RIWAYA:ROHO MKONONI 20


RIWAYA:ROHO MKONONI


MTUNZI: George Iron mosenya

SIMU: 0655 727325

SEHEMUYA ISHIRINI

“Fonga Fonga Fonga rafiki yangu, usithubutu walau kukimbia ama kufanya vurugu ya aina yoyote, nyanyua macho yako tazama pembe ya kushoto na kulia.” Sauti ilimsihi, Fonga akatazama na kukutana na wanaume wawili, mmoja katika kila kona. Wote wakiwa na mawani nyeusi.
“Wanakutazama wewe, ukifanya aina yoyote ya usumbufu hawatasita kukupasua kichwa chako kibovu mara moja!! Hivyo kuwa mtulivu bwana mdogo!!” aliendelea bwana yule huku akiiondoa miwani yake machoni.
Wakatazamana ana kwa ana na Fonga mwenye hofu!!
Bwana yule akamkazia macho Fonga kisha akamwambia maneno bila kutoa sauti katika namna ya kusisitiza.
“Fonga, soma ujumbe katika simu yako!!” alimwambia bila kutoa sauti, hivyo Fonga alitakiwa kuusoma mdomo wake jinsi unavyocheza cheza.
Kwa mara ya kwanza Fonga hakuelewa kitu lakini kwa mara ya pili Fonga ambaye alikuwa mtu wa kupenda kujua mengi alipokuwa gerezani alizikumbuka ishara mbalimbali zilizokuwa zikitumika gerezani hasahasa pale ambapo wafungwa wanafanya mawasiliano bila mnyampara kuwasikia ama kujua kinachoendelea. Wafungwa walizungumza kwa ishara za midomo na macho na walielewana sana!!
Fonga akausoma mdomo na kuuelewa unamaanisha nini, lakini angeweza vipi kumuamini yule bwana asiyemjua?
Pia alishangaa huyu bwana ameijuaje namba yake mpya upesi kiasi hicho hadi amsisitize kuusoma ujumbe katika simu yake?
Huu sasa ukawa utata!! Fonga alikuwa katika fumbo asijue nini cha kufanya, lakini wazo la kukimbia alishalitoa akilini upesi.
“Fonga, kama ulivyo nakusihi usimame kisha hatua za taratibu, moja baada ya nyingine fuata uelekeo ninaokuelekeza.” Sasa alitoa sauti.
Fonga hakuleta ubishi, alisimama na kuanza kufuata alichokuwa anaelekezwa. Ni kama walikuwa marafiki tu lakini waliotofautiana kauli, hakuna mtu ambaye angeweza kushtukia jambo lililokuwa linaendelea baina yao.

Ilikuwa nafasi nyingine muhimu ya Malle kumwokoa Fonga na kisha kumfahamu kiundani zaidi, macho ya vijana wa mzee Beka yalipomuona aliamua kuchukua jukumu la kumkamata upesiupesi. Alifanya maamuzi hayo ili aweze kumwokoa.
Kabla hajamkabili alijaribu kumtumia ujumbe mfupi wa kumtahadharisha juu ya usalama wake, lakini ajabu hakumuona akijishughulisha kuitoa simu yake na kusoma ujumbe. Ni hapa alipoamua kumkabili na kwa usalama wake kwani alikuwa amevaa vinasa sauti ambavyo vilisafirisha kila alichokiongea na kuwafikia wenzake. Hivyo ilikuwa mtihani mwingine kumweleza Fonga juu ya jambo linalokaribia kumtokea.
Malle, alipomweleza Fonga asimame na kufuata maelekezo yake alikuwa katika uelekeo wa kumtegesha Fonga mahali pasipokuwa na watu wengi ili kuwapa nafasi wenzake ambao walikuwa tayari kuua waweze kufyatua risasi na kummaliza Fonga!!
Roho ilikuwa inamdunda sana kwa tukio ambalo alikuwa anakaribia kulishuhudia!! Nafsi ilimsuta. Akaukumbuka uchangamfu wa Fonga, akazikumbuka harakati zake ambazo zilimpa umaarufu.
Akakikumbuka na kisa ambacho kinasababisha Fonga auwawe, kilikuwa kisa cha kiuonevu sana. Malle hakuwahi kushiriki katika mauaji ya kionevu kama yaliyopangwa kwa ajili ya Fonga!!
Yaani Fonga huyu huyu aliwahi kusota miezi tisa jela na mingine mine rumande kabla ya hukumu. Kisa Monica!!
Msichana ambaye alikuwa katika mapenzi na bwana Beka, kisha akaachana naye na kujihusisha na Fonga. Bila Fonga kutambua kuwa alikuwa ametoka kumwacha kibopa yule kwa mbwembwe zote.
Fonga akajikuta matatani, akafungwa akijua amefungwa kionevu kabisa, angefanya nini wakati mwenye pesa alikuwa ameamua?
Sasa Fonga akiwa mtaani tena anakumbwa na mkasa huyu, dhidi ya bwana Beka tena kisa tu bwana Beka anamtaka Joyce kinguvu na Joyce hamtaki!!
Malle akauhesabu huu kama uonevu dhidi ya mtu mtaratibu sana akaamua kumpigania tena.
Roho ya Fonga ilikuwa mikononi mwa Malle.
Kwa akili ya upesi ya kuzaliwa, Malle alipoukaribia mlango alijifanya kupishana vibaya na muhudumu wa hoteli ile, mara wakagongana, kinasa sauti kidogo kilichokuwa sikioni kikadondoka.
Akainama upesi kukichukua lakini hakufanya juhudi za kukirejesha sikioni, mawasiliano baina yao yakawa yamekatika.
Tukio hili la kugongana na muhudumu lilionwa na wenzake kutoka pande zote za ukumbi ule.
Hawakujua kuwa Malle amefanya yale maksudi!!
Sasa aliweza kuongea bila wao kumsikia.
“Fonga, sikiliza Beka ameagiza uuwawe, nipo upande wako. Ni mimi niliyekutumia ujumbe ulipokuwa na Joyce siku ile pale kwake hatimaye ukapitia dirishani, sasa sikia. Naomba ufanye jambo moja la kuwahadaa wale wenzangu. Akili yako ifanye kazi upesi sana, Fonga yaani upesi sana. Naamini utaweza, ukisikia nasema neno maliza, timua mbio. Haraka..uwashe simu yako nitawasiliana na wewe.” Alimaliza kuzungumza kwa sauti ya kawaida kisha akajiweka makini na kukivaa tena kinasa sauti.
“Fonga utasimama hapo hadi nikuruhusu mimi kuondoka, na hautaondoka bila kunijibu maswali yangu!! Sina hofu kuhusu wapiti njia. Nitakisambaza kichwa chako na hautakuwa na nafasi nyingine ya kujutia ulichokifanya pumbavu mkubwa” Malle alibwatuka maneno yale kwa ghadhabu kuu. Fonga akawa katika mchanganyiko wa hofu na uoga.
“Brother one, Brother two. MALIZA!!”

Mlio wa bunduki haukusikika lakini hekaheza zilizushwa na mtapakao wa damu eneo lile, kila mmoja alihaha na kujiuliza nini kimetokea. Mabonge makubwa makubwa ya damu yalikuwa yameharibu hali ya hewa.
Ulikuwa ni mshikemshike.
Mwili wa mwanadamu ulikuwa umetulia tuli chini. Haukutamanika kuutazama hata kidogo. Ulikuwa ni mwili usiokuwa na kichwa. 
Yalikuwa mauzauza ya ghafla sana kutokea pale.
Malle hakugeuka mara mbili kutazamana na maiti ya Fonga, matone ya damu katika nguo yake yalimaanisha kuwa Fonga alichelewa sana kukimbia.
“Nilijaribu kadri ya uwezo wangu!!” alisema kimoyomoyo huku akitoweka eneo lile ambalo halikuwa salama tena.
Malle akatokwa namachozi baada ya miaka mingi kupita. Tukio lile lilikuwa limemuumiza sana. Kuuwawa kwa mwanadamu kiuonevu. Tena mwanadamu ambaye wanafahamiana.
Heka heka zile zilizoondoa amani katika eneo lile zilimfanya Beka pia aamue kuingia chumbani kwake. Aliongozana na Joyce Kidoti Keto.

****
BEKA alikuwa katika shangwe kuu, alifurahia taarifa ya tetesi kuwa yule bwana aliyepigwa risasi maeneo ya Rombo Green View ni Fonga. Taarifa hii ya tetesi alipewa na kijana wake aendaye kwa jina la Malle.ni huyu ambaye alikuwa amemuweka Fonga katika mtegowa kufyatuliwa risasi na jukumu la kufyatua likibaki kwa wale vijana wengine.
Sasa Beka alikuwa chumbani na Joyce. Alikuwa katika kutimiza lengo lake la pili. Kummiliki Joyce moja kwa moja hasahasa baada ya Fonga kuuwawa.
Beka akiwa na furaha ileile mara simu yake iliita, alipoitazama ilikuwa ni namba mpya.
“Bernad Kamara” sauti ilimuita upande wa pili, haikuwa sauti ngeni.
“Naam, nani mwenzangu.” Aliitika katika sauti ya utulivu sana.
“Muache huru binti huyo uliyenaye na kisha bila kushurutishwa mwache Betty huru. Kisha endelea na mambo yako bila tatizo.” Alisisitizwa kwa sauti iliyotangaza amani na humohumo ikitangaza vita.
Maneno kutoka simu yalilifikia sikio la Joyce, akajikaza kama ambaye hajasikia neno lolote lakini asingeweza kujikaza zaidi.
“Wewe ni nani na unanipigia simu ya kunipa vitisho vya kitoto.”
“Hutakiwi kunifahamu Beka maana haitakusaidia lolote. Mwache Joyce bila kumfanya lolote muathirika wa Ukimwi mkubwa wewe, mwache huyo mtoto. Natambua kuwa ulimuua Monica kwa sababu angekutangaza kuwa ulimwambukiza Ukimwi, mwache Joyce asome…mwache Betty huru pia….kwani hao wamekukosea nini?” sauti ile iliendelea kuuliza.
“Unasema nini mpumbavu wewe. Hivi unatambua mimi ni nani? Unatambua kuwa unazungumza na nani shenzi wewe.” Beka alitaharuki, yaliyosemwa yalikuwa na ukweli ndani yake. 
Huyu ni nani sasa ajuaye kuhusu yeye, huyu ni nani huyu?
“Roho yako ipo mikononi mwangu dakika hii hapa. Lakini ipopia katika maamuzi yako. Sikutishi bwana Kamara Benard. Namaanisha kuwa, mwache huru binti huyo? Mwache mara moja na yule mwenzake mwache huru.”
“Weweni nani kijana. Na nani amekupatia namba yangu ili upige simu kunichafua?”alihojihuku akiwa anatabasamu. Hasira ilikuwa imempanda.
“Fonga wa Fonga, napiga simu kutoka kuzimu!!” akajitambulisha kisha simu ikakatwa!!!
Beka alivyopiga haikuwa ikipatikana. 
Wacha wee!! Beka alihaha, mara avute shuka mara ashikelaptop yake, mara achukue taulo.
Joyce Keto akiwa katika nguo za kulalia alikuwa akimtazama kwa uoga mkubwa sana.
“Joyce mpenzi …..eehh hivi umemsikia huyo mjinga?” aliuliza Beka huku akiwa anaona haya kumtazama Joyce machoni.
“Amesemaje?” aliuliza kinafiki Joyce.
“Achana naye ni mjinga mmoja tu anataka kunichafua” alijibu Beka huku akirejea tena kitandani bila kuwa amefanya walau moja ya jambo lolote alilonuia kufanya.
Hali ilikuwa tete!!

****

MIKONO ya Fonga ilikuwa inatetemeka sana wakati akiwa kandokando ya barabara ya Shekilango akitazama hekaheka za hapa na pale kuwatazama wananchi walivyokuwa wanalia na wengine wakiogopa kuutazama mwili usiokuwa na kichwa.
“Kwa hiyo ningekufa vile ama!! Beka nilikukosea nini?” alijiuliza huku akikosa muhimili thabiti na asiamini kama yu hai tena.
Ghafla akamkumbuka bwana ambaye alimwokoa kutoka katika mauti yale ya mara ya pili. Sasa alimuamini kupita maelezo na kuelewa kuwa bwana yule hakika alikuwa na kitu cha ziada.
Fonga akalivua shati lake lililopata madoa kadhaa ya damu ya mwanadamu, akasalia na fulana yake isiyokuwa na mikono.
Akajitupia garini na kuondoka zake huku akijiuliza Beka atamfanya nini Joyce. Lakini asingeweza kurejea tena eneo lile mpaka akili yake ipate utulivu kiasi fulani.
Safari yake iliishia Manzese, huku hakuelekeakatika chumba chake. Bali alienda katika vyumba vingine walipoishi marafiki zake ambao alishirikiana katika mambo mengi.
Ni huku alipoweza kufungua simu yake ambayo aliweka namba yake ya siku zote.
Akakutana na jumbe mbili tofauti ambazo zilikuwa na maana kubwa sana kwake. Kwanza akakutanana ule ujumbe wa kumsihi atoweke eneo lile (Rombo Green view) kwani si salama, ujumbe huu haukuwa na maana tena. Lakini ujumbe wa pili ulikuwa na maana zaidi na ulimfanya awe na kiburi cha kuamini kuwa atamshinda mpinzani wake.
Lakini alisikitika kuwa kijana aliyejisajili simu yake kwa jina la ‘Malemi Stanslaus’ aliamini kuwa yeye ni maiti, kwani ujumbe mwingine uliingia ukisema ‘NILIJARIBU KILA NIWEZAVYO R.I.P Fonga’.
Fonga akatabasamu na hapo akaamua kujiita Fonga kutoka kuzimu!!
Hata alivyompigia simu Beka na kumweleza juu ya maasi yake alikuwa akijiona kama mfu, na hakuhofia kuhusu kifo.
Kama alitakiwa kufa kwa kupigwa risasi ya shingo, na sasa yu hai. Kuna lipi jingine la kuhofia.
Hakuwa na lolote la ziada.
Fonga akaingia katika chumba kimojawapo cha bafuna kujisafisha mwili wake, kisha akabadili nguo zake.
Rafiki zake walikuwa wakimtazama kila mara wasiamini kama yu hai tena!! Maana kwa alichowasimulia ni kama filamu tu!! Filamu ya kutisha na kushangaza.

****

Alichofanikiwa Joyce ni kumshawishi Beka kwa mara ya kwanza atumie kondomu, hilo alifanikiwa.lakini baada ya simu ile, mambo yakabadilika Beka akalazimisha wafanye mapenzi bila kinga, kisa tu alikuwa na mpango wa kumuoa siku za usoni hivyo hata akipata mimba si tatizo kwake.
Joyce alikataa katakata huku akilia na kumzuia Beka.
“Kwa hiyo hicho kiFonga chako nd’o huwa unakubali bila kondomu sivyo, sasa ni heri unichukie lakini hutoki humu ndani hivi hivi. Nasema hivi ama zangu ama zako maana ninapokubembeleza Joyce unaniona mimi fala kabisa. Umalaya wako alokufundisha mama yako sasa hapa umefikia kikomobastard!!” Beka akapandwa na hasira na kujikuta akitokwa na maneno hayo mazito, huku akihaha kupambanana Joyce.
Joyce alikuwa ni yuleyule aliyembwaga dada mkuu wa shule ya Kifanya mjini Njombe baada ya kujaribu kumnyanyasa na kisha akafikia mbalina kumtukania mama yake ambaye tayari ni marehemu. Beka naye akamtukania mama yake.
Joyce akapandwa na hasira na hatimaye akamkabili. Akamrukia na kumshambulia kwa kucha zake huku akitweta kwa hasira.
Beka hakutegemea shambulizi kutoka kwa mrembo yule,akajirusha kando lakini Joyce alikuwa mwepesi na tayari kwa lolote, pale unapomtukania mama yake.
Joyce akamvagaa Beka na kufanikiwa kumtupa chini,hapa sasa ikajirudia ile filamu ya Joyce nadada mkuu wa Kifanya.
Joyce aliyekuwa maridadi katika kufuga kucha ambazo zilipakawa hina na kuwa imara zaidi alianza kushambulia kwa kufinya uso wa mzee Beka. Mara amfinye kifuani.
Beka akaanza kusota kwa maumivu, kabla hajakaa sawa Joyce akamdokoa machoni.
Ebwana ee!! Beka akaanza kulia kama mtoto mdogo.
Joyce akamwachana kuruka kitandani aweze kuchukua nguo zakew avae na kuondoka. Beka akasimama na kumuwahi huku akiona kwa kutumia jicho moja.
Kosa alilofanya Beka ni kumkaba Joyce kabali kwa nyuma.
Kabla kabala ile haijanoga. Joyce makucha alitumia tena makucha yake. Akaurusha mkono ukatua mahali sahihi alipokuwa anahitaji.
Mkono ukakamata korodani za Beka, kisha kucha imara zikabinya huku zikifinya.
Sio balaa hili???
Beka akalegeza ile kabali, akanyanyua miguu yake na kusimamia kucha!! Macho akayakodoa mpaka usawa wa mwisho.
Hauhitaji kusimuliwa maumivu yanayotokana na shambulizi la namna ile. Beka hakuwa na ujanja.
“Beka unataka kuniambukiza mimi ukimwi, unataka kuniua maksudi, kumbe ni wewe ulimuua Monica, kumbe ni wewe unamshikilia Betty. Beka wewe ni mnyama,mnyama kabisa hufai kuendelea kuishi hayawani wewe.” Joyce alikaripia huku akizidi kumbana.
“Sasa ili tusiende mbali nakuomba usiniguse hadi nitakapotoka nje ya chumba hiki, vinginevyo nitakuua Beka. Nitakuua” alitisha Joyce, Beka akakubali.
Joyce akavaa nguo zake huku akimtazama mzee yule iwapo atafanya lolote.
“Fungua mlango!!” aliamrisha Joyce.
Beka akapiga hatua. Akaufikia mlango na kuufungua.
Joyce akapiga hatua aweze kutoka nje, na hapa mambo yakambadilikia. Beka aliachia teke moja madhubuti likatua katika tumbo la Joyce Kidoti. Binti akarushwa nyuma na kutua kitandani.
Beka akamuwahi tena na sasa akawa amemkalia kwa juu.
Kipigo kitakatifu kikafuata!! Joyce alipokea ngumi nzitonzito kutoka kwa Beka.
“Sasa na wewe unamfuata huyo Monica wako sawa eeeh!!” alisema Beka, wakati huo damu zikiwa zimeyachafua mashuka haswa. Joyce alikuwa hoi.
“Yaani Monica ameniambukiza Ukimwi halafu mnasema mimi ndo nimemwambukiza sivyo,sasa nakuua ili ukamuulize yeye mwenyewe nini mkasa wa kifo chake sawa eeh.” Alizidi kuwaka. Beka alikuwa ameingiwa na roho ya kuua. Hakuwa na huruma zaidi.
Mara mlango ukafunguliwa, ilikuwa kama kimakosa hivi, lakini hapakuwa na kosa lolote. Mara wakaingia wanaume wawili na mwanamke mmoja.
Beka akakumbuka kuwa aliacha mlango wazi baada ya kufuata sharti la Joyce alipotaka amfungulie mlango aondoke.
“Bernad Karama, mheshimiwa mbunge wa jimbo la madhambi una swali la nyongeza?” sauti ya kiume iliuliza. Sauti ambayo Beka alikuwa anaifahamu.
Alipotazama vyema akakutana na mshtuko wa mwaka 2008.
Alikuwa anatazamana na marehemu Fonga!!
Alipokodoa macho, Fonga akatambua kuwa alikuwa akiuliza swali kuwa ‘si umekufa wewe?’ naye akalijibu.
“Nimekufa lakini nimerejea kidogo tu kukuletea salamu zako kutoka kuzimu!!”
“Fonga…” sauti ya mshangao kutoka kwa Joyce!!.
“Beka kuzimu wanakuhitaji!! Ni hilo tu.” Alisema kwa hasira kiasi safari hii.
Beka akapagawa!! Hakika alikuwa amekamatika.
Wakati Beka akidhani kuwa mtu mwenye kumtia hofu ndani ya chumba kile ni Fonga peke yake, haikuwa hivyo!!
Vichwa vitatu ndani ya chumba kile vilikuwa vimekamilika haswa!
Alipojaribu kufurukuta, alijikuta akitua katika mikono ya mwanamama. 
Kilichomtokea hakukitegemea kutoka kwa mwanamke!!
Meno mawili yakadondoka chini.
Alipigwa kichwa kimojatuna yule mwanamama ambaye alikuwa kimya na hata alipomtoa meno hayo bado alikuwa kimya kama vile sio yeye aliyempiga na kichwa.
Beka akatua chini kama meno yake, sasa alikuwa amepiga magoti damu zikimtoka mdomoni.

***BEKA matatani…….nini kitaendelea?
Je? Betty atapatikana, na yupo wapi..
Nini hatma ya Isaya?......

BOFYA LIKE ukimaliza kuisoma, pia kama kuna maoni tiririka katika ‘comment box’.
ITAENDELEA…..KESHO

Post a Comment

Previous Post Next Post