Na Kija Elias, Moshi — WAFANYAKAZI wa Supermarket ya Nakumatt, iliyopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wameulalamikia uongozi wa duka hilo kwa madai ya kuwanyanyasa na kuwaomba rushwa ya ngono.
Wafanyakazi hao ambao tayari walishafikisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama walidai wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya unyanyasaji ikiwemo kuombwa rushwa ya ngono na Meneja Mkuu na na msaidizi wake.
Walisema imekuwa kawaida kwa kila msichana anayefika kuomba nafasi kazi, lazima aombwe rushwa ya ngono huku wanaume wakitakiwa kinyume na maumbile: “Kila msichana anaefika hapa kuomba nafasi ya kazi, anaombwa rushwa ya ngono ndipo apatiwe kazi huku wanaume wakiingiliwa kinyume na maumbile,” walisema.
Aidha walisema sababu iliyowafanya wafikie maamuzi ya kuandamana hadi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa
kutaka msaada ni kukithiri kwa vitendo hivyo.
Akizungumzia tuhuma hizo, Meneja wa Nakumatt Moshi, Alfrick Milimo alikanusha tuhuma hizo na kudai kwamba zote hizo ni njama za kupakana matope za watu wasiolitakia mema duka hilo.
Alisema kumekuwa na watu wanaozunguka kuwashawishi wafanyakazi huku akikumbushia matatizo yalitokea kipindi cha nyuma kati ya uongozi na wafanyakazi wake na kuwa tayari wameshabaini njama hizo.
Alisema katika duka lake kuna wafanyikazi wa Kenya na Tanzania lakini mara nyingi tatizo linatokea pale wanapowalazimisha Watanzania kufanya kazi maana wengi hawapendi kufanya kazi bila kushurutishwa: “Niko hapa kwa ajili ya kuwafundisha, kuwaonya na kuwaelekeza lakini inaonekana kuwa unapofanya hivyo unaonekana kuwa wewe ni mbaya na wanafika kazini na mavazi yasizoendana na maadili ya kazi pia wanasinzia kazini,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, amekiri kupokea malalamiko hayo kutoka kwa wafanyakazi hao na kuahidi kuyashughulikia. Alisema tayari ameshaagiza Idara ya kazi kulifuatilia suala hilo kwa karibu na kutoa taarifa mapema ikiwa ni pamoja na idadi kamili ya Watanzania na Wakenya wanaofanya kazi katika duka hilo.
إرسال تعليق