SIMULIZI: USILIE NADIA
MTUNZI: George iron Mosenya
SIMU: 0655 727325
SEHEMU YA NANE
Nikaingia rasmi katika safari nyingine ya maisha ya kikimbizi, yaani ukimbizi katika nchi yangu huru kabisa!!!!
Lakini ningefanya nini iwapo nimelaaniwa!!!
Nina njaa naomba twende kula” alimaliza Nadia….akafuta machozi!!
Nilipata mshtuko kusikia kuwa kumbe Nadia aliwahi kupata kesi ya mauaji!! Laiti angekuwa amemuua Desmund wala nisingeshtuka, kumbe aliua katika jiji ambalo yupo kwa sasa. Mwanza!!! Lakini hakupanga kuua.
Halafu kumbe Jadida aliwahi kwenda Musoma…harakati zipi zilimpeleka dada huyo ambaye ni marehemu tayari.
******
Mlo unaoitwa ‘mlo kamili’ uliletwa katika meza yetu ambayo kwa maksudi kabisa tuliiacha izungukwe na viti viwili ili tuwe na uhuru wa kufanya mambo yetu. Hasahasa mazungumzo maana tulihitaji kuwa na faragha kwa kila kitu tulichokuwa tunafanya.
Nadia alipitia orodha ya chakula, safari hii tuliagiza chakula cha kufanana.
Sato na ugali wa dona!!
Hakika Nadia alikuwa na njaa!!
Mbaya zaidi hatukuwa tumepata kifungua kinywa asubuhi ya siku hiyo.
Kila mmoja akajikita katika sahani yake na kushambulia awezavyo, mara kwa mara nikimtupia jicho Nadia niweze kupata kitu cha kuandika hasahasa katika muonekano. Sikutaka kupitwa na tukio hata moja, hata jinsi anavyomeza chakula nilitaka kufahamu ili nikiandika kitu niwe nimeandika kitu chenye uhalisia na safari yangu hii iwaridhishe waliokuwa wanaifahamu na hata pesa zao waone zimeenda kiusahihi kabisa.
Nikiwa nimefikisha ugali wangu nusu ya safari huku samaki aina ya sato akiwa ameteketea upande mzima na macho ya samaki huyo yakiwa wazi yakinitazama. Niligutuka kuwa Nadia alikuwa amesita kula na alikuwa akiangaza macho huku na kule.
Nilimtazama kwa kwa sekunde kadhaa kisha akaonekana kupata kitu alichokuwa akikihitaji, akanyanyua mkono wake akapunga hewani.
“Nini tena Nadia…mbonaa….” Nilimuuliza huku nikiitazama sahani yake.
“Mwenzangu, nimeshiba kama nini?”
“Nadia umeshiba, yaani hivyo vitonge viwili tu Nadia hebu acha utani wewe.” Nilijaribu kubishana naye, wakati huo yule mtu wa kunawisha alikuwa amefika tayari akaanza kunawa mikono.
Nikakosa la kusema!!
“We acha huyo samaki hapo bwana!” nikamzuia yule muhudumu,tamaa zilikuwa zimeniingia tayari, na pia ubahili wa kumlipia samaki yule mkubwa kisha Nadia hata upande mmoja hakuwa amemaliza.
Muhudumu akanitazama kwa jicho la chuki lakini midomoni akatoa tabasamu lao la kawaida. Sikujali kuhusu hilo.
“Lakini Nadia..yaani samaki ndo umedonoa hivyo?” nilimuhoji, kisha nikaendelea,”Au waifungashe tukaisonsomole chumbani”
Nadia akalipuka kwa kicheko baada ya mimi kutumia neno lile maarufu sana kwa wasukuma jijini Mwanza na mkoani Shinyanga. Wakimaanisha ‘kula katika namna ya kufurahia’
“Ujue zamani nilikuwa nakula sana, huyo samaki huyo mbona hata robo tatu ningeweza kumfikisha mimi mwenyewe,unadhani mi huwa nina aibu katika kula, nakula sana tu lakini huwezi amini zamani niliambiwa kuwa mtu ukiwa umezoea kula chakula kidogo sana pasi na matakwa yako basi unajikuta bila kujua tumbo linajibana na kuwa dogo siku ukijaribu kula chakula kingi haiwezekani.
Sikuwahi kuamini, lakini maisha niliyoishi Musoma Vijijini huko yalinifanya niamini kuwa haya mambo yapo. Ile familia ya mzee Marwa ile, basi tu Mungu hakuwapa utajiri. Hakuwapa mali na dhiki zote akaziacha juu yao sijui kwaninihata. Ujue bila wao Nadia mimi ningekuwa nishakufa zamani sana, yaani zamani sana mwandishi. Sawa walikuwepo wanafamilia na mapungufu yao lakini hakika mzee Marwa ni mtu mwema sana japo najua ananichukia sana!!!
Dah! Safari ikiwa una nia mbaya nayo hakika unaweza kuwavurugia hata wengine ambao hawana nia mbaya, yaani jinsi nilivyokuwa nakereketwa hapa kooni, jinsi nilivyokuwa nina hasira nikiwa ndani ya basi. Yaani ilikuwa sawa kabisa mwandishi, yaani kila mtu nilikuwa na hasira naye ndani ya gari. Kila mwanaume nilimuona kama Desmund ama Ramso Rama, na kila mwanamke alifanana na mama yake Desmund huku wasichana wakimfanania yule wifi feki mwanaharamu kabisa. Aliyenigusa nilijikuta natoa tusi zito, kondakta akiwa wa kwanza kisha akafuata abiria ambaye alinigonga bahati mbaya, nikamtapikia matusi ilhali nikijishangaa japo sikuweza kujizuia.
Abiria niliyekaa naye siti moja pia aliipata moto moto ya matusi huku nikitishia kupigana. Watu wakadhani huenda nimechanganyikiwa. Wakaamua kunisusia!!
Safari za usiku sijui kama zina raha yake, lakini nililazimika kusafiri usiku,niliondoka Mwanza na gari ya mwisho kabisa kuelekea Musoma. Sikutaka hata mtu mmoja auone uso wangu. Hofu ilinitawala sana, hofu ya kukamatwa kwa kesi ya mauaji jijini Mwanza hivyo niliamua kusafiri usiku.
Baada ya basi zima kuwa limenichukia mimi naye niliendelea kuchukia zaidi.
Ni basi kuwa Mungu alituzibia namna ya mtu kuweza kuona mambo yaliyo katika moyo wa mwenzako. Lakini abiria wangeuona moyo wangu jinsi ulivyobeba uchungu mzito hakika wangelia na kusaga meno, wanaume wangejilaani huku wanawake wakiinama kwa aibu.
Lakini hawakujua haya yote, nilipoanza kulia ghafla ndani ya gari, wakatambua kuwa ukichaa unaanza kunipanda, nikiongea peke yangu jirani yangu anasogea pembeni kidogo ili nisimdhuru. Hali hii haikuwa njema hata kidogo!!
Hatimaye jirani alipopata upenyo wa kupita akatoweka asirejee tena, siti ya watu wawili nikabaki peke yangu.
Nililia sana, kila mmoja alinitafsiri alivyojua ye mwenyewe mi sikujali tena hayo.
Hatimaye ukafika ule muda wa kutengwa, muda ambao ulinikutanisha na familia nyingine kiajabu ajabu.
Familia ya mzee Marwa!!
Mwendo wa basi ulianza kupungua, kisha waliokuwa mbele wakaanza kutishia amani kwa , maneno yao.
“Tumetekwa…..tumetekwa jamani. Majambazi weeee!!” Alilalamika mwanaume mmoja.
“Mwanaume wewe acha hofu za kijinga jinga nani kasema tume…” kondakta alibwata lakini hakuimaliza kauli yake. Mara kweli tukawa tumetekwa.
Kwanza ikapigwa risasi, bila shaka hewani, lakini kwa wakati ule kila mmoja angeweza kuisikia ikiwa imelia katika sikio lake na labda kujihisi amekufa.
Hata mimi nilihisi nimekufa lakini nikajishangaa kuwa nipo hai katika kiti kilekile, cha ajabu sasa wale abiria waliokuwa wamenikimbia kwa kuhisi mimi nina wazimu, wengi walikuwa wamenikumbatia bila uoga. Wanadamu bwana, hapa huja ile kauli kuwa panapo matatizo wengi watakukimbilia wewe lakini uwapo na tatizo basi watakukimbia wao na usiwakamate katu!!
Mimi sikuwakimbia, na ningeweza vipi kuwakimbia iwapo walikuwa wameniegemea? Basi ukawa mshike mshike!!
Kwangu mimi kidogo ilikuwa salama, mara ghafla msukumo ukazidi kisha nikaanza kusikia milio ya ajabu ajabu akina mama wakilia na wanaume wakilalamika kwa maumivu. Jicho langu likafanikiwa kuona panga si panga jambia si jambia.
Kaka, usiombe kuona ninachokuhadithia mara likanyanyuliwa likashushwa, waaa!! Damu pwaa!! Mkono chini!! Abiria kanyofolewa mkono!!” Nadia akasita akanitazama machoni, bila shaka alitaka kutambua kama nimeguswa na kipengele kile, wacha wee alichokiona anajua yeye, maana mimi kama mimi japo sijioni nilijua kuwa nimekodoa macho sana. Inatisha msomaji!! Mkono kuondolewa!! Eti panga si panga jambia si jambia!! Nadia bwana!! Akaendelea!!
“Watu wakapiga mayowe mimi nikiwa hata uwezo kufungua mdomo sina, wakinamama wakazidi kunilalia, mara jicho langu likaiona panga si panga jambia si jambia likinyanyuliwa tena, mara likatua. Safari hii mlio uliotoka ni paa!! Mwanamama akapiga mayowe alikuwa amepigwa na ubapa wa maana!! Uzito ukaanza kupungua mimi nikiwa sijui nitafanya nini, kumbe ni mmoja baada ya mmoja anatolewa nje.
Nami nikafikiwa, kabla ya kuvutwa nikatoka mwenyewe, nikaenda nje upesi, maana wale waliojichelewesha walipigwa na ile panga si panga jambia si jambia. Niliposhuka ndani ya gari nikavutwa, kushoto. Ndani ya sekunde kadhaa nilikuwa uchi wa mnyama.
Nikasukumwa huku nikiona aibu huku aibu ikaniisha, kila abiria alikuwa uchi wa mnyama.
Kilikuwa kizaazaa. Wakati huo sasa wimbo wa mtaji wa masikini ule wa msanii gani sijui ulikuwa upo bado.
Wale majambazi au watekaji walikuwa wanao, wakawasha redio, Banza Stone…eheee!! Nimemkumbuka Banza anaimba kwenye redio sisi tunacheza uchi. Tena tulitakiwa kucheza kwa bidii huku kila mara mmoja wetu akiingia katikati kunengua mauno. Wakati tunaendelea kucheza ikafika zamu ya dereva kukata mauno, kama ingekuwa filamu hakika ningecheka maana dereva alikuwa kibonge na ana tumbo kubwa!!.
Dereva kibonge, akagoma. Mwandishi ujue alikuwa jirani yangu sana, nilimsihi, nilimsihi akubali yaishe, sijui kama alidhani bado nina wazimu wa kwenye gari lakini mimi nilikuwa nimeona kitu. Mwandishi niliona macho yanayofanana na ya marehemu Jaduda. Macho yasiyokuwa na utani na yanayomaanisha yanachosema. Yule jambazi hakuwa katika utani!!!
Kilikuwa kitendo cha sekunde kadhaa yule mwanaume jambazi ambaye alikuwa akionekana macho tu, aliruka na panga si panga, jambia sijambia.
Ohooo!! Damu ya mwanadamu ni ya moto sana aisee!!, damu ya dereva ikanirukia, alikuwa amechomwa bisu la tumboni.
Wacha watu waanze kupiga mayowe wakilia huku Banza Stone akizidi kuimba mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe…..nasi tukitakiwa kucheza. Huku mwenzetu mmoja akipigania uhai bila dalili yoyote ya kufanikiwa!!!
Ilitisha kutazama!!!
Baadaye tukaamriwa kulala chini kifudi fudi, sasa hakuna aliyebisha kila mtu alilala hivyo. Kimya kikatanda, redio ikiendelea kuimba kuwa mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe. Sisi tumelala kifudifudi. Uchi wa mnyama….tochi mbili zikitumulika. Tuakendelea kutambua kuwa wale majambazi wapo nasi!! Nusu saa ikakatika.
Mbwa waliokuja kutubwekea na kisha kumng’ata mmoja wetu akapiga mayowe ndio walitukurupua tena……
Kila mmoja akaanza kuhaha akitafuta namna ya kujistiri na hali ile.. Wengine walikuwa na watoto wao, wengine na wake zao, huenda na wengine na baba mkwe zao.
Kizaazaa!! Nani atajali katika hali hii???
Huyu avae ya huyu mara huyu avae ya huyu. Hapakuwa na umoja, huenda hicho kitu ndio kilisababisha hata tukashindwa kuelewana, mtu mmoja akavaa nguo yangu nilipomshika akanitukana akidai mimi ni kichaa.
Umoja ukajengeka, wakamuunga mkono kuwa mimi ni kichaa na sijui ninachokiongea, wengine wakaenda mbali zaidi na kusema kuwa ni mimi nimewazulia balaa lile la aina yake.
Mara nikatengwa maneno yakawa maneno!! Mara nisukumwe mara nitukanwe!! Hakuna aliyekuwa nani mwandishi!! Hakuna hata mmoja!!
Ile nguo aliyoing’ang’ania yule dada ndio nguo ambayo ilikuwa ndani yake nimeishonea ile pesa yangu niliyomuibia marehemu bosi wa Mwanza….na niliamini kuwa lazima itakuwemo, nilishona kwa ustadi mkubwa sana. Wale majambazi wasingeweza kuiona!!
Mwandishi Ni heri ningekaa kimya tu nisijibizane na umati ule …..ni heri ningekubaliana na usemi wa mwenye nguvu ndo mwenye haki.
Nilikosea sana kuthubutu kuongea….nilikosea sana kuidai haki yangu……” kilichotokea ……..
***NINI KILIMSIBU NADIA BAADA YA KUIDAI HAKI YAKE…..
#Usikose kipengele atakachoendelea kusimulia tena……ujue kwa mzee MARWA nini kilijiri na alifika vipi??
##TOA MAONI YAKO…..SHARE ZAIDI NA ZAIDI.
Itaendelea !!
إرسال تعليق