RIWAYA: ROHO MKONONI 1




RIWAYA: ROHO MKONONI.

MTUNZI: GEORGE IRON MOSENYA

Sms: 0655 727325

SEHEMU YA KWANZA.

Malumbano yaliendelea, ilikuwa kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya usichana kujikuta katika mkwaruzano na wazazi wake wote wawili,tena wote wakiwa wanayapinga maamuzi yake aliyokuwa amefikia. Ni kweli alikuwa na umri mdogo na hakudanganywa na mzigo wa matiti ulioanza kujaa kifuani pasina kumtia kero. Bado aliamini ana hadhi ya kuitwa ‘mtoto’ maana aliwategemea wazazi wake kwa kila kitu. Lakini katika jambo hili aliamua kusimama kidete kujitetea.
Mama alikuwa haamini anachokisikia na mzee Kisanga n’do alikuwa akihisi yu ndotoni.
“Mama…” aliita kisha akageuka na upande wa pili akiwa wima, “Baba….nawaheshimu sana na hilo wote mnalijua….lakini naomba katika hili muielewe azma yangu…muwe na utu katika hili baba…hivi leo Betty akifikia hatua ya kuwa yatima tutakuwa na furaha gani? Ndio undugu huu tunaojisifia kila kukicha. Undugu wa kushindwa kufanya jitihada kidogo tu kuokoa uhai….” Aliongea kwa huzuni kuu, sauti yake ikipambana na mikwaruzo.
“Mama Joyce….mwanao huyo.” Mzee Kisanga alimwambia mkewe katika namna ya kushutumu. Kisha akasimama ili aweze kuondoka.
“Baba Joyce mume wangu, yaani leo hii amekuwa mwanangu na si mtoto wetu heee! Makubwa mbona haya.” Mama Joyce aliduwaa. Mzee Kisanga hakujibu lolote, akaingia chumbani kwake.
Baada ya dakika kadhaa ulisikika mchakato wa baiskeli ikiegeshwa nje ya nyumba yam zee Kisanga.
“Kaka yake huyo labda aongee naye vizuri, mimi sitaki kuamshwa na upuuzi wenu.” Mzee Kisanga kutokea chumbani alizungumza. Joyce na mama yake wakasikia. Walikuwa wanatazamana tu kama majogoo yaliyopigana na kukosekana mshindi sasa yamekosa la kuamua mshindi.
“Ehee! Joy Joy mdogo wangu nini tena? Umekuwaje kwani eeh …mama Shkamoo.” James kwa papara na kiherehere alianza kuzungumza huku akitumia kiganja cha mkono wake kujifuta jasho. Alikuwa amevaa mavazi yaliyotangaza dhiki kuu.
Joyce hakujibu kitu, mama yake akaamua kuzungumza.
“Ameng’ang’ania sasa hatujui tumfanyeje tena.” Alisema kwa upole. James akaketi jirani na Joyce ambaye ni mdogo wake toka nitoke.
“Joyce mimi sina elimu hakika, hata hilo darasa la saba sikumaliza mdogo wangu, lakjni hilo jambo unalotaka kufanya dadangu litakugharimu maisha Joy, hivi unataka mama na baba waanze kupalilia mashamba wenyewe ama shida yako umuue baba kwa presha. Joy kama chumvi inakosekana humu ndani, tutaitoa wapi pesa ya kukupeleka hospitali kwa ajili ya tiba. Hakuna serikali hapa Ukala nadhani unajua ni sisi kama sisi. Joy utatutia wazimu, mtoto wangu huko anaumwa nimeshindwa hata kupata shilingi ya kumnunulia Panado. Joy katazame nimenyonga baiskeli isiyokuwa na upepo ili nije huku mdogo wangu, tuhurumie basi. Eeh! Mambo mengine tumwachie Mungu….unanielewa kadadaa” James alimaliza kwa kumuita jina lake la utotoni. Jina ambalo humfanya Joyce atabasamu lakini siku hiyo hakutabasamu, hakika hali ilikuwa tete.
“Mama!” Joyce aliita. Mama yake akanyanyua kichwa na kumtazama, Joyce akawahi kukwepesha macho hakupenda kumtazama mama yake akiwa anatokwa machozi. Kisha akaendelea, “Unakumbuka siku ile shambani……ulipojikata na jembe tukiwa tunalima?”
“Nakumbuka mwanangu.”
”Mimi sikuwepo…..ni nani aliyefanikisha wewe kufika hospitali.”
“Ni Betty lakini…”
“Hakuna lakini mama niache niendelee kuongea…..” Joy aligeuka mbogo. “Ni Betty na la kuongezea ni kwamb a alitumia ile pesa yake ya ada kulipia huduma hospitali. Nani anajua kama wazazi wake walimtukana, nani anajua kama pesa ile ndo ilikuwa akiba pekee ya wazazi wake?” alihoji. Hakuna aliyemjibu, wote walikuwa katika hamaniko.
“Mtumbwi wa baba ulipovunjika ziwani, wavuvi waliozama kumtafuta ni ndugu zake…ina…” kabla hajaendelea sauti nzito ya kukaripia kutoka chumbani ilichukua hatamu.
“Joyce nitakupiga bakora…nitakuharibu sura yako malaya wewe…nasema sitaki uniunganishe katika upumbavu wako huo..tena Joy ukome nasema…” Kimya kikatanda mzee Kisanga alikuwa ametetemesha.
“Baba Joy usimuite mtoto Malaya lakini nini baba….”
“Na wewe kimya pumbavu kabisa wewe na mtoto wako tena unganikeni basi tuone kama mtanipunguzia chochote, kwa hiyo mnafichiana tabia zenu sivyo….”
Wakati mama na kaka yake Joyce wakiwa wameinama bila kujua nini cha kufanya, mzee Kisanga akiendelea kupiga makelele. Joyce alisimama kwa unyonge kama asiyekuwa na mipango yoyote kichwani, kwa kumtazama alikuwa ameathirika na kauli za baba yake. Mama yake akanyanyua kichwa akamtazama.
Kilichofuata hapo hakuna ambaye alitarajia kingeweza kutokea. Ulisikika mchakato wa mara moja. Walipochelewa kwa sekunde kadhaa walikuwa wamempa nafasi Joyce. Nafasi hadimu kabisa.
“We Joy wewe….njoo hapa nikikukamata Joy njooo!!” James, kaka yake Joyce alipiga kelele za hamaniko wakati Joy akionekana kwa mbali akiinyonga baskeli huku akiwa amesimamia. Mwendokasi alioondoka nao ni wanawake wachache wanaweza kuumudu.
“Nini? Amekuwaje eeh!” sauti ya mzee Kisanga ikaingilia mshangao wa mama na mwana. Wakageuka na kumtazama bila kumjibu kitu chochote.
Akatukana kikerewe huku akiingia ndani na laana zake zisizokuwa na mlengwa. Joyce alikuwa ametoweka.
“Wewe na wewe…..nawapa masaa matatu aaah manne..namtaka mwanangu hapa….”
Maajabu sio huyu alisema yule Malaya ni mtoto wa mama yake!!
Mama Joyce na mtoto wake wa kiume wakastaajabu, lakini hawakusema lolote kwani tabia ya mzee Kisanga waliijua fika.
Wakatoweka bila kuwa na uelekeo maalum. Huku kila mmoja akijitahidi kulaani kitendo hicho kuliko mwenzake.

****

Uguma wa maisha katika kisiwa cha Ukala wilaya ukerewe haikuwa simulizi mpya. Sema ilikuwa haizoeleki, si kwa wageni wala wazawa. Wapiga kura walitegemea kushibisha matumbo yao kwa uvuvi mdogomdogo ambao viongozi waliuita haramu, kilimo nacho hakikuwa uti wa mgongo wa maendeleo na badala yake mavuno yaliyopatikana yalitumika kama chakula tu baada ya mahindi kusagwa na jiwe la mkono na kuwa unga wa kupikia ugali na uji kwa watoto wadogo. Huduma za kiafya zilikuwa mbali sana huku wakazi wengi wa kisiwa hicho wakitegemea hospitali ya Murutunguru ambayo ilikuwa maalumu kwa ajili ya wanachuo na wanafunzi wa shule za sekondari Murutunguru.
Licha ya huduma hizi mbovu ambazo zilionekana ubovu wake katika kipindi cha kampeni na mikutano ya kisiasa, bado wananchi walitembelewa na wageni waliojiita wataalamu na kuwahusia kuhusu kutoa damu kwa lengo la kusaidia ndugu zao na pia kwa akiba ya siku za usoni iwapo watakumbwa na jambo lolote litakalohitaji damu.
“Changia damu sasa kwa uhai wako na wa jamaa zako” hiyo ilikuwa kauli mbiu iliyokaririwa hassahasa na watoto wa shule za msingi ambao viatu kwao vilikuwa anasa.
Wazawawakajipanga foleni na kutolewa damu hasahasa baada ya kupimwa uzito. Betty na Joyce walikuwa kati ya wasichana wachache waliohamasika na tungo hizo za kuburudisha kutoka kwa wataalamu. Walihamasika kwa sababu walikuwa na kumbukumbu ya baba yake Betty kupoteza uhai kwa kupungukiwa damu mwili, ikakosekana damu ya ziada ya kuongezewa. Baba yake Betty akaaga dunia huku akilalamika kuwa anakufa kwa sababu ya umaskini.
Laiti angekuwa na pesa angekimbizwa mkoani Mwanza, huko angepata tiba madhubuti na hakika asingepoteza uhai.
Kwa hiari yao huku wakitabasamu wakajitolea damu kwa ajili ‘yao na ndugu zao’. Lile tabasamu likatoweka zilipoanza kusikika tetesi kuwa wagonjwa wanauziwa damu kila wanapohitaji huduma hii.
Ina maana hawa si ndugu zetu!! Betty na Joyce walijiuliza.
Nani angewajibu……
Lisilokufika huwezi kulijua uchungu wake hadi likukumbe moja kwa moja.
Zile tetesi kuwa damu ianuzwa tena kwa bei ghali; hazikuwa tetesi tena, mama yake Betty alikuwa matatani. Upungufu wa damu ulikuwa umemuweka katika kitanda cha zahanati ya kijiji.
Lilikuwa tukio la kushangaza ambalo lilianzia shambani mfanowe tamthilia ya kufikirika.

"Uuuuuuwiii" kilio kikali kilisikika kutokea shambani walipokuwa wanalima ilikuwa sauti ya mamake Betty akitoa kilio cha uchungu tena uchungu mkali..
"Mamaaaa weeeee nakufaaaa" alipiga kelele huku akiliachia jembe lake, Betty alisikia kilio kile cha mtu mzima mbio mbio kuelekea alipokuwa mama yake huku Joyce naye akifuatilia nyuma kwa kasi lakini ajabu yeye (Joyce) ndiye aliyewahi kufika kabla ya Betty.
Mama Betty alikuwa chini akilia kwa maumivu makali, damu ilikuwa inaruka juu kama mkojo wa mtoto mdogo aliyekuwa amebanwa muda mrefu na sasa uvumilivu umemshinda akawa ameuachia, jembe lilikuwa limejeruhi mguu wa mama Betty, bila kupoteza muda huku Betty akishangaa Joyce alivua blauzi yake ambayo zamani lilikuwa jeupe kwa ajili ya shule lakini sasa lilikuwa na rangi ya vumbi kutokana na shughuli za kilimo huku likiwa limechanika makwapani, alipolivua akabakiwa na sidiria ya njano iliyofubaa aakaizungusha kwenye mguu wa mama Betty kwa ustadi mkubwa kisha akashauri wajikongoje kwenda nyumbani kwa msaada zaidi.
"Hapana Joyce, najiskia vizuri naweza kuendelea kulima." mama Betty alisema kwa sauti ya chini huku akiukunja uso wake kukabiliana na maumivu ya jeraha lile.
"Hapana mama hapana hiyo damu haijakatika hata kidogo inaendelea kuvuja, twende walau tukaweke chumvi kidogo itasaidia japo kukausha" Joyce alipinga vikali akisaidiwa na Betty, wote hawa walitumia taaluma yao ndogo waliyopata katika somo la sayansi walipokuwa shuleni, mama hakuwa na la kupinga walielekea nyumbani huku ile shati aliyofungwa mama Betty ikizidi kuwa nyekundu. Wekundu wa damu!!
Walipokelewa na wazazi wa Joyce kwa huzuni huku kila dakika mama Betty akitoa shukrani kwa Joyce kwa ukarimu na huruma aliyoonyesha kwake. Mguu wa mama Betty ulipofunguliwa hali haikuwa shwari bado damu ilikuwa inavuja kudhihirisha jembe lilikata mshipa mkubwa wa damu, hata chumvi aliyowekewa haikusaidia kitu zaidi ya kupotelea kwenye dimbwi la damu kimaajabu. Ilistaajabisha hakika!!
"Nahisi nachoka na ninaishiwa nguvu….nahisi kizunguzungu jamani" alitoa kauli hiyo ya kushtua mama Betty ambaye alikuwa amejikaza kwa muda mrefu, hali iliyozusha hofu kwa kila mtu. Ilikuwa lazima wahofie kwa sababu vifo mfululizo vilitokea katika namna hiyo ya kustaajabisha.
Bila kuaga Joyce alichomoka mbio na kurejea baada ya dakika 20 akiwa na baskeli, alikuwa anahema juu juu, jasho likiwa linamtiririka.
"Twende hospitali" aliomba Joyce na wote wakatii amri mama Betty akapandishwa kwenye baskeli
"Sidhani kama nitafika" alianza kulalamika jambo ambalo lilimrejesha Betty kwenye kumbukumbu ya kifo baba yake alijisikia upweke sana kwa mara nyingine alikuwa anataka kukubali mama yake afe kizembe, Joyce hakuacha kumfariji na kumtia moyo.
****
Ilikuwa kama bahati usafiri wa mtumbwi kuvuka visiwa vya Ukara kuelekea Ukerewe ambao zamani ulikuwa wa tabu sana kutokana na wavuvi kuwa bize na zoezi la kuvua samaki na dagaa muda wote lakini tangu serikali ipandikize kampuni ya kigeni ya "Fisheries" kutoka Uswisi ambayo ilitawala maeneo yote yaliyosifika kwa kuwa na wingi wa samaki wavuvi wazaliwa wa hapo hawakuwa na shughuli za kufanya tena, hali ilikuwa ngumu sana. Hivyo mitumbwi yao wakaigeuza matumizi na kuwa ya kuvushia maskini wenzao. Kisiwa kimoja kwenda kingine.
Ujio wa akina Betty na mgonjwa wao ilikuwa kama bahati ya mtende walipokelewa kama wafalme na kugombaniwa kama mpira wa kona tena katika dakika za majeruhi, gharama za mtumbwi uendao kasi kwa sababu ya kuwa na injini, shilingi 5000 iliwashnda hivyo iliwalazimu kuchukua mtumbwi wa kawaida wa makasia ambao kulingana na hali ya mama Betty ilikuwa ni kama kucheza bahati nasibu.
Bahati na sibu na roho ya mwanadamu!!
"Mungu atakuwa nasi" baba Joyce aliwaambia wenzake wakati wakiijiandaa kupanda ndani ya usafiri huo.

"Mama Joyce wewe rejea nyumbani ukatazame watoto na mji mimi na Joyce tutaongozana na Betty huko Hospital. Alianza kupakiwa mgonjwa, baadaye baiskel na kisha wakapanda watatu hawa kwenye mtumbwi ambapo wapiga makasia wawili walikuwa wametangulia.
Mtumbwi wa kubeba watu wanne ulikuwa na idadi ya watu sita sasa. Utata!!
"Ee Mungu weka mkono wako katika safari hii" Lilikuwa ombi la Joyce wakati mtumbwi ukiachia nanga yake.na makasia kuanza kupigwa kwa kasi sana. Alijua kuwa walikuwa katika hali ya hatari lakini wangefanya nini kama serikali haikuwa ikijali lolote kuhusu wao.

* * * *

Baba yake Joyce alinyonga baiskeli kwa kasi, mgonjwa akiwa ameshikilia kiti cha mbele kwa nguvu sana. Joyce na Betty walifuata kwa nyuma mbiombio kwa miguu huku wakiwa peku wote hawa dhumuni lao kufika mapema katika kituo cha afya cha Murutunguru.
Pancha katika matairi yote haikuzuia safari kuendelea. Ilikuwa ni bora kuacha kuziba pancha lakini wawahi kufika hospitali. Nguvu zilikuwa zinazidi kumwishia Mama Betty japo damu zilikuwa zimekatika sasa kama ni kweli zilikuwa zimekatika. Huenda zilikuwa hazijakatika bali zilikuwa zinaelekea kuisha mwilini.
Saa tisa alasiri walikuwa tayari chumba cha daktari, Joyce na Betty wakiwa hoi kwa kukimbia mwendo mrefu sana bila kupumzika wakati mama Betty alikuwa amepewa dawa aina ya PPF kwa ajili ya kukausha damu na Panadol kwa ajili ya kupunguza maumivu, hizo ndio dawa zilizopatikana hapo pamoja na Asprin, pilton na dawa mseto za malaria kwa uchache. Kwa waliotoka mjini wangejiuliza kama eneo hilo lina mwakilishi bungeni.
"Mgonjwa wenu anaupungufu mkubwa wa damu na ni hatari kwa maisha yake" aliongea daktari huyu ambae vazi lake jeupe lilikuwa limechakaa sana huku likiwa na matundumatundu kama limeliwa na Panya.
"Na kituo chetu hakina akiba ya damu mpaka Bugando Mwanza"
"Kwa hyo tunatakiwa kufanya nini?" alihoji.
"Kama hamwezi kwenda Mwanza kuchukua au kama yupo wa kujitolea atoe kuokoa maisha yake"
"Nitajitolea mimi" alijibu haraka Baba Joyce.
"Damu yako ni kundi gani??" aliuliza daktari.
"Mh! sifahamu kwa kweli" alijibu

"Haya nifate huku ukapime kwanza" palepale alisimama daktari akifuatiwa kwa nyuma na Baba. Joyce hadi chumba chakavu kilichoandikwa kwa kutumia mkaa "MAABARA"

"Mgonjwa wenu kundi 'O' na wewe ni kundi 'B' haiwezekani hata siku moja" alitoa majibu daktari baada ya kuipima damu ya mgonjwa na baba Joyce.
"Tunafanya nini sasa tena Daktari?" alirudia kuuliza lile swali tena baba Joyce
"Ni kama nilivyokwambia agiza kutoka Mwanza" alijibu kwa ukali wakati huu. Kijasho chembamba kikamtiririka babake Joyce, wakati huo Betty na John walikuwa mlangoni wakisikia maongezi yanavyoendelea.
"Sasa....aah! Mwanza mh!"
"Ndio ni shilingi elfu thelathini tu chupa moja…." daktari alimwambia huku akikunakuna kichwa chake chenye mvi. Kisha akamalizia, “Nadhani hiyo itamwongezea siku za kuishi.”

"Kama shilingi 5000 ya imetushnda itakuwa 30000?" alijiuliza baba Joyce huku akisimama na kutoka nje ambapo aliwakuta Betty na Joyce. Hakuwa hata na la kusema zaidi ya kuwakodolea macho yaliyokata tamaa kabisa.
"Basi mimi nina dadu ya kundi 'O' niruhusu nitoe" alisema Joyce kwaq kiherehere akikumbuka majibu aliyopewa juu ya kundi la damu yake siku alipojitolea damu, jambo ambalo mzazi wake alipinga vikali kwa kuhofia usalama wa mwanae huyo mkubwa kutokana na umri wake kuwa mdogo..
Mgogoro ukaanzia hapa na kusafiri hadi nyumbani, wazazi wakipingana na Joyce. Joyce akisimamia msimamo kuwa anaweza kutoa damu na kumwokoa mama yake Betty….
Huu ukawa utata ulioishia katika mtafaruku, Joyce akakimbia na baiskeli akiwaacha mama na kaka yake wakitukanwa……
Akakimbilia alikotambua yeye na akili yake………

*****

***JE? Baada ya mgogoro na wazazi wake…JOYCE amekimbilia wapi na ile baiskeli?? Na anataka kufanya nini ambacho wazazi wake wanampinga???

***BETTY amefiwa na baba yake tayari je mama yake naye anafuata??

** FUATILIA kisa hiki na ujifunze mengi sana yenye umuhimu katika maisha yetu ya sasa….

## BOFYA LIKE BUTTON Iwapo tumeanza pamoja safari hii ya riwaya mpya……

NINI KITAENDELEA KATIKA ROHO MKONONI…..FUATILIA KESHO..

Post a Comment

أحدث أقدم