DAR ES SALAAM, Baada ya miaka 10 ya ‘ndoa’ kati ya kipa Juma Kaseja na Simba ya
Dar es Salaam, klabu hiyo ya jezi nyekundu na nyeupe kutoka Mtaa wa
Msimbazi imetangaza rasmi kuachana naye.
Kaseja alisajiliwa Simba mwaka 2003 akitoka klabu
ya Moro United, na tangu wakati huo alikuwa kipa tegemeo wa Simba kwa
misimu tisa akiiwezesha kutwaa mataji kadhaa ya Ligi Kuu.
Katika kipindi chote cha kucheza Simba, Kaseja
ambaye pia ni nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), ni
mara moja tu mwaka 2009 alijiunga na mahasimu wakubwa wa Simba, Yanga na
kucheza msimu mmoja.
Uamuzi wa kuachana na Kaseja ulifikiwa na Kikao
cha Kamati ya Ufundi kilichoketi juzi na jana na kuamua kutoendelea naye
tena baada ya mkataba wake kumalizika.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Danny Manembe alisema
jijini Dar es Salaam jana kuwa, klabu yao ina makipa watatu wapya, hivyo
hawana tena sababu ya kuendelea na Kaseja.
Makipa waliopo Simba kwa sasa ni Abel Thaira,
Andrew Ntala aliyesajiliwa kutoka Kagera Sugar na Abuu Magube
aliyepandishwa kutoka kikosi B.
“Tuna makipa watatu, hawa ni wengi sana kwetu.
Hatuwezi tena kuongeza kipa mwingine, hivyo Kaseja tunaachana naye,”
alisema Manembe. Akiongeza, Manembe alisema kocha mpya wa Simba,
Abdallah Kibadeni katika orodha ya wachezaji anaowataka kwa ajili ya
msimu ujao, hakumjumuisha Kaseja hivyo na wao wameamua kuachana naye.
Muda mfupi kabla ya Simba kutangaza uamuzi huo,
Mwananchi iliwasiliana na Kaseja ambaye alisema: “Sitaki kuzungumzia
habari za Simba kwa sasa, nina mambo mengi muhimu nataka kuyafanya.”
Itakuwa mara ya kwanza kwa Simba kuanza msimu wa
ligi bila Kaseja kwa miaka tisa, huku kipa huyo pia akiweka rekodi ya
kucheza mechi nyingi za watani, ambapo mpaka anatemwa ameshasimama
longoni mechi 25.
Post a Comment