Taifa Stars yawatoa hofu Watanzania mechi dhidi ya Morocco


http://www.michezoafrika.com/NewsImages/Taifa-Stars-vs-Morocco.jpg
Thomas Ulimwengu akiwatoka wachezaji wa Morocco katika mechi ya awali iliyochezwa jijini Dar

BAADHI ya wachezaji wa timu ya soka ya taifa, TaifaStars wamewataka watanzania wasiwe na hofu yoyote dhidi ya pambano lao na wenyeji wao Morocco kwa kuahidi kuibuka na ushindi licha ya kucheza ugenini.
Stars inatarajiwa kuvaana na Morocco usiku wa Jumamosi nchini humo katika mechi ya mkondo wa pili kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazili.
Katika mechi ya kwanza ilioyochezwa Machi mwaka huu, Stars iliisambaratisha Morocco kwa mabao 3-1 na kuzidi kung'ang'ania nafasi ya pili katika kundi lao la C ikiwa na pointi 6, moja nyuma ya vinara, Ivory Coast ambayo itakuwa ugenini wikiendi hii kucheza na Gambia.
Licha ya kutambua ugumu wa mechi hiyo ya Jumamosi dhidi ya Morocco baadhi ya wacheza wa Stars wamewatoa hofu watanzania kwa kutamba kuwa ni lazima wawazime kwa mara nyingine Morocco japo wapo nyumbani kwao.
Mmoja wa wachezaji hao aliyezungumza na MICHARAZO kutoka Morocco ni Zahoro Pazi aliyerejeshwa katika kikosi hicho, alisema haoni sababu ya watanzania kuwa na mchecheto dhidi ya mechi hiyo kutokana na namna wachezaji wa Stars walivojiandaa.
Pazi alisema wachezaji wote wana ari na morali kubwa ya kuhakikisha wanaipa Stars ushindi mbele ya wenyeji wao kwa nia ya kujiweka nafasi nzuri kabla ya kuvaana na Ivory Coast katika mechi ijayo.
"Tunaendelea vyema na tunapenda kuwaambia watanzania nyumbani wasiwe na hofu, tutapigana kiume kuwapa raha na tunaamini Morocco watakaa Jumamosi hata kama watatucheza usiku," alisema.
Naye Himid Mao, alisema ushidni Jumamosi ni lazima kwa namna walivyofanya maandalizi na kujiamini kuwa wanaweza kurudia walichokifanya Tanzania kwa Morocco kwakuwalaza mabao 3-1.
Stars ambayo haijawahi kushiriki Fainali hizo za Kombe la Dunia, inahitaji ushindi ili kurejea nyumbani kuwasubiri Ivory Coast kabla ya kumalizia mechi za kundi lake Septemba mwaka huu dhidi ya Gambia ambao mpaka sasa wanaburuza mkia wakiwa na pointi moja tu.

Post a Comment

Previous Post Next Post