MFANYAKAZI wa Jaji Kileo, Philemon Laiza (27) anadaiwa kumchinja mtumishi wa ndani wa jaji huyo, ambaye ni raia wa Kenya, Perpetua Mainab (30).
Mtuhumiwa huyo, ambaye alikuwa ni mtunza bustani katika nyumba ya Jaji Kileo, alifanya unyama huo wiki iliyopita.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum, Suleiman Kova, alisema mwili wa mtumishi huyo wa ndani ulikutwa kwenye dampo la kutupia takataka maeneo ya Mikocheni B.
“Tukio hilo lilitokea karibu na dampo la kutupia taka Mikocheni ‘B’, katika eneo linalomilikiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
“Mfanyakazi huyo wa ndani alikutwa ameshakufa baada ya mwili wake kuchinjwa sehemu ya shingo, jeraha sehemu ya mkono wa kushoto karibu na kiganja, jeraha kwenye paji la uso na mwili wake ukiwa umetapakaa damu sehemu za kichwani,” alisema Kova.
Alieleza kuwa mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akifanya kazi pamoja na marehemu, alikiri kuwa na marehemu siku hiyo ya Ijumaa ya Juni 8 mwaka huu.
Alisema baada ya polisi kufanya upelelezi mtuhumiwa alikutwa na kiatu kimoja cha marehemu na nguo alizovaa siku ya tukio, ambazo zilikuwa zimetapakaa damu.
“Nguo hizo za marehemu zilikuwa zimetapakaa damu na baada ya mahojiano ya muda mrefu, mtuhumiwa alikiri kuhusika na tukio hilo.
Kamishna Kova alisema kuwa mtuhumiwa alipohojiwa alidai kuwa marehemu alitoweka nyumbani tangu siku ya Ijumaa na baada ya kubanwa na polisi mtuhumiwa alikiri kuhusika na tukio hilo.
Kova alisema mtuhumiwa bado anahojiwa na upepelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani
إرسال تعليق