Kampuni ya kutengeneza transfoma ya Misri kuwekeza Zanzibar

Kampuni ya kutengeneza transfoma ya Misri kuwekeza Zanzibar

Na Othman Ame, OMPR

KAMPUNI ya Kimataifa inayojihusisha na masuala ya huduma za Umeme ya Misri ya Elesewedy Electric imeonesha nia ya kutaka kuwekeza kiwanda cha kutengeneza Transfoma pamoja na vifaa mbali mbali vya Umeme hapa Zanzibar.

Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki ya Kati na kati mwa Bara la Afrika wa Kampuni hiyo, Mohamed Sakr alieleza hayo alipokutana kwa mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake, Vuga mjini Zanzibar.

Mohamed Sakr alisema uongozi wa Kampuni hiyo umeridhika na mazingira ya Utulivu na ukarimu uliopo hapa Zanzibar na Kampuni yake kushawishika kutaka kuwekeza vitega uchumi vyake ili kutoa huduma za Nishati sambamba na kuzalisha soko la ajira kwa vijana wa Zanzibar.

Alisema Kampuni yao yenye ubora nambari moja Afrika na Mashariki na kati na nambari tano duniani, imekuwa ikitoa huduma za umeme na kufikia hatua za kuongeza Matawi yake katika mataifa mbali mbali ulimwenguni.

Mohamed aliyataja baadhi ya Mataifa ambayo Kampuni hiyo imeshawekeza miradi yake kuwa ni pamoja na Cameroun, Equatorial Guinea, Kenya na Ethiopia kwa Afrika na Colombia na Brazil katika Bara la Amerika ya Kusini na Russia iliyopo barani Ulaya.

“Mtazamo wetu ni kuwekeza mradi wa dola za Kimarekani milioni 300 nchini Kenya na dola za kimarekani milioni 600 nchini Ethiopia, wakati muelekeo wetu hivi sasa tumelenga kuwekeza hapa Zanzibar “, alisisitiza Mkurugenzi huyo wa Kanda ya Mashariki ya Kati na kati kati mwa Bara la Afrika wa Kampuni hiyo ya Elsewed.

Mohamed alimueleza Balozi Seif kwamba Kampuni hiyo imepanga kutumia mtaji wa zaidi ya dola za Kimarekani bilioni tatu (U$ 3,000,000,000) kwenye miradi yake katika kipindi kijacho.

Naye Balozi Seif Ali Iddi aliuhakikishia uongozi wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na masuala ya huduma za Umeme Nchini Misri kwamba Serikali itajitahidi kuona malengo ya Kampuni hiyo yanafanikiwa ipasavyo.

Balozi Seif alisema hatua hiyo itaongeza nguvu za uwekezaji zilizolengwa na Serikali hapa nchini hatua ambayo itasaidia kupanua wigo wa ajira ambao Serikali pekee hauwezi kuutekeleza.

Balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Kampni hiyo kuharakisha hatua za maombi ya mradi wao ili taasisi zinazosimamia Nishati, Uwekezaji na Viwanda ziupitie na kutoa mchango wao katika kufanikisha azma ya kuanzishwa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Nae Mwantanga Ame anaripoti kuwa, Balozi Seif ambae ni Mbunge wa Jimbo la Kitope amewakumbusha wazazi wa Kijiji cha Mgonjoni kiliomo ndani ya Jimbo hilo kuwapatia elimu watoto wao ili kuwajengea mazingira bora ya maisha yao hapo baadaye.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akisalimiana na Wananchi hao pamoja na kuwapatia futari na nguo wananchi hao wa Mgonjoni kwa ajili kumudu kuendelea vyema na ibada yao ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani unaoendelea.

Alisema hakuna kitu bora na sahihi cha wazazi hao wanarithisha watoto wao isipokuwa elimu ambayo ndiyo itakayowabadilisha Kiuchumi na kimaendeleo katika Kijiji chao.

“ Kinamama muelewe kwamba mtakuwa na kazi ya ziada katika kuwahimiza watoto wenu kwenda kujipatia elimu “. Alisisitiza Balozi Seif.

Katika kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kijiji cha Monjoni Balozi Seif amechangia Shilingi 1,000,000/- kwa ajili ya ununuzi wa matofali, saruji na fedha za fundi kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti wao.

Aliwahakikishia wananchi hao kwamba Uongozi wa Jimbo hilo utaendelea kutafuta mbinu mbali mbali za kutatua matatizo yanayowakabili likiwemo suala la Madrasa na Skuli.

Naye Mke wa Mbunge huyo Mama Asha Suleiman Iddi amewaomba akinamama wa Kijiji hicho kujikusanya pamoja na kuunda kikundi cha ushirika na yeye atakuwa tayari kuwapatia mtaji wa kuendesha shughuli zao za uzalishaji.

Mapema asubuhi Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi alikabidhi vifaa mbali mbali kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa Madrasat Mujitahidina iliyopo katika Kijiji cha Kitope Tobora.

Vifaa hivyo ni pamoja na Matofali, Nondo, Mchanga fedha za fundi pamoja na kukipatia chuo hicho Misahafu na Juzuu kwa ajili ya wanafunzi wa Madrasa hiyo.

Akizungumza na Walimu, Wanafunzi na Wazazi wa Kijiji hicho Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha amewasihi Washirika na wahisani wa ujenzi wa Misikiti Nchini hivi sasa kuelekeza nguvu zao katika ujenzi wa Madrasa za Quran.

Mama Asha alisema Visiwa vya Zanzibar hivi sasa vimepunguza kiu ya Misikiti ambayo baadhi yake imejengwa ikiwa na upungufu wa waumini jambo ambalo kama nguvu hizo zimetumiwa katika ujenzi wa madrasa ili kupunguza kero kubwa linaloikabili Jamii la uhaba wa maeneo ya kusomea Quran.

Aliwakumbusha waumini kurejea katika maadili ya zamani ya upendo miongoni mwao ili ile sumu ya chuki, uhasama na matendo mengine maovu wanayofanyiana waumini hao yapungue au kuondoka kabisa.

Alifahamisha kwamba mioyo lazima ibadilike katika njia ya Mwenyezi Muungu ili jamii ipate kufanikiwa katika mambo yao ya kila siku badala ya kuwatumia Walimu na wafanuzi wa madrasa katika matendo maovu ya mifarakano isiyo na hatma njema.

Post a Comment

أحدث أقدم