
MWENYEKITI
wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe,
anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi
dhidi ya jeshi hilo, vyombo vya dola na serikali kwa ujumla.
Taarifa ya
jeshi hilo iliyotolewa na Msemaji wake, Mrakibu Mwandamizi, Advera
Senso, imesema kuwa Mbowe amekuwa akitoa kauli ambazo zimekuwa na mlengo
wa uchochezi na kuijengea jamii taswira hasi juu ya vyombo vya ulinzi
na usalama na kuwafanya wananchi kuwa na hofu.
Mbowe
akiandamana na mawakili, Nyaronyo Kicheere na Peter Kibatara,
alijisalimisha mwenyewe makao makuu ya polisi majira ya saa 8:30 mchana,
mara tu baada ya kuwasili jijini kutoka safarini.
Hatua hiyo
imetokana na kitendo cha polisi juzi usiku wa manane kuvamia nyumbani
kwake jijini Dar es Salaam na walipomkosa waliacha namba ya simu ya Mkuu
wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ili ajulishwe kwamba
anahitajika.
Aidha, jana
askari wengine kutoka Polisi na wengine wanaoaminika kuwa ni wa Idara ya
Usalama wa Taifa walikwenda katika hoteli moja mjini Moshi walikoamini
kwamba kiongozi huyo amejificha kwa nia ya kumkamata lakini
hawakuambulia kitu.
Hata hivyo,
wakati Mbowe akishikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma hizo, wenzao wa Mkoa
wa Dar es Salaam wamedai polisi hawawezi kusumbuka kumkamata kiongozi
huyo kwa mambo ya kisiasa.
Naibu
Kamishina wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ally Mlege,
aliwaambia jana jijini Dar es Salaam waandishi wa habari kuwa polisi
hawawezi kujiingiza katika malumbano ya kisiasa baina ya vyama hivyo
viwili.
“Hatuna
kauli yoyote kuhusu mivutano ya kuanzisha na kuendesha vikosi vya ulinzi
na usalama inayoendelea ya kisiasa kati ya CCM na CHADEMA, jamani hayo
ni mambo ya kisiasa,” alijibu Mlege.
Mbowe
amehojiwa kutokana na uamuzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA kutaka kuanzisha
kikosi cha vijana cha ulinzi cha Red Brigade na kauli ya kulituhumu
jeshi hilo kumjua aliyehusika na bomu lililorushwa kwenye mkutano wa
CHADEMA jijini Arusha na kuua watu wanne.
Mwenyekiti
huyo pia anahojiwa kwa madai ya kulituhumu Jeshi la Polisi kuisaidia CCM
katika uchaguzi mdogo wa madiwani Arusha, pia madai ya kutoa kauli
kwamba kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukaa kimya kuhusiana na mauaji
hayo, kunaonesha dalili za serikali kujua nani alihusika na tukio hilo.
Tuhuma nyingine ni madai ya kuhamasisha chuki kati ya jeshi na wananchi, pia kuchochea wakazi wa Mtwara katika sakata la gesi.
Mbowe ambaye
alihojiwa takriban kwa saa tano, aliachiwa kwa dhamana na anatakiwa
kuripoti tena Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Julai 23, saa 8 mchana.
Kauli ya CHADEMA
Kufuatia
tukio hilo, CHADEMA wamesema kitendo cha kumkamata kiongozi huyo
kimedhihirisha wazi kuwa serikali ya CCM imeshindwa kuongoza nchi kwa
mujibu wa sheria.
Mkurugenzi
wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema hatua ya serikali
ya kuwafungulia wapinzani tuhuma za uchochezi kwa kusema ukweli haina
tofauti na vitendo vya serikali ya kikoloni iliyomkamata na kumfungulia
mashitaka Mwalimu Julius Nyerere tuhuma kama hizo.
“CHADEMA
kama ilivyokuwa TANU, tunashinda. Jeshi la Polisi ambalo askari na
maofisa wake ni watuhumiwa wa mauaji si tu ya bomu na risasi Arusha,
bali hata ya Mwangosi na mauaji mengine, isitumie madai ya uchochezi
kuidhibiti CHADEMA na viongozi wake.
“Polisi
kumhoji Mbowe siku chache baada ya kauli za Kikwete alizotoa kwenye
mkutano wa TCD ni dalili kwamba wamesukumwa na mamlaka za juu yao. Jeshi
la Polisi limshauri Kikwete kama anaona CHADEMA inasema uongo na
uchochezi, basi aunde tume ya majaji ili ukweli ujulikane,” alisema
Mnyika.
CHADEMA
imesema chama hicho kimekuwa kikisimamia ukweli kuhusu mauaji yenye
mwelekeo wa kisiasa tangu mwaka 2011, Arusha, 2012 Morogoro na Iringa na
2013 mkoani Arusha.
“Vyombo vya dola vikiwa ni sehemu ya watuhumiwa, ukweli huo unaitwa uchochezi na kutukamata badala ya watuhumiwa wa mauaji.
“Alichokisema
Mbowe ni maamuzi ya Kamati Kuu na kama wanaona ni uchochezi basi
wakamate wajumbe wote wa Kamati Kuu na wakishitaki chama,” alisema
Mnyika ambaye katika kumsindikiza Mbowe aliandamana na Benson Kigaira na
John Mrema.
Tendwa ashambuliwa
Katika hatua
nyingine, CHADEMA imemshambulia vikali Msajili wa Vyama vya Siasa, John
Tendwa, kwa kile walichokiita ‘undumila kuwili’ kutokana na suala zima
la ulinzi wa vyama.
Taarifa
iliyotolewa na John Mnyika alisema Tendwa katika Mkutano Mkuu wa chama
hicho Agosti 13, 2006, akiwa kama mgeni mashuhuri alibariki na
kukubaliana na mabadiliko ya katiba yaliyofanywa na chama hicho.
Alisema moja
ya mabadiliko yaliyofanywa na kuungwa mkono kwa pongezi na Tendwa ni
uamuzi wa chama kuwa na chombo cha kulinda viongozi na mali za chama
kitakachoitwa Brigedi Nyekundu.
“Tendwa
katika hotuba yake alipongeza mabadiliko hayo ya katiba na ikasajiliwa
katika ofisi yake mwaka 2006, baada ya kukubali kwamba imekidhi mahitaji
yote muhimu.
“Leo
anapogeuka na kuwaacha polisi kuadhibu viongozi wetu kwa kile
alichokiunga mkono wakati ule ni jambo la kusikitisha sana na lenye
lengo la kufuata mkumbo wa kauli ya Kikwete na polisi badala ya
kuzingatia katiba na sheria za nchi.
Mnyika alisema badala ya Tendwa kuitishia CHADEMA ambayo haijavunja sheria, ingekuwa bora akakifuta Chama Cha Mapinduzi.
“Hiki
kimevunja sheria katika chaguzi ndogo za Kiteto, 2007, Tarime 2008,
Busanda na Biharamulo 2009, Uchaguzi Mkuu 2010, Igunga 2011, Arumeru
2012 na za marudio kwenye kata 21, mwaka 2013 kote nchini.
“Kwa muda
mrefu tumekuwa tukieleza kuhusu makambi ya Green Guard yanayofanya
mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya kufanya mashambulizi na matukio kwa
Wanachadema na wanahabari.
“Mathalani
mbali ya kushambuliwa CHADEMA, Green Guard ya CCM imewahi kuwashambulia
waandishi wa habari, Frederick Katulanda wa Mwananchi mwaka 2010 katika
kampeni za Uchaguzi Mkuu, Musa Mkama wa Dira ya Mtanzania huko Igunga
katika uchaguzi mdogo 2011, Munir Zacharia wa Channel Ten huko Zanzibar
katika uchaguzi mdogo wa Bububu na ushahidi wa hayo upo,” ilimaliza
taarifa hiyo
Post a Comment