RIWAYA: ROHO MKONONI 18


RIWAYA: ROHO MKONONI


MTUNZI: George Iron Mosenya

SEHEMUYA KUMI NA NANE

Asubuhi na mapema walikuwa mbele ya meza ya kung’ara ya Mzee Beka.
“Sijaona kichwa cha habari hata kimoja juu ya kifo chake!!” Beka aliunguruma huku akizunguka katika kiti chake.
“Bwege kapitia dirishani…sijui kashtukaje tu” alijibu kiongozi wao.
“Yeye nd’o bwege ama nyie aliyewatoroka?mnamuita bwege, yaani anapita na yule Malaya wake dirishani mnasema bwege. Bastard!!!” aling’aka huku akitabasamu, vijana wale wakatambua kuwa amechukizwa na kilichotokea. Kila alipokasirika alikuwa akitabasamu.
Hawakuwa na cha kujibu!!!
“Sihitaji maelezo marefu zaidi. Sitanunua gazeti lolote hadi mtakaponiletea gazeti likizungumzia kifo cha Fonga!!” aliamrisha kisha akafanya ishara ya kuwafukuza vijana wale!!
“Na sihitaji kukaa wiki nzima bila kusoma magazeti….” Alimalizia huku na wao wakimalizia kutoka nje ya ofisi ile.
Beka akisema huwa anamaanisha!!
Hilo walilitambua, kila mmoja akaondoka na lake kichwani. Kasoro Malle tu!!

****

SAA nane usiku,si Joyce wala Fonga aliyekuwa amepata usingizi. Japo walipeana migongo na kila mmoja kutulia kana kwamba amesinzia.
Joyce ndiye aliyekuwa na hofu zaidi. Mwanzo alijihisi yu salama sana na mtu ambaye alistahili kuonewa huruma alikuwa ni Betty pekee. Sasa mambo yamebadilika na yeye anahofu juu ya uhai wake.
“Fonga….we Fonga!!” Joyce aliita huku akimtikisa Fonga.
Fonga akageuka na kutazamana na Joyce.
“Ni nini kimetokea, na ule mlipuko sijui risasi, kuna nini Fonga?” aliuliza Joyce.
Fonga akachefuliwa na lile swali, lilikuwa la kitoto sana, Joyce alifahamu fika kuwa wote walikuwa katika kukimbia uliposikika ule mlio. Sasa kulikoni anamuuliza yeye. Alitaka kumjibu vibaya lakini akajionya kuwa Joyce anaweza kumfikiria vibaya. Isitoshe bado hajawa na uhakika kama penzi litachanua ama kusinyaa na kutoweka.
“Tutazungumza asubuhi Kidoti. Kwa sasa lala!! Maana halipo jipya.” Alijibu kisha akampa tena mgongo..
“Ah ah Fonga…nataka kujua sasa hivi.” Alilazimisha huku akimgeuza tena yule mwanaume.
“Kidoti, nikikwambia unatafutwa uuwawe nd’o kipi sasa utafanya usiku huu.” Alisema kwa hamaki kidogo.
Joyce akakodoa macho, akajutia kulazimisha kuelezwa jambo hilo usiku huo. Japokuwa alikuwa amelala kitanda kimoja na Fonga bado hakuhisi amani, akaamua kumkumbatia kabisa ili aamini kuwa wapo wote kitandani.
Usingizi ulimpitia baadaye sana!!!

***

UZURI wa chuo kikuu cha Dar es salaam ni uwingi wa wanafunzi. Unaweza kusoma miaka mitatu na ukamaliza masomo yako bila kufahamu wanafunzi wenzako.
Baadhi ya masomo kuna wanafunzi hadi mia nane. Hivyo ni ngumu sana kumfahamu mwanafunzi mmoja mmoja. Vinginevyo uamue kabisa kumfahamu kwa matakwa binafsi.

Hakuwahi kuvaa mavazi ya aina ile, lakini siku hii alilazimika kuyavaa. Nikabu!!
Alikuwa akionekana macho yake tu na viganja vya mikono. Alikosa amani kabisa lakini alilazimika kuwa hivyo!!
Miezi iliyobaki ili mwaka wa chuo uweze kumalizika ilikuwa mingi sana kutokana na hali halisi.
Kwanza rafiki yake kipenzi hajulikani alipo, kabla hajakaa sawa anakutana na mwanaume anampatia pesa naye anampatia penzi.
Hii haikuwa jibu!! Bado likaongezeka jingine la kuvamiwa nyumbani kwake akiwa na huyo mwanaume. Tukio hili la ajabu linamtatanisha na kumweka katika maswali.
Akiwa hana ndugu wala rafiki, anaamua kumuamini Fonga. Mwanaume ambaye alimpa pesa kwa penzi kisha wakakumbanana tukio la ajabu.
Akaamua kumsikiliza Fonga kwa atakalosema. Hakuwa na ujanja!!
Hakuijua historia yake lakini akaamua kumuamini!!
Sasa Fonga alikuwa amemuamuru awe anavaa Hijabu ambalo ataificha sura yake humo. Akapewa sharti la kutoitembelea tena nyumba yake iliyovamiwa usiku ule. Fonga alisema mengi ya muhimu!! Joyce akayasikiliza kwa makini moja baada ya jingine.
Kisha akaambiwa neno la mwisho!! Naye akalikariri.
“Mengineyo niachie mimi!! Betty anarudi na wewe chuo unamaliza”
Joyce akatii. Kwani maji ya shingo tayari yashamfika.
Sasa alikuwa darasani akifuatilia kipindi huku akijiuliza nini hatma yake.
Alipishana na rafiki zake bila kuwasalimia.
Jambo lililomtesa zaidi!!
Joyce akahamia nyumbani kwa dada yake Fonga aitwaye Zubeda!!
Zubeda akamtambua kama wifi yake!!
Maisha yakaendelea!!!

*****

BEKA, mzee aliyefanikiwa kuzichuma sana pesa enzi za ujana wake alikuwa amekaa kitandani akitafakari mambo mengi sana kwa wakati mmoja.
Ilikuwa ni siku ya tatu, kimya kikiwa kimetanda. Hakuna gazeti lililoletwa katika ofisi yake. Hiyo ilimaanisha kuwa Fonga alikuwa hai na Joyce bado alikuwa mtaani.
Hii ilikuwa ni fedheha sana kwake, na alikosa imani na vijana wake wa kila siku ambao anawaamini kuwa hawawezi kumuangusha.
Sasa walikuwa kimya!!
Mzee huyu ambaye jina la Beka lilikuwa limetapakaa kuliko jina lake la kuzaliwa alikuwa akimtafakari Fonga kisha akamfikiria Joyce Kidoti. Akawaweka katika mzani na kuona Fonga anafanya uvunjaji wa haki za binadamu kuwa katika mahusiano na msichana yule. Beka aliamini kuwa hawaendani hata kidogo!!
Sasa alikuwa anaitaka roho ya Fonga na akimtaka Joyce akiwa hai!! Lakini atampata vipi iwapo vijana wake machachali walikuwa wanaelekea kushindwa?
Swali gumu kabisa lililokosa jawabu!!
Akapiga kite cha hasira na kujitupa tena kitandani!!
Kisha akachukua simu yake na kuwapigia vijana wake. Akitarajia majibu yoyote yenye uhai aliishia kuambiwa, Joyce hakuwahi tena kukanyaga nyumbani kwake, na Fonga hajulikani alipo.
Kama hiyo haitoshi, Joyce haingii tena darasani!!
“Mmejaribu kuangalia kama polisi wamemchukua kwa ajili ya upelelezi wao.” Aliuliza kwa upole.
“Tumefuatilia kwa makini, polisi walikuja siku mbili tu kisha wakasema upelelezi unaendelea. Bila shaka hawakumpata.”
“Una uhakika gani kwa kusema upelelezi unaendelea wanamaanisha hawakumpata?” aliuliza huku akicheka kwa dharau.
“Niliwasiliana mapema na yule Mr. X Inspekta uliyeniunga…..”
“Haya nimekuelewa…nadhani umeelewa sasa maana ya kukuunganisha naye. Umenifurahisha kwa hilo.” Alijibu Beka kwa utulivu!!
Kisha akaendelea, “Jitahidini….hapana…hakikisheni wiki haimaliziki bila kumpata huyo mshenzi wa tabia.” Alimaliza na simu ikakatwa.
Kichwa kilikuwa kinamchemka sana, hakuamini kuwa ni Fonga alikuwa amerejea tenakatika maisha yake!!
Kwanini Fonga? Kwa nini? Alijiuliza mara mbilimbili huku akijisikia fedheha kuibughudhi akili yake kumfikiria kijana yule!!.
Amenitafuta maksudi ama bahati mbaya mimi sitajali na sitajisumbua kumpa onyo….nataka kusoma gazeti kuwa Fonga amekufa…..tena kafa kinyama!!! Alisema kwa sauti ya juu huku akihaha kujirusharusha katika kitanda chake cha kifahari.
Kabla ya kulala, alipiga simu mahali kuwa anajisikia hovyo na daktari amemzuia kufanya shughuli zozote, hivyo hataweza kuhudhuria mkutano wao walioupanga!!

*****

TAARIFA ya Joyce kuvamiwa ilisambaa kupitiamarafiki zake, walihaha kuupata ukweli juu ya wapi Joyce atakuwa amepelekwa.
Ilionekana balaa sana hali hii ya mwanafunzi kutekwa. Tena mwanafunzi mwenyewe Joyce Kidoti. Msichana maarufu kabisa.
Kila aliyemjua alipatwa na mafadhaiko.
Polisi waliowahi kufika eneo la tukio walifanya mahojianona majirani, pia katika upekuzi wakafanikiwa kupata kitambulisho cha kupigia kura!!
Joyce Kisaka!! Kilisomeka hivyo!!
Siku iliyofuata wakaenda katika uongozi wa chuo kikuucha dar es salaam. Wakaelekezwa ofisi inayoshughulika na mambo ya wanafunzi, ‘Dean of student’. Huku wakamuulizia Joyce Kisaka.
Mwanamama mratibu wa ofisi ile akasaka hilo jina na majibu yakawa ‘hakuna mwanafunzi aitwaye Joyce Kisaka’ katika orodha yake.
Polisi wakashangaa, kwani kila aliyekuwa jirani nanyumba hiyo alitambua kuwa mkaaji wa nyumba ile alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Japo hawakujua ni mwaka wa ngapi.
“Nilisikia wakisema anaitwa Kidoti sijui…” alisema polisi mmoja jina hilo maarufu.
“Ahaaa!! Joyce Kidoti…..huyo sawa!!” alisema kwa furaha yule mwanamke huku akibofya kompyuta yake na kisha kuwaonyesha sura iliyopo katika jina la Joyce Keto.
Sura ya Joyce Keto na Joyce Kisanga ilifanana. Kikubwa zaidikilichofananisha sura hizikilikuwa ni kidoti.
Polisi wakajiuliza kwanini anatumia majina mawili tofauti.
Hawakujua kuwa Joyce Keto ni jina la kununua tu na jina halisi ni Joyce wa Kisaka.
“Huyu Joyce Keto unayemsema unamtambua uwepo wake chuoni?” askari mmoja alimbana swali yule mama asiyeisha kutabasamu.
“Aaaah…..ok….hebu ngooja..” aliongea kwa kusita huku akibofya kompyuta yake.
“Alright!! Joyce Keto ana ruhusa, alichukua siku ya jumatatu, siku nne zimepita sasa si leo nd’o ijumaa eeh.” Alisema yule mama. Kisha akaendelea, “Halafu alisema akifika Makambako atanipigia huyu mtoto jamani.” Alilalama.
Polisi wakaduwaa, nyumba anayoishi ilivamiwa siku ya jumatano.
Ina maana Joyce aliondoka siku mbili kabla? Kwa hiyo hajui kaqma amevamiwa? Haya yakawa maswali.
“Hivi kwani nyie ni kina nani jamani eeh maana siwaelewi elewi.” Ghafla yule mama kutabasamu akaficha tabasamu lake sasa akawa makini, na kuwauliza wanaume wale.
Wakajitambulisha kuwa ni askari, tabasamu likaendelea!!
Polisi hawakuwa na jingine.
Tukio la nyumba ile kuvamiwa likahesabiwa kama kesi ya kawaida tu ya ‘kuvunja na kuiba’.
Cha msingi aliyehisiwa kujeruhiwa alikuwa hayupo siku ya tukio basi amani ikatawala tena!!

Kwa akili hii ya kushikiwa na Fonga, Joyce alitikisa kichwa na kukiri kuwa Fonga alikuwa ‘Babu kubwa’. Kwanza katika mchezo huu alianza kwa kuwaondoa polisi mchezoni, wasijisumbue kumtafuta Joyce ambaye hakuwepo siku ya tukio.
Pili alimtengenezea Joyce mazingira ya kutuliza akili yake, ili asije akafeli masomo yake ambapo mitihani ilikuwa imekaribia!!
Huo ukawa mwisho wa Joyce kuhudhuria chuoni kwa amani huku akiwa na ruhusa maalumu. Ruhusa ambayo aliipata tarehe ya kufoji kwa kutoa pesa.
Mama kutabasamu akaingiza katika pochi shilingi laki moja.
Japo alitokwa kijasho kusikia Joyce anatafutwa na askari, lakini hakuthubutu kumkana kutokana makubaliano.
Kwa kufanya hivyo angejipotezea pia kibarua chake alichosotea mpaka kukipata!!
Mchezo ukaendelea vyema!!
Fonga akazichanga karata!!
Joy akaendelea kuishi na Zubeda maeneo ya Machimbo!!!

****

ISAYA alikuwa mmoja kati ya wanachuo ambao si tu walikuwa wamechanganyikiwa bali walikuwa wanakaribia kurukwa na akili kabisa.
Taarifa ya kupotea kwa Betty ikiwa haijatulia katika kichwa chake, mara anasikia Joyce Kidoti kavamiwa,jibu la kwanini kavamiwa nalo likiwa halina wa kujibu. Linatokea zito jingine kabisa kuwa siku anayovamiwa hakuwepo kwake.
Uthibitisho zaidi ni kuwa alikuwa na ruhusa siku mbili kabla.
Isaya akachanganywa sana na taarifa hii!! Akaiona kama ni ya kuundwa vile. Lakini nani wa kuiunda kisomi kiasi kile? Alishangaa.
Hakika alitakiwa kuhisi hivyo maana. Siku ya jumatano kuna rafiki alimtembelea Joy kisha akampigia simu Isayana kumwambia kuwa ametoka kwa Betty muda mchache uliopita.
Lakini katika kuvamiwa inasemekana Joyce hakuwepo.
Hapana!! Joyce katekwa si bure hii!!
Isaya alikataa kata kata yeye na nafsi yake.
Katika kukataa huku akaamua kumpigia simu Fonga ili aweze kumpadili la kumfuatilia Joy huku akiendelea kuhakikisha Betty anapatikana.
Akajaribu kupiga simuya Fonga!!
Simu haipatikani!!!
“Fonga naye kwa vimeo aaargh!”alilalamika, huku akijaribu tena na tena pasi na mafanikio.
Isaya hakutaka kulazia damu hili jambo, kwa sababu alipajua nyumbani kwa Fongaakaamua kumfuata huko huko.
Hakuwa na hofu na lolote kwa sababu alikuwa anatumia gari binafsi. Hata asingemkuta bado isingemgharimu chochote.
Isaya akaenda peke yake nyumbani kwa Fonga.
Akapita njia za mkato Mabibo, akaibukia Manzese.
Nyumbani kwa Fonga hapakuwa na mtu.
“Alikuwa hapa leo lakini akaondoka, hakusema anaenda wapi.” Kijana mmoja alimjibu Isaya.
Gari lilipotoweka kijana yule akanakiri namba!!
Huyu alikuwa ni kijana wa Fonga!!
Kijana katika oparesheni yake ambayo alikuwa hajaipa jina.

****

Wakati Isaya anafika nyumbani kwake. Yeye Fonga alikuwa njiani kuelekea Machimbo kuonana na Joyce. Kuna jambo muhimu ambalo Joyce alihitaji kujadili naye, hata Fonga naye alihitaji kumweleza Joyce juu ya maendeleo ya mchakato huo ambao kwa wakati huo ulikuwa mchakato wa kumrejesha Betty uraiani akiwa hai.
Kama walitarajia kuonana kwao ni kwa ajili ya kujadili kuhusu Betty pekee basi hawakuwa sawa hata kidogo!!
Ilizuka vita mpya,huenda ngumu kuliko ile ya awali ambayo Fonga alikuwa amejipanga kukabiliana nayo!!

**Ni kitu gani walijadili..
**Beka anataka nini kwa Fonga na Joyce??
**Je ni yeye amemteka Betty…

KUNA SIRI GANI NYUMA YA HAYA!!!!

ITAENDELEA 

Post a Comment

Previous Post Next Post