RIWAYA: ROHO MKONONI 16


RIWAYA: ROHO MKONONI


MTUNZI: George Iron Mosenya

CALL: 0655 727325

SEHEMU YA KUMI NA SITA

Furaha ikizidi sana hupunguza uwezo wa kufikiri!! Uchungu ukizidi vilevile huleta tatizo hilo hilo.
Joyce akalala na Fonga hadi asubuhi.
Alipotoka pale ndani alikuwa na milioni tatu kibindoni huku nyuma akimwacha Fonga akijiuliza ile ladha ya penzi alilolingoja kwa muda mrefu hatimaye ameipata.
Watu wawili walikuwa wanaota kwa pamoja lakini ndoto mbili tofauti.
Joyce akiota kumuokoa Joy kwa sababu pesa aliyoipata akiongezea na ile ya kwenye akaunti ya Betty basi jumla inafika milioni sita!!
Fonga akaota ndoto ndogo tu lakini nzito, akaamua kuweka tena kichwani suala la kuoa. Kumuoa Kidoti.
Baada ya muda mrefu wa kuachana na mapenzi baada ya tukio la mwenye pesa mmoja kumnyang’anya mpenzi wake aliyempenda hadharani kisha kumweka rumande kwa kesi asiyoijua, kesi iliyomfanya atumikie kifungo cha miezi tisa jela. 
Kitendo ambacho kilimfadhaisha Fonga na kukoma kabisa kujihusisha na mapenzi, sasa alikuwa amefika tena kwa Joyce Kidoti. Na kisha akatangaza ndoa katika nafsi yake.
Hakika ilikuwa ndoto ndogo, lakini nzito sana!! Ilikuwa nzito kwa sababu hakujua kama kuna mambo mengine mazito yalikuwa yakiendelea nyuma ya pazia!!

*****

SAA nne asubuhi Kidoti allikuwa amejitawala katika chumba chake, hakutaka kukumbuka sana juu ya Fonga na nini kilichotokea, alichofikiri kwa wakati huo ni pesa aliyopata na katika namna ya kumwokoa Betty bila kutumia kivuli cha Isaya.
Joy alijipa moyo kuwa penzi alilompa Fonga ilikuwa njia tu ya ukombozi na hapakuwa na jingine la ziada pale.
Joy hakutulia sana chumbani kwake, akaitwaa kadi ya benki ya Betty, akajisogeza katika mashine ya kutoa pesa.
Akatoa shilingi laki tano. Kiwango cha mwisho kabisa kutoa pesa katika mashine kwa kipindi hicho.
Akatoa katika akaunti yake pia shilingi elfu hamsini!!
Akarejea nyumbani, alipotulia akapiga simu katika ile namba iliyokuwa imemuonya kuwa apige simu akiwa ana pesa, vinginevyo asifanye thubutu yoyote ya kuwasiliana naye.
Sasa Joy alikuwa na pesa kadhaa, akamtwangia simu bwana mwenye sauti nzito!!
Simu ikaita kidogo kisha ikapokelewa.
“Samahani kaka nimepata nusu hadi sasa lakini baada….” Kabla hajamaliza akaingiliwa kati na sauti ile.
“Nitafute ukiwa na pesa kamili. Nakupa siku mbili tofauti na hapo sitakuwa na haja na pesa yako. Nakukumbusha. Ole wako uwashirikishe polisi!!” Kisha simu ikakatwa.
Ama kwa hakika mtekaji huyo hakuwa na utani hata kidogo. Alinuia kabisa kufanya kitu kibaya kwa Betty.
Joyce akabaki kuitazama tu simu yake akidhani itasema naye lolote!!
Haikufanya jitihada zozote za kumfurahisha…..
Taratibu akalegea bila kujizuia, kisha akaanza kutokwa na kilio cha chini chini kama mtoto mdogo anayelia huku akiwa amezibwa mdomo wake!!
Hakufanya jitihada zozote za kuyafuta machozi yake!!
Hakika alikuwa matatani!!
Ule mzigo wa urafiki wa dhati ulikuwa unaanza kumuelemea haswa.
Alipokumbuka kuwa anakaribia siku nne bila kuhudhuria vipindi darasani, akataharuki, akampigia simu kiongozi wa darasa kuulizia lolote lile linaloendelea.
Akaambiwa kuwa asubuhi ya siku inayofuata kutakuwa na mtihani. Akatajiwa somo, akapagawa!!
Lilikuwa somo gumu sana na muhimu katika kozi yake.
Joyce akajikunyata baada ya kukata simu, akaanza kulia kama mtoto, akakumbuka kumlilia na mama yake aliyekufa miaka kadhaa nyuma.
Alisikitisha kumtazama!!!!
****

Mzee, Akunaay Zingo na mwanaye kipenzi, Isaya walikuwa katika mshangao mkubwa. Mshangao wa kujiuliza ni akina nani wale ambao walidiriki kumnyakua Betty kutoka mikononi mwa mwanaye na kisha kukaa kimya hadi dakika hiyo.
Mzee Akunaay alikuwa ametoa maelezo polisi juu ya namba iliyowahi kumpigia simu na kumtahadharisha juu ya mpango kabambe wa kutekwa kwa wapenzi wawili, Isaya na Betty ambao walikuwa wametoka kuvikana pete za kujitambulisha kama wapenzi.
Tatizo namba ile ilikuwa haipatikani tena!!
Ikawa haina maana tena.
Isaya alikuwa amepagawa zaidi kwa hilo tatizo. Cheo cha baba yake hakikusaidia lolote kuhusu upatikanaji wa Betty ambaye ni mchumba wake, na alitarajia kumuoa kabisa ili aweze kujiweka katika nafasi nzuri ya siasa za chuoni na pia kama shambulizi la uhakika kwa Joyce ambaye alimtosa na kuapa kuwa hampendi hata kidogo.
Sasa alikuwa katika fumbo na kujiuliza ni nani yuko nyuma ya mambo haya. Lakini jibu halikuwa jepesi. Jeshi la polisi nalo lilikuwa halijapata mstakabali wowote maana kila penye dalili ya kuleta mwanga wa mafanikio, kiza kisichotarajiwa kilitanda.
Huu ukawa mtihani mkubwa sana!!
Mtihani mgumu kabisa kuwahi kuwafika!!
Pesa na umaarufu zikakosa umaana.
Mzee Akunaay akaamua kuhoji juu ya mahusiano yao yalipoanzia na ni wapi walikutana.
“Unawafahamu wazee wake kwani?” Alimuuliza mwanaye huku akiwa amesimama akipiga hatua kwenda mbele na kurudi nyuma.
“Tulikuwa hatujaenda bado.” Alijibu huku akiwa ameinama Isaya.
“Kwa hiyo, hauwajui si nd’o hivyo!!” alikazia mzee Akunaay.
Isaya hakujibu kitu.
“Yaani Isaya mwanangu wewe na akili zako za kiutu uzima kweli unakwapua tu msichana barabarani haufuatilii hata wazazi wake, mji anaotoka, ghafla ghafla tu unamvika pete eti unataka kuoa. Hivi kilikusibu nini lakini mwanangu eeeh! Ulikuwaje Isaya ukafanya mambo ya kishenzi kama haya. Sasa sisi tutajuaje kama alikuwa ni mtu mbaya labda, sasa tazama amekuingiza katika matatizo tayari….mi si nilishasema watoto wa siku hizi mkishapata elimu kidogo mnajifanya kujua kila kitu. Mnajichagulia tu wqsichana wa kuoa, hakuna kuwasikiliza hata wazazi. Haya yapo wapi? Yapo wapi Isaya.” Alibwatuka mzee Akunaay huku akisahau kabisa kuwa ni yeye alikuwa akitamba katika kipaza sauti siku ya sherehe ya Isaya, kuwa mwanaye amechagua mke anayefaa sana.
Na kama haitoshi ni yeye aliyelipia chumba kwa ajili ya mapumziko yao baada ya kuvikana pete.
Sasa anamgeuka Isaya na kumwona kama mkurupukaji katika maamuzi. Maamuzi ya kujiingiza katika mahusiano na Betty.
Binti ambaye mzee Akunaay alilalamika kuwa hakuwa akijulikana ni wapi anapotoka na wapi anaishi.
Isaya alitaka kujibu tuhuma za mzee wake lakini akakumbuka kuwa yule alikuwa ni baba na alikuwa na haki ya kulalamika bila kukumbuka lolote lile.
Na mtoto kwa mzazi hakui!!
“Sasa nasema kama baba yako mzazi, kuanzia dakika hii sitaki ujihusishe na huyo binti. Apatikane ama asipatikane! Unanielewa Isaya, nasema hivi, apatikane ama asipatikane!! Sitaki kukusikia naye tena.” Alimaliza kwa amri, kisha akatoweka katika chumba ambacho alikuwa amechukua kwa hifadhi jijini Dar es salaam.
Isaya akachanganyikiwa!!
Lakini hakuwa na ujanja, mzee akapunguza makali katika kuwasisitiza askari juu ya umuhimu wa huyo mtu aliyepotea, na kufikia hapo Isaya bnaye akanywea! Akabaki kujipa imani kuwa ipo siku Betty atarejea.
Huo ukawa mwisho wa kumsaka kwa kuwatumia askari.
Akamfikiria mtu mwingine ama namna nyingine ya kumsaka Betty katika njia ambayo baba yake mzazi hataweza kuitambua.
Akaumiza sana kichwa na kupata jibu!!
Alipoachana na baba yake huku kila upande ukiwa umenuna. Isaya aliamua kupiga simu na kujaribu harakati nyingine.
Hii ilikuwa ni masaa machache kabla hajaenda polisi kuandika maelezo yake ya ziada. Akaamua kumaliza kwanza jambo hili kwa kadri akili ilivyomtuma.
Simu ikaanza kuita! Akatabasamu!!

******

FONGA alikuwa katika chumba chake akiona kama miujiza juu ya filamu nzima ilivyochezeka katika namna ya kustaajabisha, ni kweli hakuwa na pesa za kutosha. Na alifadhaika sana kumwomba Joyce shilingi elfu mbili wakati alikuwa katika matatizo.
Tatizo la kumwomba pesa halikumsumbua sana kichwa kwani hilo lilikuwa la kupita, akalipuuza.
Kisha akakumbuka kuwa lipo la kudumu ambalo ni mapenzi. Hili lilimuumiza kichwa kwa mwaka na miezi kadhaa. Aliisikia kabisa nafsi yake ikimsukuma kumtamkia Joy kuwa anampenda, lakini akajikosoa kwa kujiuliza, ‘nitamwonyesha vipi kuwa nampenda bila kuwa na pesa?’…hiki kikawa kikwazo kwake.
Akaingojea sana siku ya kupata pesa, hiyo siku haikufika mapema kama alivyotaraji. Hata siku Joy anamweleza juu ya shida ya shilingi milioni kadhaa alihisi fadhaa ikiishi naye kwa nukta kadhaa, aliamini kuwa kama angekuwa na pesa hiyo ilikuwa siku ya kumweleza Joy kuwa anampenda. Angempatia pesa kisha angemchombeza, aliamini kuwa asingeweza kukataa. Lakini hakuwa na pesa!
Mara baada ya Joyce kutoweka, alijiendea nyumbani kwake akiwa na mawazo hayohayo. Alisikitika na kujutia sana kuikosa nafasi.
Mara akapokea simu ambayo ilibadili kila kitu.
Alikuwa ni Isaya! Isaya aliuhitaji sana msaada wake kiupelelezi kama itawezekana atambue ni nani amemteka Betty na wapi anaweza kupatikana.
Kwa sababu ilikuwa dili ya kipelelezi Fonga akaomba apewe miliuoni tatu na nusu kama kianzia ili aweze kuunda majeshi yake vizuri kwa kazi.
Kwa sababu Isaya alikuwa na shida sana, hakupingana naye. Akakubali kutanguliza milioni tatu na laki nane.
Upesi Fonga akajiandaa na kwenda kukutana na Isaya.
Akaikuta pesa tayari ipo katika bahasha!!
Akajitia kuwa yu makini sana na kazi yake.
Alikuwa amevaa miwani ya jua na koti kubwa ilhali jua lilikuwa linawaka. Alifanya haya ilimradi tu kumpagawisha Isaya na kumpumbaza kimawazo.
Isaya akauvaa mkenge. 
Fonga akatia pesa kibindoni.
Alipotoka pale akampigia simu Joyce Kidoti kwamba wakutane lipo la muhimu la kujadiliwa!! Joyce ambaye alinusurika kulala rumande siku hiyo akakubali mara moja!
Majira ya saa tatu usiku walikuwa nyumba ya kulala wageni.
Pesa ya kuwalipa watu kwa ajili ya upelelezi, ikakabidhiwa kwa Joyce Keto Kidoti. Huku mfukoni akisalia na shilingi laki nane pekee.
Ama kwa hakika, nguvu ya penzi ni mojawapo ya nguvu za ajabu zisizoonekana ulimwenguni. Mapenzi haya yalikuwa yameitafuna sasa akili ya Fonga.
Pesa ilipotoka, penzi nalo likatolewa.
Bwana Fonga akakiri kuwa alikuwa sahihi kabisa kusema, asingeweza kumpata Kidoti iwapo haipo pesa ya kutangaza nia hiyo.
Cha kustaajabisha zaidi ni penzi la usiku ule, hakika lilikuwa maridjdhawa na sasa Fonga yupo kitandani kwake akiitafakari siku hiyo nzima ilivyoanza kwa tabu na kuisha kwa furaha iso’ kifani.
Fonga akapiga funda kubwa la kahawa iliyoanza kupoa. Kisha akajikita katika wazo la ziada. Wazo kuhusu ile pesa aliyoitoa.
Alitambua kuwa ile ilikuwa pesa ya kazi, lakini mapenzi yakaizidi nguvu kazi iliyokuwa mbele yake.
Ghafla akashambuliwa na wazo la ghafla!
Kama ile pesa ilitolewa kwa ajili ya kumpata Betty, basi hata ikiwa katika mikono ya Joy bado ilikuwa ni kwa ajili ya kumrejesha Betty.
Hapa sasa Fonga akavamiwa na wazo kuwa anatakiwa kufanya kila namna Joy aweze kumshirikisha juu ya Betty na jinsi gani atazitumia pesa zile kuweza kumwokoa.
Kwa kulijua hili, iwapo Betty atapatikana basi Fonga angeweza kumhadaa Isaya kuwa ni juhudi zake hadi hapo kumwokoa. 
Hili lilikuwa wazo sahihi kabisa. Wazo lisilokuwa na utata wa aina yoyote. 
Kisha akajikumbusha kuwa Joy anatakiwa kukolea haswa katika mapenzi ili aweze kudiriki kumsimulia juu ya Betty na mbinu ambazo anahitaji kuzitumia kumpata. 
Ni hapa Fonga alipokiri kuwa, anatakiwa kumtawala kiakili mtoto wa chuo kikuu, mlimbwende nambari wani. Joyce Keto.
Fonga akajipa moyo kuwa elimu yake ya kidato cha nne itamwongoza vyema ikisaidiwa na elimu ya mtaani.
Kitu cha kwanza kabisa alihitaji kujua kwa nini Betty ametekwa? Hili lingempa mwongozo mpana sana hadi kufahamu kwa nini Joyce adai milioni kadhaa kwa ajili ya kumwokoa?
Na kwa nini alimtuma Fonga kumfuatilia siku ile ili asifanye mapenzi na Isaya?
Swali hili lilimshtua sana Fonga. Siku yeye alipoagizwa kumfuatilia Betty nd’o siku hiyohiyo ambayo Betty alitekwa na kupotea moja kwa moja hadi wakati huo pakiwa hakuna taarifa yoyote.
Lazimkakuna kitu Joy anatambua hapa!! Na ili mambo yaende sawia, lazima awe name bega kwa bega kama mpenzi wake.
Kwa kufanya hivyo nitazijua siri zote na kisha nitafaidi pesa ya Isaya!!
Alijisemea Fonga huku akirusha miguu yake huku na kule kama kwamba jambo hilo ni dogo na litamalizika mara moja!!
Laiti angejua kisa cha Betty kutoweka, laiti angeonyeshwa japo kwa sekunde kadhaa tu mchezo ambao anataka kuingia kuucheza.
Basi angeghairisha mara moja na kuendelea na maisha yake ya kuunga-unga jijini Dar es salaam!!
Lakini Mungu ni wa ajabu, hata sekunde moja ya mbele yako hujui nini kitatokea.
Fonga mtoto wa Manzese, akajiingiza kichwakichwa mchezoni!!

**BETTY ametekwa kwa sababu zipi? Na yupo wapi?
***JOYCE anatakiwa kuwa na pesa kamili aweze kumwokoa rafiki yake. Je atafanikiwa katika hili.
***ISAYA anamtegemea FONGA, FONGA naye anamtegemea JOYCE, JOYCE naye anaitegemea sauti katika simu!!!

Ni kizungumkuti…..

##SHARES, LIKES, COMMENTS ndo mapambo ya uwanja wetu…TUUPAMBE!!

ITAENDELEA

Post a Comment

Previous Post Next Post