Watu 10, 799 wanaswa na dawa za kulevya Tanzania


Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe Mizengo Pinda

WATU 10,799 wamenaswa wakijihusisha na dawa za kulevya katika kipindi cha miaka mitano pekee na kuonyesha namna gani biashara ya dawa hizo lilivyo tatizo nchini.
Kwa mujibu wa hutuba ya Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Urasimu na Bunge) William Lukuvi katika Siku ya Kupiga vita Dawa za Kulevya Duniani ni kwamba biashara ya dawa za kulevya ni tatizo nchini.
Pinda alisema kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.
Aidha, amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara haramu ya dawa za kulevya nchini.
“Vile vile katika kipindi hicho jumla ya Watanzania 240 walikamatwa katika nchi mbalimbali, zikiwamo Brazil, Pakstani na Afrika Kusini,” alisema Pinda.
Alisema hali hiyo imekuwa ikiharibu taswira ya nchi na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu,  masharti magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
Pinda alisema hali hiyo inatokana na sifa mbaya inayojengeka kwa Watanzania wanaosafiri katika nchi hizo.
Alisema zipo dalili kwamba, endapo biashara hiyo itaachwa iendeleee, athari zaidi, zikiwamo kuingiliwa kwa misingi ya kiutawala na wafanyabiashara wa dawa kwa manufaa binafsi, kuongezeka kwa waathirika wa rushwa.
Aidha, alisema uwapo wa biashara hiyo huongeza mzunguko wa fedha haramu na kusababisha mfumko wa bei na hivyo kuongeza hali ya umaskini.
Pinda alisema kwa mujibu wa vyombo vya dola, takwimu zinaonyesha viwango vya Heroin na Cocaine zinazoendelea kukamatwa nchini, kuanzia mwaka 2000 ni vikubwa kuliko vile vilivyokamatwa miaka 10 iliyopita.
Alisema mwaka huu pekee kumekuwa na ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya katika eneo la kimataifa la Bahari ya Hindi karibu na nchini .
Kwa mujibu wa Pinda, jumla ya kilo 914 za Heroin zilikamatwa na kikosi kazi cha kuzuia uharamia cha Jeshi la Kimataifa.
Alisema askrimu, mikate na maandazi vilivyofanyiwa uchunguzi katika moja ya shule jijini Dar es Salaam vilibainika kuwa na kiasi kidogo cha dawa hizo za kulevya.
Aliwataka walimu na walezi kuwa makini na watu wanaouza vyakula katika maeneo karibu na shule ili kuepuka wauzaji hao kuwafundisha wanafunzi kutumia dawa za kulevya.

Post a Comment

أحدث أقدم