WAZIRI MKUU PINDA AZINDUA MRADI WA KUIMARISHA HALMASHAURI YA MIJI 18

Waziri mkuu Mizengo Pinda, akipokea mkataba wa mradi wa uhimarishaji wa Halmashauri za miji 18 uliozinduliwa leo, katika manispaa ya moshi, mkoani kilimanjaro, kuotka kwa mkurugenzi wa Benki ya Dunia, Philippe Donger, kulia ni waziri wa nchi Tamisemi, Hawa Ghasia.picha na Fadhili Athumani.
WAZIRI mkuu wa Jamhuri ya Tanzania, Mizengo Peter Pinda amezindua mradi wa kuimarisha halmashauri za miji 18 ya Dola milioni 225 inayofadhiliwa kwa fedha za mkopo kutoka benki ya dunia.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda (katikati), Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini, Philippe Donger kushoto) na waziri wa nchi Tamisemi, Hawa Ghasia(kulia) na baadhi ya washiriki katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa kuimarisha halmashauri za miji 18 uliofadhiliwa na benki ya dunia katika picha ya pamoja jana, manispaa ya moshi mkoani kilimanjaro.picha na Fadhili athumani.
 
katika hafla hiyo iliyofanyika leo, katika ukumbi wa Kuringe, Manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro, Waziri Pinda amezitaka Halmashauri zote kuhakikisha zinajenga tabia ya kutenga Bajeti kwa ajili ya kutunza miradi yote inayoanzishwa hapa nchini ikiwemo Barabara na mradi huo.

Waziri Mkuu Pinda ameyasema hayo katika Warsha ya uzinduzi wa mradi wa kuimarisha halmashauri zote za miji 18 Tanzania Bara iliyofanyika jana katika ukumbi wa Kuringe, manispaa ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro, mradi uliofadhiliwa kutokana na Fedha za mkopo wa Dola milioni 225 kutoka benki ya dunia.

Pinda amesema endapo mradi huo unaolenga kuimarisha Halmashauri ya miji 18 Tanzania bara ya Iringa, Moshi, Tabora, Lindi, Babati, Kibaha, Geita, Mpanda, Bariadi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Morogoro, Singida, Njombe, Musoma, Korogwe na Bukoba itasimamiwa vizuri na kutekelezwa kwa wakati itawezesha halmashauri kuibua vyanzo vingine vya mapato.

“Mheshimiwa Rais aliagiza na mimi narudia, Halmashauri zijenge tabia ya kutenga bajeti kwa ajili ya kutumnza miradi inayoanzishwa ikiwemo barabara na mradi huu tunaouzindua leo,” alisema Pinda.

Pinda amesema uzinduzi wa mradi huo ni thibitisho wa utayari wa Tanzania kutekeleza kazi kubwa na yenye kuleta matumaini ya maisha bora kwa wananchi wote na faraja kwa wageni watakaotembelea miji ya Tanzania siku zijazo.
Pinda ameishukuru Benki kuu ya dunia kwa kuiteua Tanzania kwa ajili ya mradi huo ambao utekelezaji barani aferika unaanzia nchini hapa kama mradi wa mfano huku akiwaagiza viongozi wote wa Halmashauri zote kumi na nane, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha mradi huo unafanikiwa .

“Wote tumesikia kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza katika Bara la Afrika kuteuliwa kufanya majaribio ya mfumo huu wa kupima matokeo ya mradi. Uteuzi huu umekuja wakati muafaka ambapo nchi yetu inaonesha imani kubwa ya jinsi serikali ilivyoamua kuwaletea maendeleo wananchi wake,” alisema

Waziri Pinda amesema kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, serikali haitafumbia macho uzembe au uharibifu wa fedha na vifaa utakaosababisha kazi hiyo kukwama na utekelezaji wa chini ya kiwango.

“Mafaniko ya mradi huu yataongeza imani kwa wananchi wetu, kuvutia wadau wengine kushirikiana na Halmashauri zetu kutekeleza miradi ya maendeleo, hatufumbia macho uzembe au uharibifu wa fedha au vifaa utakaosababisha uteklezaji wa mradi huu kukwama,” alisema Pinda.

Awali akisoma taarifa ya wizara, Kaimu Katibu mkuu, ofisi ya waziri mkuu (TAMISEMI), jumanne Sagini alisema Mradi huo uliofadhiliwa kwa kiasi kikubwa na Benki ya dunia, unalenga kuimarisha uwezo wa halmashauri za miji 18 katika utoaji huduma (Urban Local Government strengthening programme-ULGSP).

Amesema katika kutekeleza mradi huo, miji yote itakuwa imenufaika pakubwa na hivyo kubadilisha sura ya miji yetu na kuifanya ivutie uwekezaji, kuishi na kufanya kazi.
Kwa upande wake waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu (TAMISEMI), Hawa Ghasia, amesema mradi huo unalenga kuendelea kuziimarisha halmashauri za miji katika maeneo makuu matano ambayo ni Uboreshaji wa mfumo wa Mipangomiji, Ukusanyaji wa mapato ya ndani hususan mapato yatokanayo na kodi ya majengo.

Maeneo mengine yatakayolengwa na mradi huo ni uboreshaji wa mifumo ya udhibiti wa fedha, manunuzi ya mswala ya mazingira na kijamii, uboreshaji wa mifumo ya utekelezaji, uendeshaji na utunzaji wa miundombinu kwa ajili ya huduma za jamii na kuboresha uwajibikaji na uwazi.



Mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2013 hadi 2018 kwa mkataba kati ya Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania, uliosainiwa mwezi desemba mwaka 2012 ambapo jumla ya Dola za kimarekani milioni 225 zimetengwa huku dola milioni 201 zitapelekwa moja kwa moja kwenye halmashauri

Post a Comment

أحدث أقدم