Jaji Damian Lubuva. |
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imefanya mabadiliko kwenye karatasi za kupigia kura na fomu za matokeo
ya uchaguzi ambazo zilitolewa awali kabla ya kuahirishwa kwa uchaguzi
mdogo wa madiwani unaotarajiwa kurudiwa leo katika kata nne za hapa.
Aidha, karatasi za kura za awali, zilikuwa na rangi ya kijani iliyopauka na sasa imebadilika na kuwa pinki.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva alipozungumza na waandishi wa habari juu ya uchaguzi huo utakaohusisha kata za Themi, Kimandolu, Elerai na Kaloleni.
Alisema fomu za matokeo ya uchaguzi zimebadilishwa ambapo namba zilizotumiwa awali hazitatumika, bali sasa zimetolewa namba mpya (ingawa hakuzitaja lakini zitakuwepo kwenye fomu hizo) na kusisitiza kuwa lengo la kubadilisha fomu hizo ni kuondoa uwezekano wa kutumika fomu za awali.
Jaji Lubuva pia aliasa vyama vya siasa kwenye kata hizo kuhakikisha vinaweka mawakala kwenye vituo vya kupigia na kujumlishia kura na kuongeza kuwa mawakala hawaruhusiwi kuandika majina ya wapiga kura na namba za kadi zao.
Alisema baada ya kupiga kura wapigakura wanatakiwa kuondoka vituoni na kurejea majumbani, kwa kuwa vyama vya siasa vitakuwa na mawakala wao ambao watalinda maslahi ya vyama husika na wagombea wao.
“Tume inasisitiza kuwa kwa mazingira na hali halisi ya Arusha, wapiga kura na wananchi kwa ujumla wasibaki kwenye vituo baada ya kupiga kura na hata kama sheria inaruhusu umbali wa meta 200, pia viongozi wa Nec tumekuja hapa kuangalia uchaguzi huu na kila kitu kimeshawasili, hivyo wananchi wasiwe na hofu,‘’ alisema.
Aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili wapate wawakilishi wao kwenye halmashauri. Kuhusu wapigakura ambao namba zao zitatofautiana na za kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura hawataruhusiwa kupiga na pia watu wasivae sare za vyama.
Kwa mpigakura mwenye ulemavu wa kutoona ataruhusiwa kuja kituoni na mtu atakayemchagua ili ampigie kura.
Msimamizi wa uchaguzi wa kata ndiye atakuwa na mamlaka ya kutangaza matokeo ya awali na kuwasihi wana Arusha kudumisha hali ya amani na utulivu.
Awali Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Sipora Liana alisema uchaguzi huo, uliahirishwa Juni 15 kutokana na mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa Chadema, hadi Juni 30 lakini uliahirishwa tena.
Wagombea udiwani katika kata ya Themi ni Victor Mkolwe (CCM), Lobora Ndarpoi (CUF) na Kinabo Edmund (Chadema); wa Elerai ni Boisafi Shirima (TLP), Emmanuel Laizer (CCM), Jeremiah Mpinga (Chadema) na John Bayo (CUF).
Wagombea katika kata ya Kimandolu ni Edna Saul (CCM) na Rayson Ngowi (Chadema), huku Emmanuel Mliari (CCM), Abbas Mkindi (CUF), Kessi Lewi (Chadema) na Ngilishi Pauli (Demokrasia Makini) wakigombea katika kata ya Kaloleni.
Kati ya vituo 136 Kaloleni ina 27, Elerai 55, Kimandolu 39 na Themi 15, huku idadi ya wapigakura ikiwa ni 60,123 na kutoa mchanganuo kuwa Kaloleni ina 12,636, Elerai 23, 797, Kimandolu 17,294 na Themi 6,396.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Sabas alipoulizwa juu ya ulinzi siku hiyo ya uchaguzi alisema umeimarishwa na aliwaondoa wananchi hofu na kuwataka wajitokeze bila wasiwasi.
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel Natse ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, aliwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kupata wawakilishi wao.
Hata hivyo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alidai kuona baadhi ya magari yamebadilishwa namba za usajili na kuwekwa vioo vya giza na kudai kuwa haijulikani magari hayo yatatumika kwa lengo gani leo.
Alidai Chadema ilifuatilia magari hayo hadi Makao Makuu ya Polisi jijini hapa na kuripoti, lakini ikajibiwa vibaya na polisi huku akisisitiza kuwa na picha za magari hayo.
Alidai pia kuwa baadhi ya wananchi wa Elerai ambao ni wafuasi wa Chadema, juzi usiku walipigwa mawe majumbani mwao huku wengine wakitukanwa na kusisitiza kuwa chama hicho kitalinda kura ili kudhibiti wizi.
Post a Comment