Kiganja cha binadamu. (Picha ya Maktaba). |
Mwanaume mmoja amelazwa katika
Hospitali Teule ya DDH-Bunda, baada ya kukatwa kwa panga kiganja chake
cha mkono wa kushoto na mkewe kwa kile kilichodaiwa alinyimwa fedha ya
matumizi.
Baada ya tukio hilo, kiganja hicho kilianguka chini na kumwacha mwanamume huyo akiugulia maumivu makali.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoani Mara, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Ferdinand Mtui, tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji cha Kitaramanka wilayani Bunda.
Mganga wa zamu hospitalini hapo, Dk Alphonce Kwesi, alisema kuwa majeruhi amelazwa hospitalini hapo na amekatwa kiganja cha mkono wa kushoto, ambacho kimetenganishwa kabisa na mkono na kwamba hali ya majeruhi inaendelea vizuri.
Aidha, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Masoud Mohammed amesema mtuhumiwa huyo Kerina Nyamkangati, tayari amefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Bunda na kusomewa mashitaka mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Said Hamad Kasonso.
Mohammed alisema mshitakiwa huyo anatuhumiwa kumkata kwa panga mume wake kwenye kiganja cha mkono wa kushoto na kukiondoa baada ya kunyimwa pesa za matumizi.
Alisema kuwa mshitakiwa huyo alikana mashitaka na kupelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na kesi yake itatajwa tena mahakamani hapo Julai 23 mwaka huu.
Post a Comment