Mbeya umeendelea kujenga sura ya uasilia wa waliopo kwenye madaraka kutokana na wanasiasa kuvutia maeneo walikotoka bila kujali vigezo vya msingi ikiwemo idadi ya watu.
Kulingana na vikao vinavyoendelea, wilaya ya Rungwe tayari imeshajitengenezea mazingira mazuri ya kupigiwa debe kuwa mkoa kwa kile kinachobainishwa kuwa madiwani wengi katika mkoa wa Mbeya asili yao ni wilaya ya Rungwe
Dhana ya “kumitu kukhaja ” inaonekana wazi wakati huu  kwenye mchakato wa kutoa mapendekezo ya wapi na maeneo yapi yaunganishwe kuunda mkoa wa mpya  baada ya Mh Rais Kikwete kutamka wazi na kubariki mchakato huo wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi mei mosi.
Mfano wa kujipigia debe unaonyesha kuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya Mbarali Keneth Ndingo ni mkazi wa Rungwe hivyo maamuzi ya baraza la madiwani la Mbarali yanaonekana kuwa na msukumo wa nyumbani, ambapo wamependekeza makao makuu yawe Rungwe
Maajabu ya musa yanajitokeza katika ugawaji unaopendekezwa ambapo inaelezwa kuwa Mbarali wanapendekeza halmashauri za Busokelo, Rungwe, Kyela, Ileje na Mbozi ziunde mkoa mpya wakati kijiografia havina uwiano kati ya Mbozi na Rungwe.
Kulingana na takwimu za sense ya mwaka2012, wilaya ya Mbozi kabla ya kugawanywa kupata Momba ilikuwa na wakazi 740,719 idadi ambayo ni sawa na idadi za wakazi wa wilaya za Kyela, Rungwe na Ileje ambazo kwa pamoja ni wakazi 685,098 hivyo kuwepo kwa pengo la 55621 zaidi kwa upande wa Mbozi
Kulingana na jiografia ya mkoa wa Mbeya, Mkoa ambao kwa sasa ungeweza kuundwa kwa kuunganisha wilaya za  Ileje, Mbozi, Momba  na sehemu ya wilaya ya Chunya  (jimbo la Songwe) ambalo limejitenga na eneo la Lupa kwa umbali wake.
Kwa takwimu hizo hizo mkoa wa  huo ungeweza kuwa na idadi ya wakazi 1,201,327 ambao  ni asilimia 44.4 ya takwimu za sasa za wakazi wa mkoa wa Mbeya wanaofikia 2,707,410.
Ingawa jitihada za kujipanga zimeanza kwa upande wa wilaya za Rungwe, Mbarali na Kyela kwa kufanya ushawishi wa mbinu,ukweli unabakia kuwa wilaya ya Mbozi peke yake inavigezo vyote vya kupata mkoa mpya kuanzia idadi ya watu, eneo la utawala,makazi, uwezo wa raslimali za ndani kujiendesha na fulsa za kiuchumi zilizopo na zinazoweza kupatikana.

Post a Comment

Previous Post Next Post