MTANZANIA ATEULIWA KUONGOZA JESHI LA KULINDA AMANI HUKO DAFUR


Lt. Jenerali Paul Ignace Mella,Mkuu Mpya wa Jeshi la Mseto kati ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika maarufu kama UNAMID linalolinda Amani huko DARFUR Nchini Sudan. 
Lt. Jenerali. Mella kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) anachukua nafasi iliyoachwa na Lt. Jenerali Patrick Nyamvumba kutoka Rwanda ambaye amemaliza muda wake Machi 31,2013.
---------
Kwa mara nyingine Bendera ya Tanzania imeendelea kupepea katika Tasnia ya Ulinzi wa Amani ya Kimataifa.

Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Bi. Nkosizana Dlamin Zuma wametangaza... uteuzi wa Luteni General Paul Ignace Mella Kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) kuwa Mkuu Mpya wa Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa huko Darfur ( UNAMID)

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, na nakala yake kutumwa katika Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, imeeleza kwamba, Lt. Gen. Mella anachukua nafasi iliyoachwa na Mkuu wa zamani wa Jeshi hilo (UNAMID), Lt. Gen Patrick Nyamvumba kutoka Rwanda ambaye amemaliza muda wake wa utumishi March 31,2013.

Wasifu wa Luteni General Paul Ignace Mella unaelezwa kuwa ni Mwanajeshi wa muda mrefu na mwenye uzoefu na utumishi uliotukuka katika JWTZ akiwa amewahi kushika nyadhifa mbali mbali muhimu za uongozi.

Baadhi ya nyadhifa hizo ni pamoja na Naibu Kamanda Kikosi cha Tanzania chini ya Umoja wa Mataifa huko Liberia ( 1993-95), Kamanda wa Kikosi cha JWTZ, Afisa Mnadhimu-Makao Makuu ya Jeshi, Mwambata Jeshi-Ubalozi wa Tanzania Uganda na hadi sasa alikuwa ni Mkuu wa Usalama na Utambuzi- JWTZ.

Uteuzi wa Lt. Generali Mella unafuatia mchakato mrefu ulioshindanisha wateuliwa kutoka nchi mbalimbali duniani, na hatimaye yeyé akaibuka mshindi.

Post a Comment

أحدث أقدم