![]() |
| Mheshimiwa Edward Lowassa Photo swahili TV |
Na Swahili TV
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Edward Lowassa, amemsifia
Rais Jakaya Kikwete kuwa ameweza kuifanya Tanzania kupata heshima
katika ulingo wa kimataifa, aliyasema hayo wakati akihojiwa na Swahili
TV jijini Washington DC.
Alisema kitendo cha Rais wa Marekani Bwana Barack Obama kuja nchini na
viongozi mbalimbali wa mataifa makubwa kumeonyesha Rais Kikwete
anakubalika.
“Ni hivi karibuni tu Rais Xi Jinping wa China, Rais Obama na Rais
mstaafu wa Marekani George W. Bush walikuwa nchini Tanzania, hii
inaonyesha kuwa Tanzania iko juu katika medani za kimataifa” alisema
Mheshimiwa Lowassa.
Mheshimiwa Lowassa ambaye yuko nchini Marekani kwa ziara ya kikazi,
aliongeza kwa kusema, Rais Kikwete anastahili pongezi sana kwa hilo
kwani sio rahisi kwa viongozi wa mataifa makubwa kutembelea nchi zingine
labda kama mko juu sana katika medani za kimataifa.
Pia alisema Rais Kikwete amekuwa akihusishwa na utatuzi au ushauri wa
kutatua matatizo mbalimbali ya nchi zingine na pia ameanza kuishirikisha
Tanzania katika usimamizi wa amani katika nchi mbalimbali.
Tanzania iliweka historia hivi karibuni kwa maraisi wawili wa Marekani
kukutana katika nchi moja kwa wakati mmoja, Rais Barack Obama na
George W.Bush walikutana jijini Dar es Salaam mwezi huu.

إرسال تعليق