Slaa amuibukia Kinana

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeibua tuhuma nzito dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), `kumhujumu’  na kumvua ubunge Tundu Lissu (Singida Mashariki).

Njama hizo zinadaiwa na Chadema, kupangwa na CCM, ili zifanikiwe kupitia mahakama.

Tayari Chadema imetangaza kunasa mawasiliano kadhaa yanayolenga kutekeleza mkakati huo, ikiwa ni pamoja na kuitumia kampuni moja ya uwakili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa, alidai kuwa hatua hiyo imefikiwa na CCM kwa madai kuwa Lissu amekuwa ‘mwiba’ kwa serikali kila anapokuwa ndani na nje ya Bunge.

Alidai kuwa Chadema imekamata nyaraka mbalimbali zinazoonyesha kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, anatoa maelekezo kwa waliokuwa mawakili wa makada wa CCM waliofungulia kesi dhidi ya Lissu, wakipinga matokeo ya ubunge wake mwaka 2010.

Hata hivyo, shauri hilo liliamriwa na Mahakama Kuu kwa `kuyatupa’ maombi ya kutengua ubunge wa Lissu, Aprili 27, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, CCM kupitia kwa Katibu Mkuu wake, iliwataka mawakili hao kufungua rufaa katika Mahakama ya Rufaa, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, kanda ya Dodoma.
Bonyeza Read More Kuendelea



“Lengo la njama za Kinana na CCM ni kuhakikisha kwamba Lissu anafutiwa ubunge, ili asiweze kushiriki katika mchakato wa Katiba Mpya kama mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba litakalojadili na kupitisha rasimu ya Katiba Mpya baadaye mwaka huu,” alidai Dk. Slaa.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, katika kipindi kifupi cha Lissu kuwa bungeni, amekuwa mwiba kwa CCM na serikali yake, akiwawafumbua macho Watanzania kuhusu masuala aliyoyaita ‘makubwa ya kikatiba na kisheria’.

Dk. Slaa alisema baada ya Lissu kuwasilisha hotuba ya upinzani kuhusu bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria, Kinana aliwasiliana na mawakili na kutoa maelekezo hayo.
Akiwasilisha hotuba yake, Lissu ‘aliishambulia’ Tume ya Mabadiliko ya Katiba na CCM, kwa madai ya kuvuruga mchakato wa uundwaji wa mabaraza ya katiba ya wilaya, lengo likiwa ni kuhakikisha yanakuwa chini ya CCM.

Alidai kuwa mawakili wanaoshughulikia kesi hiyo ni kutoka kampuni ya mawakili ya Wasonga Associate Advocates ya mjini Dodoma.

Hata hivyo, NIPASHE Jumamosi ilipowasiliana na wakili Godfrey Wasonga, ambaye na namba zake za simu zipo kwenye waraka wa kampuni hiyo, alikanusha madai ya Dk. Slaa na kusema hazitambui nyaraka hizo.

Wasonga, alisema hana biashara yoyote na CCM na kwamba habari ya kupata maelekezo kutoka kwa Kinana au kukidai chama tawala fedha, alikuwa anazisikia kwa mara ya kwanza.


Wakili huyo alitaka kujua kama waraka huo umeandikwa neno ‘siri’, alipojibiwa sivyo, aling’aka kuutambua.

“Hiyo barua si unayo wewe? Mimi hapa sina, sasa nitazungumziaje barua ambayo unayo wewe. Sijui chochote kuhusu hiyo barua. Sijatuma barua yoyote na wala siidai fedha zozote CCM,” alisema.

Dk. Slaa alidai CCM imekuwa ikiwatumia wazee wanaowaita makada, Shaaban Itambu Selema na Paschal Marcel Hallu katika kufungua rufaa hiyo.

Watu hao ndio wanaotajwa katika shauri la awali lililofunguliwa dhidi ya Lissu na kutupwa na Mahakama Kuu kanda ya Dodoma.

“CCM na mawakili wanawatumia wanakijiji hao bila kuwapa taarifa au kuwashirikisha kwa namna nyingine yoyote,” alisema.

Aliongeza, “huyu Shaban Itambu Selema amekula kiapo mahakamani Dodoma kwamba yeye na mwenzake ambaye bado ni Katibu Kata wa CCM huko kwao, hawakuambiwa chochote juu ya kufunguliwa kwa rufaa hiyo.” 

Dk. Slaa alidai kuwa baada ya rufaa hiyo kufunguliwa, wakili Wasonga alimwandikia barua Kinana kumkumbushia malipo ya awali ya shauri hilo la rufaa.

Barua ya wakili huyo inayokwenda kwa Katibu Mkuu wa CCM na ambayo Dk. Slaa aliisambaza nakala yake, ilieleza;

“Naambatanisha invoice ya malipo ya awali ya Tshs. 2,000,000,  fedha za maandalizi ya awali ya sababu za rufaa pamoja na vitabu husika.”

Barua hiyo ya Mei 20, 2013 inayoonyesha kuandikwa na Godfrey S.J. Wasonga kwa niaba  ya Wasonga & Associates Advocates, ilieleza kuwa, “ikumbukwe ya kwamba katika shauri la mwanzo nilikuwa nalipwa na CCM Singida Mkoa na hawakumaliza malipo…”

“Pia shauri hili tutahitaji kuongezewa wakili mmoja kutoka Dar es Salaam na malipo ya usikilizwaji.”

Taarifa zinaeleza kuwa, pamoja na kufunguliwa kwa rufaa hiyo, lakini bado haijapatiwa namba ya usajili, licha ya kulipiwa ada ya kuifungulia na imeshapokewa na masijala ndogo ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Dodoma.

Dk. Slaa alidai kuwa gharama nyingi hasa za kesi za uchaguzi, zinaligharimu taifa na si CCM na endapo mchezo huo (CCM), kubambikiza kesi utaendelea, alimuomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati.

Jitihada za kumpata Kinana azungumzie madai hayo hazikufanikiwa kutokana na simu yake kutopatikana.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa CCM alisema Kinana aliyekuwa katika ziara ya kisiasa huko Ludewa, hayupo katika hali ya kuzungumzia mambo yanayokiathiri chama hicho.

“Katibu Mkuu anazunguka kukijenga chama, sidhani kama utampata kuzungumzia uvumi huo, hao watu tumeshawazoea,” alisema pasipo kutaka jina lake litajwe.

Post a Comment

أحدث أقدم