Ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama, umesababisha wafanyabiashara ndogo ndogo, maarufu kama machinga kutimuliwa katika maeneo kadhaa ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam ikiwa ni hatua ya kuliweka jiji hilo katika hali ya usafi.
Jana asubuhi Halmashauri ya Wilaya ya Ilala iliendesha operesheni kubwa ya kuwaondoa wamachinga katika maeneo hayo, sambamba na vijana wanaojihusisha na shughuli zinazosababisha uchafuzi wa mazingira.
Katika operesheni hiyo iliyowashirikisha mgambo na polisi, machinga 21 walitiwa mbaroni na wanaendelea kushikiliwa kwa makosa ya kufanya biashara maeneo yasiyoruhusiwa.
Manispaa ya Ilala, imethibitisha kuwapo kwa operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara hao na kufafanua kuwa inalenga kusafisha mazingira kwa kuwa kuna ugeni mkubwa wa kiongozi huyo wa taifa kubwa na lenye nguvu za kiuchumi na kijeshi duniani.
Baadhi ya wafanyabiashara wamelalamikia hatua hiyo kwa madai kuwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kufanyia biashara hayana wateja na hivyo kulazimika kuwafuata wateja.
Afisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Tabu Shaibu, alisema operesheni hiyo ni endelevu na inalenga kufanya usafi katika Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la mkuu wa mkoa huo, Said Sadiki, la kusafisha jiji.
“Si utamaduni mgeni anapokuja nyumbani kwako ni lazima ufanye usafi wa hali ya juu, na operesheni yetu imelenga kuwafanya watu kupenda usafi, lakini pia tunajiandaa kwa ajili ya ugeni wa Obama,” alisema.
Shaibu alisema operesheni hiyo imefanywa kwa ushirikiano na polisi na mgambo wa manispaa kwa lengo la kushughulikia kero za wananchi ambao wamekuwa wakishindwa kutembea kwenye maeneo husika kutokana na wafanyabiashara hao kuziba njia.
“Kuna mama lishe, wauza nguo, bidhaa za sokoni, wasafisha viatu ambao wamesajiliwa kufanyakazi hiyo, lakini wameongeza bidhaa nyingine,” alisema.
Alisema waliokamatwa watatozwa faini ya Sh. 50,000 kwa mujibu wa sheria za mipango miji na kuongeza kwamba watakaoshindwa watafikishwa mahakamani.
Alisema ni lazima sheria za mipango miji zifuatwe kwa kila eneo kufanya kazi iliyokusudiwa na si kila mtu kujiamulia kubadili matumizi ya eneo fulani.
Alisema kabla ya kuanza operesheni hiyo, Juni 14 na 15, mwaka huu, manispaa ilitoa tangazo la kuwataka waondoke kwenye maeneo hayo na kwamba baadhi walitii na wengine walikaidi.
Baadhi ya wafanyabiasha Bakari Ally, Abdalah Sharif, Yusuph Mzee na Eric Hosea, waliliambia NIPASHE kuwa wanalazimika kufanyabiashara maeneo hayo kwa kuwa ndipo kuliko na wateja.
Sharif alisema maelezo kuwa wanachafua mazingira siyo sahihi kwa kuwa biashara ya nguo na viatu haisababishi uchafu.
“Biashara hii ndio tegemeo kwa ajili ya kulisha familia yangu, amri imetolewa ila siwezi kukaa nyumbani nalazimika kufanya kwa kujificha,” alisema Hosea na kuongeza: “Ujio wa Obama usigeuke kero kwa sisi wazawa.”
Sharif ambaye alikutwa akiendelea na biashara ya viatu, alisema analazimika kufanya hivyo kwa woga kwa kuwa ana wateja wengi eneo hilo na amekopa fedha kupata mtaji wa biashara hiyo ambayo inahitaji marejesho kila wiki.
“Tunaishukuru serikali imetutengea maeneo ya Karume, Ilala na kwingine, lakini kumeshajaa, tunakosa wateja na tunalazimika kuwafuata wanaotoka maofisini,” alisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marietha Komba, alisema operesheni hiyo pia inalenga kukamata wauzaji na wavuta bangi ambao hupora mali za wananchi nyakati za mchana na jioni.
Rais Obama anatarajiwa kuanza ziara ya kutembelea nchi tatu za Afrika za Senegal, Tanzania na Afrika Kusini kuanzia mwishoni mwa Juni hadi mwanzoni mwa Julai.
CHANZO: NIPASHE
إرسال تعليق