DIWANI MMOJA WA CHADEMA AOMBA KURA KWA KUZINADI SERA ZA CCM

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbroad Slaa
DIWANI mmoja wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyekuwa anagombea umakamu mwenyekiti wa halmashauri ya Geita, aliomba kura kwa kunadi sera za Chama cha Mapinduzi (CCM), imefahamika. Diwani huyo, Dioniz Bugali wa Kata ya Kamhanga, vilevile alimteua Diwani wa CCM kuhesabu kura zake.
Bugali alifanya kituko hicho mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Geita kwenye mkutano wa nne wa baraza la madiwani kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Katika uchaguzi huo wa makamu mwenyekiti wa halmashauri, mgombea wa wa CCM alikuwa Masoud Kimondo ambaye ni diwani wa kata ya Kaseme na kwa Chadema alikuwa yeyé, Bugali.
“Nimesimama hapa kuomba kura…kabla ya kuomba kura naomba niseme neno…nafasi hii ya makamu mwenyekiti wa halmashauri sikuwa naitaka isipokuwa nimelazimishwa na chama changu(CHADEMA)kugombea.
“Nachotaka kusema hapa ni kwamba nikishindwa sitakata rufaa.
“Ninampongeza sana mgombea mwenzangu wa CCM,mimi hapa pamoja na kuwa ni diwani wa Chadema na ninagombea nafasi hii kupitia chadema,lakini bado ni katibu mwenezi wa CCM kwenye kata yangu ya Kamhanga…nipeni kura zenu,”alijinadi Dionizi baada ya kupewa nafasi kuomba kura.
Kauli hiyo ilisababisha madiwani wa CCM kulipuka kwakicheko wakidai Bugali ni mwenzao na wengine wakiitambia Chadema kwa kusema, “Haloohalooooooooooooooo … Chadema mmesikiaaaa…hiyo ndiyo CCM…Spidi 120…Chadema hamna chenu Kamhanga huyo ni mwenzetu.”
Pia baada ya kura kupigwa diwani huyo wa Chadema alimteua Diwani wa CCM Kata ya Nkome, Karema Chiratu kuwa wakala wake wa kuhesabu kura huku madiwani wenzake wanne wa Chadema wakibaki mdomo wazi.
Akisoma matokeo hayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Lupuga, alimtangaza Kimondo kuwa mshindi kwa kupata kura 29,dhidi ya Bugali aliyepata kura mbili.

Post a Comment

Previous Post Next Post