Na Hassan Hamad OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema
matarajio ya wananchi kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba ni kuona
unaondoa vikwazo vya utafutaji na matumizi ya rasilimali asili zikiwemo
mafuta na gesi.
Maalim Seif ameeleza hayo nyumbani kwake mbweni alipokuwa na mazungumzo
na ujumbe wa Uingereza ulioongozwa na Naibu Waziri anayehusika na Mambo
ya Nje na Jumuiya ya Madola, Mark Simmonds ambapo pamoja na mambo
mengine walizungumzi juu mchakato wa katiba na maendeleo ya utafutaji
na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar.
Amesema wakati Zanzibar imeshaamua kuliondoa suala hilo katika orodha ya
mambo ya Muungano, bado inasubiri taratibu za kisheria ambazo zinaweza
kupatikana baada ya kukamilika kwa mchakato wa katiba.
Amesema mara baada ya kukamilika kwa mchakato huo na suala la mafuta na
gesi asilia kuondolewa katika mambo ya Muungano, Zanzibar itatangaza
zabuni za uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ambapo makampuni mbali
mbali yataruhusiwa kuomba zabuni hizo, na hatimaye kuanza rasmi kwa kazi
ya uchimbaji.
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim
Seif Sharif Hamad akizungumza na Naibu Waziri wa Uingereza anayehusika
na Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola, Mark Simmonds, nyumbani kwake
Mbweni.
Amefahamisha kuwa mchakato wa katiba umefikia hatua nzuri baada ya
kuanza kwa mabaraza ya katiba tarehe 12/07/2013, ambayo itafuatiwa na
bunge la katiba na baadaye wananchi wataamua katiba hiyo kupitia kura ya
maoni.
Kuhusu nishati ya umeme ambapo Uingereza ni mshirika wa karibu wa
nishati hiyo nchini, Maalim Seif amesema Zanzibar imo katika mchakato wa
kutafuta nishati mbadala itokanayo na jua pamoja na upepo, ambapo
tayari imeonesha mwelekeo mzuri.
Amesema nishati hiyo itakapopatikana itaondosha usumbufu unaojitokeza
mara kwa mara na kupunguza utegemezi wa upatikanaji wa umeme kutoka
Tanzania Bara, sambamba na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Aidha Maalim Seif ameelezea mazingira ya uwekezaji Zanzibar, na kuuomba
ujumbe huo kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza hasa katika sekta za
utalii na uvuvi wa bahari kuu.
Amesema Zanzibar ambayo kwa sasa imetoa kipaumbelele katika sekta ya
utalii, inakaribisha wawekezaji katika ujenzi wa hoteli za nyota tano
katika visiwa vya Unguja na Pemba.
Ameongeza kuwa Zanzibar pia ina mpango wa kujenga bandari ya kibiashara
katika eneo la mpigaduni, pamoja kuvifanyia matengenezo makubwa viwanja
vya ndege, ili kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji.
Nae bw. Simmonds amesema Uingereza itaendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta mbali mbali ikiwemo nishati.
Ameahidi kuwasiliana na makampuni ya utalii, uvuvi na ujenzi ili
kuangalia uwezekeno wa kuja kuwekeza Zanzibar katika maeneo mbali mbali
nchini.
Chanzo - ZanziNews
Post a Comment