RIWAYA: ROHO MKONONI 9


RIWAYA: ROHO MKONONI


MTUNZI: George Iron Mosenya

SEHEMU YA TISA

“Vipi jamaa keshaacha kukusumbua siku hizi…maana kimyaa au ndo tayari na wewe…ushadata.” Betty alimchokoza Joy wakiwa kitandani.
“Aaargh asingeweza kunipata kirahisi, ameuchuna siku hizi aibu kwake…ananitishia mimi pesa ananitishia majivuno.” Alijibu Joy kwa jeuri huku akiibetua midomo yake.
“Na hicho kidoti wanakomaje!!!” 
Wakacheka kwa pamoja!!! 
Mara simu ya Betty ikaita akaipokewa, alikuwa bwana mmoja mfanyakazi wa benki.
“Mi natoka shoga!!.” Alimuaga Joyce wakati anajiandaa kwenda kwa bwana mwingine.
“Huyu ananipa laki tano leo, nakaribia kufikisha milioni nne dah safi sana. Na roho saba zipo rehani tayari pumbavu zao.” Alibwabwaja huku akitangaza chuki ya waziwazi.
Akaondoka zake!!!

****
HAKIKA Isaya mtoto wa Akunaay alikuwa amepatikana kwa mara ya kwanza katika uwanja wa mapenzi, alijaribu kufikiria na kuweka picha za wasichana lukuki ambao aliwahi kuwanao katika mapenzi na kisha kuwaacha solemba.
Alijiuliza kama kuna msichana walau mmoja ambaye amewahi kumuumiza kichwa aidha katika kumpata kimapenzi ama la kumwacha. Jibu lilikuja upesi tu, jibu la HAPANA.
Hapa Isaya akatabasamu kidogo na kisha kujiona yeye ni wa pekee sana na hana hadhi ya kukataliwa na msichana yeyote aidha ndani ya chuo ama nje ya chuo hicho.
Lakini sasa mbona anaumia kichwa iwapo yeye ni wa pekee?? Swali hili lilimvamia katika namna ya kumfadhaisha katika namna ya pekee. Alitambua nini maana ya swali lile, akajaribu kulikwepa jibu lakini haikuwezekana akaamua kukiri kuwa, Joyce alikuwa pekee zaidi yake. Maana yeye na upekee wake anaouamini amejikuta akiumia kichwa kwa sababu ya msichana huyo.
“Kama ni wa kipekee zaidi lazima atulizwe kipekee huyu.” Alipata wazo hilo, lakini wazo hili likajijenga na swali jingine. Nini maana ya kumtuliza mtu kipekee…..

Ghafla akamkumbuka, Joseph Matanuru, huyu alikuwa ni rafiki yake ambaye walikuwa hawachangamani sana kwa sababu ya kutofautiana mitazamo yao. Isaya akiwa mtu wa starehe na Matanuru akiwa hapendi kujirusha.

Kilichoendelea kuwaunganisha ni ule uenyeji wao wa Geita, walikutana huko kipindi cha likizo hivyo wakawa kama ndugu.
Matanuru alikuwa na maadui wengi kuliko marafiki kutokana na kupendq kusema ukweli. Ukweli unaoumiza lakini kila aliyeambiwa alikiri moyoni kuwa Matanuru alikuwa sahihi, hali ikamfanya Matanuru kuwa na maadui lakini wasioonyesha chuki waziwazi.
Isaya alikuwa mmoja kati ya waathirika wa maneno ya Matanuru. Kila mara alipozungumza naye alikuwa akimshauri mambo mengi. Yalikuwa na ukweli lakini starehe zilikuwa zimemtawala Isaya na kamwe asingeweza kubadilika.

SASA kwa mara ya kwanza Isaya kwa hiari yake mwenyewe anaenda kwa Matanuru kwa ajili ya ushauri, aliyafanya haya baada ya kumaliza kuoga na kubadili nguo zake.

Isaya alijieleza kinagaubaga juu ya tatizo lake. Na kisha akajieleza pia njia anayodhani kuwa ni sahihi kwa ajili ya kumpata Joyce kimapenzi.
Matanuru akatabasamu kisha akasimama na kuanza kutembea kwenda mbele kisha kurudi nyuma katika namna ya kujitamba.
“Isaya….hivi huju kuwa msichana anapenda kunyenyekewa, pia anapenda ufanye yale anayoyataka yeye?? Angalia huyo Kidoti anapenda nini na wewe kipende, hana shida na utajiri wako, hana shida na pesa zako Yule. Kama ni hoteli za kifahari walipokuwa kambi ya kuwania u-miss chuo walienda huko, kama ni magari ya kifahari nadhani kwa urembo wake ameshapewa na kuzikataa ofa nyingi tu….si ndo huyu walienda kupiga picha na Raisi ikulu, sasa unahisia kuwa bado ni mshamba….huyu anakuona wewe mshamba na hizo mbinu unazozitumia. Badili mbinu Isaya halafu……usimchezee Yule mtoto bwana kama kweli unampenda…..” alimaliza mtaalamu wa saikolojia Matanuru. Maneno ya ukweli kama kawaida yakauchoma moyo wa Isaya lakini atafanya nini wakati alihitaji kushauriwa.
Akaondoka kichwa chini mikono nyuma, kichwani akiwa ametingwa na mawazo mazito zaidi…
Isaya alikuwa anaionja ladha ya kupenda kwa mara ya kwanza baada ya kuwachezea wasichana lukuki kwa misingi ya kufurahisha mwili wake. Hakuwahi kujua kupenda ni nini lakini alifahamu ladha ya kutamani na kisha kukipata akitakacho, sasa hali ilikuwa tofauti kabisa.
Isaya akajikuta akikubaliana na maneno ya Matanuru japo kimoyomoyo.

*****

JOYCE KIDOTI alikuwa amejifunika shuka gubigubi kutokana na hali ya hewa kuwa ya ubaridi kiasi, lakini licha ya kujifunika haikumaanisha kuwa alikuwa amelala la! Bali alikuwa anatabasamu peke yake huku akirejea kumbukumbu kadhaa.
Joyce alikuwa akijilazimisha kuamini alichokiona na anachoendelea kukiona, japo hakumshirikisha mtu yeyote furaha hiyo ya aina yake, mastaajabu yakabaki katika akili yake.
Isaya amekuwa mchangiaji katika tamasha la Ukimwi na jinsia? Anavyojivuna yule, duh! Watu wanabadilika sana aisee!! Alijisemea kwa sauti ya juu kidogo.
Hakika si yeye tu aliyejiuliza kuhusu mabadiliko ya Isaya bali hata wanachuo wengine waliokuwa wakimfahamu fika kijana yule walistaajabu, lakini shukrani zote zilienda kwa Matanuru ambaye kwa sasa alikuwa rafiki yake mpendwa na wa karibu kabisa.
Isaya alikuwa ameacha matumizi mabaya ya pesa, alikula katika migahawa ya chuo, alikuwa akivaa kistaarabu na alipunguza kabisa starehe na dharau.
Katika mikutano ihusuyo mambo ya kijamii alishiriki ipasavyo, na kwenye mambo ya kijamii kama kutembelea wagonjwa na kusaidia yatima alitumia vyema ile kofia yake ya kuwa mtoto wa mbunge kusimamia vyema.
Tabia hii ikapenya na kumfikia Joyce ambaye alikuwa na muda mrefu tangu akate mawasiliano na Isaya. Taarifa hizi zilimshtua Joyce hivyo akaamua kuhudhuria kongamano la Ukimwi na jinsia ambalo alisikia kuwa Isaya atakuwa meza kuu kwa ajili ya kutoa mada. Hakika Joyce akamshuhudia Isaya mpya akiwa ndani ya suti nyeusi iliyomkaa vyema, maneno yenye busara yaliyomtoka yaliendana na muonekano wake.
Baada ya kongamano alimshuhudia akisalimia na watu wenye heshima zao na wsalionekana kumsikiliza sana huku wakiona fahari kuwa naye katika kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi mashuhuri wa Nkurumah uliopo ndani ya chuo kikuu cha Dar es salaam.
Joyce naye akavutika kusalimiana na Isaya, hakika aliipata nafasi hiyo hadimu ambayo wengi walionekana kuitafuta kwani kusalimiana na Isaya ilikuwa pia nafasi ya kusalimiana na mtu ambaye Joyce alihisi kumfananisha na kama aliwahi kumwona mahali, alikuwa amechelewa utambulisho wa wahusika wa meza kuu na wageni waalikwa hivyo hakuweza kumtambua mara moja mtu yule lakini akili yake ilimsisitiza kuwa aliwahi kumwona mahali. Wakati Joyce akizidi kupenya kundi la wanafunzi na wanaharakati wengine ili aweze kumfikia Isaya, alishangaa alipoguswa begani, alipogeuka alionana ana kwa ana na Isaya. Kumbe na yeye alikuwa katika jitihada za kumtafuta.
“Za siku Joyce Kidoti….umenitenga wewe.”
“Njema tu bro…masomo si unajua tena halafu tupo kozi tofauti tofauti nd’o maana.” Alijibu Joyce huku akionekana dhahiri kustaajabu kabisa na muonekano huu mpya wa Isaya. 
Kumbe mtanashati eeh!! Alijisemea Joyce. Wakati akipitiwa na wazo hili Isaya alikuwa amekidaka kiganja cha mkono wake na kumwongoza katika kundi la watu huku akiendelea na salamu za hapa na pale zikiongozwa na malalamiko ya kupotezana.
Mara Joyce akapigwa na butwaa, wakasimama mbele ya mwanaume ambaye Joyce alikuwa anamfananisha kama aliwahi kumwona sehemu. Joyce akazidi kuduwaa pale Isaya alipomgonga begani kisha naye akageuka.
“Yes Son!” aliitika yule mwanaume mtu mzima.
“Joyce huyu jamaa anaitwa Akunaay Zingo…”
“Aaaah niite muheshimiwa bwana Isaya..” aliingilia kati katika namna ya utani.
Isaya akacheka kisha akampa cheo chake, “Anaitwa mheshimiwa Akunaay Zingo…..mzee wangu huyu. Mbunge wa Geita” alitoa utambulisho huo kwa Joyce kisha akamgeukia mzee wake.
“Mheshimiwa, huyu anaitwa Joyce kidoti, nd’o mlimbwende wa chuo chetu, pia mwanaharakati mwenzangu, mkishaachia ngazi nyie wazee sisi nd’o tunaingia bungeni sasa. Ana nia name nina nia…” alitoa utambulisho ule bila kumpa nafasi Joyce ya kusema chochote.
“Ohh safi sana, mimi nawabariki sana na ninafurahi iwapo vijana kama ninyi mnapata changamoto na kuwa na akili ya kuthubutu…Joy asante sana kwa kunibadilishia huyu mtu maana alikuwa hashikiki kabisa, usimwache apotee tena.” Mzee Akunaay alisema kauli ambayo ilimfurahisha Isaya huku ikimshtua sana Joy, lakini alitabasamu tu bila kuleta ubishi.
Huyu ndiye alikuwa Isaya mpya na Joyce alikuwa akiduwaa peke yake kitandani wakati huo Betty alikuwa katika hekaheka zake za kutafuta pesa.

MWEZI WA TATU TATA.

Isaya alikuwa ameanza kukata tamaa juu ya lengo lake la kummiliki Joyce kama mpenzi wake. Alikuwa amebadilika haswa lakini bado Joyce alikuwa katika msimamo wake kuwa hakuwa tayari kujiingiza katika mapenzi.
“Isaya kiuhakika kabisa sijawahi kukupenda nisikudanganye.” Jibu hili lilikuwa pigo la mwisho kwa Isaya. Joyce alimwambia waziwazi bila kificho chochote, jibu ambalo lilimkasirisha Isaya na kuhisi hata kujishusha kwake hakukuwa na maana yoyote ile, kujiingiza katika mambo ya kijamii pia hapakusaidia kitu. 
Wapambe hawakuwahi kung’amua Joyce yupo katika mapenzi na nani jambo ambalo lilikuwa likimghafirisha sana. Akajiuliza ana tatizo gani binti yule, urafiki wa kawaida alikubali bila kinyongo na walikuwa karibu mara kwa mara mithili ya wapendanao lakini siri ilibaki mioyoni mwao. Hawakuwa katika mapenzi.
Hali hii ilimchukiza sana Isaya lakini angefanya nini wakati alikuwa akimuhitaji sana Joyce. Akaamua kuendelea kuvumilia. Lakini siku aliyopewa jibu lile alijipanga upya kiakili na kujivua ubwege akaona ngoja ngoja inaumiza matumbo na ile subira haikuvuta heri ya aina yoyote.
Isaya akaamua kufanya jambo jingine, maamuzi ya hasira yakapita kichwani mwake.
Maamuzi ambayo yanazua kizaazaa!!

****

WAKATI Isaya akijikatia tamaa na kuamua kufanya maamuzi mengine, Joyce alikuwa katika mateso ya nafsi. Kuna jambo lilikuwa linamkereketa haswa, alitambua wazi kuwa Isaya ndiye mwanaume pekee anayeweza kujiingiza naye katika mapenzi. 
Moyo wake ulimwambia kuwa ni huyo pekee anayeweza kutii kiu yake na wakadumu kwa muda mrefu. Joyce hakutaka kukumbuka jinsi Isaya wa zamani alivyokuwa na dharau na maisha ya kujikweza. Huyu wa sasa alikuwa mwanaume kamili ambaye aliamini ana vigezo vyote vya kuwa mume.
Lakini kitu ambacho Joyce hakutaka kukurupuka ni kumtamkia wazi kuwa yu tayari kuwa naye kwani alikuwa katika kumpima imani Isaya iwapo ni mvumilivu ama la! 
Hakika Joyce hakuwa akiweza kudumu siku nzima bila kumjulia hali Isaya na mara alipomuona na msichana mwingine moyo wake ulilipuka kwa kwa wivu.

Hapo ndipo alipogundua kuwa yu penzini. Tena penzi haswaa.
Kufikia hapo Joyce alipoigundua hali ile kuwa yeye si chochote bila Isaya akajiapiza kuwa baada ya kufanya mtihani wa kumaliza mwaka wa pili wa chuo atamfanyia shtukizo la aiana yake Isaya kwa kumweleza kuwa yu tayari kuwa naye katika uchumba na kisha ndoa iwapo itawezekana.
Ahadi hii ikaendelea kuishi na Joyce bila kumshirikisha mtu mwingine. Angeweza kumshirikisha Betty lakini Betty huyu wa sasa anayewachukia wanaume angemshauri kitu gani??
Maisha yakaendelea!!!
Hadi ilipokuja ile siku ya utata katika mwezi wa tatu.

****

Isaya alikuwa amepata majibu juu ya uwepo wa msichana mwingine jirani na Joyce ambaye ni rafiki kipenzi kabisa. Taarifa hii ilimfanya Isaya ajikute katika maamuzi yenye utata, maamuzi ya kulipiza kisasi.
Kisasi cha kukataliwa na msichana maskini anayeringia urembo wake, msichana aitwaye Joyce.
Isaya akaamua kubadili uelekeo wake akaamua kuhamishia nguvu zote kwa huyo msichana anayesemekana nkuwa yupo jirani sana na Joyce japo haijulikani kama ni mwanafunzi ama la! 
Isaya akaipanga siku, akawaagiza wale wapambe wake wa zamani wakamweka sawa yule binti bila Joyce kujua, binti akachukuliwa na kisha kukutanishwa na Isaya maeneo ya Mlimani City.

Moyo wa Isaya ukasukuma damu kwa kasi, kisha akashusha pumzi kwa nguvu yule binti alivyopiga hatua akiongozana na wapambe wawili kuelekea alipokuwa ameketi.
Dhahabu kutoka Geita!! Isaya alijisemea huku picha ya Joyce iukifutika upesi kama maandishi katika karatasi inayoungua.
“Naitwa Betty….” Alijitambulisha yule binti.
“Naitwa Joram…” alidanganya Isaya huku macho yake yakiushuhudia mwanya katika mpangilio wa meno yake.
Ama kwa hakika Joyce alikuwa wa pili kwa urembo, Isaya akakiri. Hapakuwa na utambulisho zaidi, Isaya ambaye alionekana dhahiri kuwa hana shida ndogondogo alikuwa kivutio mbele ya Betty. Ni aina hii ya wanaume alikuwa akihitaji. Aliwahitaji kwa ajili ya kuwachuna.
Wapambe nao walikuwa wamemjaza maneno Betty wakimsimulia juu ya bwana huyo kuwa ni mtoto wa waziri.
Betty akavutika, wapambe weakajua ameshoboka na bwana huyo. Lakini kichwani mwake hawakujua ana nini cha ziada.
Na laiti kama Isaya na kamati yake wangepewa walau ndoto ya kumjua vyema Betty, wasingethubutu hata kidogo kukaa naye na kujidanganya wamemteka.
Betty alikuwa mwanamke mwingine kabisa.
Betty alikuwa kazini!!!

*****

ZILIKUWA zimepita siku tatu bila Joyce kuonana na Isaya. Jambo hili lilimuumiza sana Joyce lakini alijipa imani nkuwa huenda ametingwa na mambo yake binafsi.
Ulikuwa usiku wa saa moja, simu ya Joyce ilivyopokea ujumbe.
Akaufungua na kufanya tabasamu hafifu, alikuwa ni Isaya.

“Mambo J.K, naomba unielewe kwa hili na ninajua utanielewa, sitaki mazoea yoyote yale ya karibu na wewe. Mpenzi wangu anahisi kuwa mimi na wewe ni wapenzi kumbe ni marafiki tu, hata mpenzi wako sidhani kama anaufurahia ukaribu huu kati yetu. Naomba tuwe tunakutana nna kuwasiliana kwa mambo ya msingi tu KAMA YATAKUWEPO. Tafadhali nisaidie kwa hili, na hizi meseji za hapa na pale tuachane nazo maana simu yangu mara kwa mara anakuwa nayo yeye. Maisha mema mdada.” 

Ujumbe ule ulimalizika huku Joyce akitetemeka. Macho yalikuwa yamemtoka mithili ya Panya aliyenasa mtegoni. Aliirudia mara mbilimbili na ujumbe ulimaanisha hapakuwa na utani hata kidogo.
Joyce alitaka kumpigia simu Isaya lakini akakumbuka kuwa aliwahi kumwambia ‘Hakuwahi kumpenda hata kidogo’ sasa watazungumza nini kigeni. 
Joyce akahaha, akatafuta wa kumshirikisha na hakupatikana kwa wakati huo. Hofu ikatanda, moyo ukaulaumu mdomo kwa kujificha kusema ukweli juu ya hisia alizokuwa nazo. 
Joyce akashuka pale kitandani na kuvaa viatu, akakimbia dukani na kujikuta akinunu vocha wakati simu yake ilikuwa na salio la kutosha. Akahaha huku na kule nab ado hali ikiwa ileile. 
Isaya amemtamkia rasmi kuwa yupo na mpenzi mpya.
Mshikemshike!!!

*** JOYCE Amemdengulia Isaya huku akijua kabisa kuwa anampenda…sasa anapokea ujumbe mkali unaompagawisha…..
***BETTY amekutana na Isayah, Isaya ana nia ya kumkomesha JOYCE je atafanikiwa? Kumbuka Betty ni muathirika.

ROHO MKONONI……..ITAENDELEA 

##COMMENT, SHARE, LIKE.....

Post a Comment

أحدث أقدم