Ratiba ziara ya Obama hadharani, kukaa siku mbili

 
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Ikulu ya Marekani na Idara ya Habari (Maelezo), wametangaza ratiba ya Rais Barrack Obama atakapozuru Tanzania huku ikionyesha kuwa atakaa siku mbili tu, kuanzia Julai Mosi na kuondoka kesho yake.
Tanzania itakuwa nchi ya mwisho ya Afrika kutembelewa na Obama baada ya Senegal na Afrika Kusini. Mara atakapowasili na ndege yake kubwa ya Air Force One, Rais Obama atazindua barabara mpya katika upande wa Mashariki wa geti la kuingia Ikulu.
Rais Obama, ambaye atafuatana mkewe Michelle pia siku hiyohiyo atazungumza kwa nyakati tofauti na  wafanyabiashara kutoka nchi za Afrika na Marekani kwenye Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam.
“Pia amepanga kuzungumza na maofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania,” ilisema taarifa ya Maelezo.
Baada ya shughuli hiyo, Rais Obama atahudhuria dhifa ya taifa atakayoandaliwa Ikulu na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete. Siku itakayofuata ataweka shada la maua kwenye sehemu ulipokuwa Ubalozi wa Marekani ikiwa ni kumbukumbu ya watu waliofariki katika shambulizi la bomu mwaka 1998. Pia atatembelea mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Symbion na atatoa hotuba akizungumzia mikakati ya Marekani ya kulisaidia Bara la Afrika kuzalisha nishati ya umeme.
“Tanzania ni mshirika muhimu wa Marekani,” alisema Ofisa wa Ikulu ya Marekani, Ben Rhodes wakati alipozungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki katika Ikulu ya Marekani kuhusu ratiba ya ziara ya Obama barani Afrika.
Pia mke wa Obama atakuwa na ratiba yake. Julai Mosi, atapata staftahi na mwenyeji wake, Salma Kikwete katika ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), Dar es Salaam.
Pia atatembelea sehemu ubalozi wa zamani wa Marekani na baadaye atashuhudia onyesho la utamaduni la Kikundi cha Baba wa Watoto, ambacho kinajumuisha watoto wa mitaani wenye umri kuanzia miaka mitano hadi 18 kwenye Makumbusho ya Taifa. Julai 2, atahudhuria mkutano na wake wa marais wa nchi za Afrika ambao pia utahudhuriwa na mke wa Rais wa zamani wa Marekani, George Bush, Laura.

Post a Comment

Previous Post Next Post