
Mwenyekiti, Aden Rage
Wekundu
wa Msimbazi Simba “Taifa kubwa” wanatarajia kufanya mkutano mkuu wa
wanachama Agosti 20 mwaka huu jijini Dar es salaam ili kujadili mambo
mbalimbali yahusuyo maendeleo ya klabu hiyo.
Mwenyekiti
wa klabu ya Simba ambaye ni mbunge wa Tabora mjini, Alhaji Ismail Aden
Rage amesema kwa kawaida mkutano huo ulitakiwa kufanyika Agosti 5 kwani
mwaka jana ulifanyika tarehe hiyo, lakini wamelazimika kusogeza mpaka
tarehe tajwa ili kuepukana na mwezi mtukufu wa Ramadhan.
“Tumeamua
kusogeza mbele mkutano mkuu wa wanachama wa klabu ya Simba, lengo letu
ni kuepukana na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, lakini pia kufika
muda huo uongozi utakuwa umekamilisha baadhi ya mambo”. Alisema Rage.
Rage alisema katika mkutano wa mwaka huu kutakuwa na ajenda mbalimbali ambazo zitajadiliwa na wanachama halali wa klabu hiyo.
Mwenyekiti
huyo alisema ajenda ya kwanza itakuwa ni kujadili taarifa ya ukaguzi wa
fedha za klabu, na baada ya kujadiliwa kwa ajenda hiyo, watajadili ya
pili ambayo ni mipango endelevu ya klabu hiyo.
Rage
aliendelea kueleza kuwa ajenda ya tatu ni Taarifa ya klabu itakayosomwa
na katibu mkuu Evodius Mtawala, baada ya hapo wanachama watachangia,
huku hotuba ya mwenyekiti ikifuatia na hatimaye kufungwa kwa mkutano
huo.
“Cha
msingi ni kuwa wanachama watakaohusika katika mkutano huo ni wale hai
tu waliolipa ada ya uanachama kupitia benki. Kama mtu anafikiri ni utani
basi ajitokeze siku hiyo wakati si mwanachama hai”. Alisema Rage.
Rage
aliwataka wanachama wa Simba kujiandaa na mkutano huo ambao utakuwa
chachu ya mafanikio ya klabu yao ikiwemo kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka
Tanzania bara msimu ujao.
“Sisi
Simba tumejipanga sana, tunataka kuiboresha timu yetu katika Nyanja
zote, Agosti 20 wanachama wote wanatakiwa kufika katika mkutano ili
kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ya kuijenga timu yao kwa
kuchangia mawazo yao”. Alisema Rage.
Ili
kufanikisha mkutano huo, leo hii wadhamini wakuu wa klabu hiyo, Kampuni
ya bia ya TBL kupitia kinywaji chake cha bia ya Kilimanjaro,
wamekabidhi shilingi milioni 20 kwa uongozi wa Simba ikiwa ni sehemu ya
udhamini wao.
Akiongea
wakati wa makabidhiano hayo, meneja wa TBL, George Kavishe alisema wao
wanajipanga kuendeleza klabu ya Simba chini ya mwavuli wa udhamini wao,
hivyo wanawatakia mkutano mwema wekundu hao wa Msimbazi Simba wenye
makazi yao mitaa ya Msimbazi Kariakoo jijini Dar es salaam
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam

إرسال تعليق