
Dar es Salaam. Rais
Jakaya Kikwete ametoa wito kwa waandishi wa habari kutoandika habari
zenye kuchochea vurugu kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kujikuta wakiwa
matatani.
Kikwete alisema hayo juzi wakati akifunga kongamano la kutafuta amani lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
“ Unaweza kuandika au kutangaza habari ya uchochezi leo, lakini vurugu
zikitokea hata kama ni baada ya miaka 20 utatafutwa na kushtakiwa kwa
habari hiyo,” alisema Kikwete.
Akitoa mfano, Kikwete alisema nchi za Rwanda na Kenya ni mifano hai kwa
kuwa kuna waandishi wa habari ambao walishtakiwa pamoja na wanasiasa kwa
uchochezi na kusababisha machafuko.
“Nawakumbusha waandishi kuweni makini kwa habari mnazoziandika na
kuzitangaza kwa kuwa mna uwezo wa kujenga na kubomoa,” alisema
Alisema vyombo vya habari,siasa na dini vikitumiwa vibaya ni rahisi kusababisha vurugu zenye kuhatarisha maisha ya wananchi.
Alitaka TCD kuandaa kongamano kama hilo kwa ajili ya waandishi wa habari wakiwa ni wadau katika kutafuta amani.
Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia akitoa maazimio ya kongamano hilo,
alisema viongozi waandamizi wa serikali wajizuie kutumia lugha za
vitisho.
Alisema pia kongamano hilo limeazimia kwamba kituo hicho kiwe karibu na
vyombo vya habari na kuwahimiza kuandika habari zenye uzalendo na
mshikamano wa kitaifa.
Mwananchi
Post a Comment