Mitambo ya wachina ikishindwa kuendelea na kazi kutokana na majengo kuachwa kwenye hifadhi ya barabara wanayoijenga.
Wakazi wa kata ya Itezi Jijini Mbeya wameilalamikia
Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa kitendo cha kufunga Barabara kuu itokayo Mwaji
kuelekea Stendi ya Tazara Uyole.
Barabara hiyo imefungwa kutokana na
Halmashauri hiyo kumwaga vifusi katikati ya barabara hiyo na kusababisha
usumbufu kwa wenye magari ambao kutokana na hali hiyo wamelazimika kuyaacha
magari yao na kutembea kwa miguu.
Kwa mujibu wa taarifa za wananchi wa kata
hiyo wamesema hali imedumu kwa zaidi ya Wiki mbili na kusababisha kukata
mawasiliano jambo ambalo ni hatari kama kutahitajika huduma ya dharula ya
kuhitaji gari kama zimamoto, Tanesco na Ambulance kwa wagonjwa.
Aidha wamehoji kuwa kuna ulazima gani wa
kumwaga vifusi kama hawako tayari kuanza kusambaza hali inayosababisha usumbufu
kwa wakazi wa maeneo hayo na bila kutoa njia mbadala ya kutumia kabla ya
kusawazisha.
Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na
mtandao huu umebaini kuwepo kwa mapungufu mengi katika kitengo cha Makandarasi
wanaohusika na barabara katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya baada ya kuwepo kwa
maeneo mengi ambayo vifusi huachwa zaidi ya mwezi mmoja.
Kuonekana kufeli kwa Kitengo hicho pia
kunadhihirishwa na ujenzi wa Barabara ndogo ya Lami inayopita pembezoni mwa
Uwanja wa Nane nane ambapo Mkandarasi ameanza vizuri kuichonga lakini baadaye
akalazimika kupunguza vipimo ili kuyakwepa baadhi ya majengo yanayodaiwa ya
Vigogo ndani ya Mkoa wa Mbeya.
Pia kinachoonekana ni kama mchezo wa
Panya wa “ nani amfunge paka kengere” kutokana na baadhi ya taasisi
zinazohusika kushindwa kutoa amri ya kuvunja majengo hayo licha ya kupita
kwenye hifadhi ya barabara pia yanatoa picha mbaya ya Uwanja wa Nane nane.
Baadhi ya watu waliohojiwa wamedai kuwa
labda Waziri Magufuli akiingilia kati ndipo majengo hayo yatakapobomolewa na
kudai kuwa huko ni kumsumbua Waziri kutokana na majengo hayo kuweza kudhibitiwa
na Halmashauri husika.
Picha na Mbeya yetu
|
Post a Comment