ROHO MKONONI
MTUNZI: George Iron Mosenya
SIMU: 0655 727325
SEHEMU YA KUMI NA NNE
“Kidoti…..Fonga naongea hapa!!” alijitambulishakisha akaacha nafasi kidogo ya jina lake kumuingia msikilizaji.
“Fonga,nini kimetokea kwani eeh!! Fonga amefanya nini Betty kwani..”
“Punguza papara Joy. Hili jambo ni zito kiasi fulani na hata mimi linanichanganya sana, sijuitu hata nikuelezeeje lakini naomba uelewe kuwa vijana wangu hawakufanikiwa kumpata Betty.wamefika eneola tukio lakini hawakumkuta na baadaye nasikiakuwa ametekwa.” Alijibu Fonga kwa sauti tulivu.
Acha wee! Hapa sasa Joyce akarukakutoka kitandani akaanza kupiga mayowe huku akijisahaukuwa simu yake bado ipo hewani.
Akalia akimuita mama yake ambaye ni marehemu tayari.
Simu kutoka upande wa pili ikakatwa!!
Joyce akauhisi ule upendo ambao alidhani unatoweka kwa Betty ukirejea maradufu na kujikuta akijutia kila kitu, hakutaka kuamini kuwa Fonga hajui lolote.
Akajutia kumuamini na kumvujishia baadhi ya siri kuhusu Betty.
Alipokuja kutulia na kujaribu kupiga simu tena Betty hakuwa akipatikana.
HEKAHEKA!!!!
JOYCE asingeweza kulala,usingizi ungepatikana vipi ilhali Betty hajulikani alipo? Hakika isingewezekana hata kidogo.
Akakurupuka kutoka kitandani, mapigo ya moyo yakiwa katika mwendo usiokuwa wa kawaida. Akavaa makubadhi na blauzi yake upesi. Akatoka nje na kuufunga mlango upesi upesi huku akikosea mara tatu kuingiza funguo katikakitasa.
Alipomaliza kuufunga na kuhifadhi funguo mahali husika, akataka kutimua mbio kwa kuhisia anachelewa zaidi, lakini mara akafadhaika na kusimama huku akijishika kiuno.
Joyce hakujua alikuwa anaharakisha kwenda wapi!!
Akanyong’onyea kisha akainama kama anayetaka kukaa chini lakini akaishia kujishika magoti yake.
Halafu kwa mwendo wa kichovu kabisa huku akilia kilio cha kwikwi akarejea chumbani kwake. Akakifikia chumba akafungua na kisha kuingia ndani moja kwa moja kitandani, bila kuondoa makubadhi miguuni akajirusha kitandani.
Kichwa kilikuwa kinamuuma haswa. Akapapasa kitufe cha kuzimia taa lakini hakufanya juhudi zozote za kuizima, ikabaki inawaka.
Macho yake yalitazamana na saa iliyoonyesha kuwa tayari ilikuwa saa sita na dakika kadhaa usiku.
Na Betty alikuwa hajarejea!!
Akiwa bado akipigana ili aweze kuupata usingizi, kwa mbali alisikia mfano wa hatua za watu. Akamwomba Mungu hatua hizo ziwe za Betty.
Hatua zikazidi kusogea zaidi lakini katika mwendo kama wa kunyata. Akatulia na akiomba hatua hizo ziwe zinakuja mlangoni kwake.
Kama alivyoomba ndivyo ilivyotokea hatua hizo ziliufikia mlango wake kisha kimya cha sekunde kadhaa halafu ukasikika mchakato mdogo, bahasha ndogo ukubwa wa A5 ikapitishwa kupitia upenyo mdogo chini ya mlango wa chumba chake.
Macho yakamtoka Joy! Akataka kupiga kelele lakini akahofia kuzua balaa. Akajiziba mdomo, hatua zile zikatoweka tena na hazikurejea!!
Joy akiwa anatetemeka na kulia kama mtoto mdogo aliiendea ile bahasha na kuitazama kama mdudu ambaye akiguswa ataleta madhara makubwa. Akausogeza mkono aitwae lakini akawa anasita, akachukua kipande cha nguo akajifunga mkononi kisha akaichukua ile bahasha na kuifungua upesi.
Ndani ya bahasha akakutana na karatasi nyingine ndogo.
“BETTY ANAUZWA SHILINGI MILIONI SITA….MTEJA PEKEE NI WEWE, AIDHA UMNUNUE AMA UACHANE NAYE.
UJUMBE HUU UMELETWA KWAKO, OLE WAKO UWASHIRIKISHE POLISI! Utamkuta machinjioni huko.”
Yowe kubwa la hofu likamtoka Joy baada ya kuusoma ujumbe huu, jasho likaanza kumtiririka na miguu ikakosa nguvu, mara akaanza kulia kwa sauti ya juu kama mtoto mdogo ambaye mama yake amemgombeza.
Hofu ikawa haimithiriki! Alikuwa anaogopa sana.
Akaanza kukiogopa chumba chake, akataka akikimbie na kwenda mahali popote ambapo patakuwa salama kwake, labda polisi ni salama zaidi. Lakini ujumbe mfupi ulionya kabisa asishirikishe watu hao.
Sasa nimshirikishe nani? Mungu wangu wee!! Alipagawa Joy, akatimua timua nywele zake kwa fujo. Ni kama aliyekuwa anafanya juhudi za kujikuna baada ya kuwashwa muda mrefu.
Akatapatapa huku na kule, mwisho akaishia kitandani.
Huku alilia sana nab ado halikuwa suluhisho, mwisho usingizi ukampitia.
Saa mbili asubuhi akakurupuka na kujidanganya kuwa aliota ndoto mbaya sana usiku uliopita, ndoto ya kuletewa ujumbe wa hatari wenye maonyo.
Lakini cha ajabu alijikuta huo ujumbe upo kitandani.
Hofu ikaanza upya alipogundua kuwa ile haikuwa ndoto.
Akaupitia vyema ule ujumbe na mara hii akaona mwisho wa ujumbe kuna nambari ya simu.
Akaichukua na kuingiza katika simu yake na kisha akapiga.
Sauti nzito ikapokea simu ile!!
Joy akasalimia ‘shkamoo’ bila kujua makamo ya yule mpokeaji.
“Mimi Joyce….Joyce Kid…Keto….” Alijiumauma binti huyu huku mapigo ya moyo yakipiga kwa nguvu sana kama kwamba anaongea na mtu uso kwa uso.
“Unasemaje?”
“Ni kuhusu Betty!!”
“Tafuta hiyo pesa kisha unipigie simu!! Sihitaji simu yako bila pesa.” Akajibu sauti nzito kisha simu ikakatwa.
Kwa mara nyingine tena Joyce hakuweza kuhudhuria vipindi darasani!!
Akajiuliza ni wapi anaweza kupata pesa nyingi kiasi kile, akaumiza akili yake kisha akatabasamu alipokumbuka kuwa yeye binafsi alikuwa na shilingi laki moja tu iliyosalia katika akiba yake.
Mara akamfikiria Betty, je pesa zake zote alikuwa akizihifadhi benki ama alikuwa akitembea nazo? Ama aliziweka ndani.
Hapo akaanza kuhaha huku na kule huku akiilaani tabia ya Betty ambayo aliichagua ya kudhulumu wanaume!! Katika kutafuta akakutana na kadi ya benki ya Betty.
Joy! Akafanya ishara ya msalaba na kukumbuka kuwa namba yake ya siri haiwezi kuwa tofauti na mwaka wake wa kuzaliwa ama la itakuwa muunganiko wa tarehe ya kuzaliwa, mwezi pamoja na mwaka husika.
Betty bila kusafisha kinywa chake aliurudishia mlango wa chumba na kukimbilia katika mashine ya kutolea pesa iliyokuwa jirani.
Namba za siri za kwanza zikagoma hii ya kwanza ilikuwa ni mwaka wa kuzaliwa, akajaribu za pili huku moyo ukiwa unapiga vilivyo kifuani. Akaingiza kwa makini kabisa nambari hizo huku akiomba Mungu maajabu yatokee.
Akamaliza na kubofya akiruhusu muamala!!
Hola!! Namba za siri hazikuwa sahihi.
Hapa Joyce akapigapiga miguu chini kama msichana aliyebanwa na mkojo na choo kipo mbali. Kisha machozi yakaanza kumtoka. Ndipo akagundua kuwa nyuma yake kuna watu watatu wakimngoja katika foleni. Akajifuta machozi kwa kutumia blauzi yake, kisha akakumbuka kuwa alikuwa amebakiza jaribio moja tu na si vinginevyo. Na katika jaribio hilo akikosea tu kadi inamezwa na huo unakuwa mwisho wa mchezo.
Joy akaitwaa kadi ile akapisha wale wateja waendelee na miamala yao. Mvulana aliyepishana naye alimkazia sana macho huku akishangaa, bila shaka alikuwa akimtambua.
Joyce hakujali hilo!! Utu wake haukuwa na maana yoyote iwapo Betty yu matatani. Mbaya na nzito kuliko, alikuwa anauzwa.
Betty anauzwa!! Betty!!! Alilalamika kimoyomoyo.
Baada ya wale wateja watatu kumaliza miamala yao, Joyce alitembea tena na kuingia katika chumba kile kidogo.
Akatazama juu kisha akajisemea maneno kadhaa ambayo kwa namna moja au nyingine yalimpa ujasiri.
“Betty najua unayakumbuka mengi katika maisha yako, ulizaliwa ukasoma, ukakutana na mimi, ukafiwa na wazazi, ulinisaidia mara kadhaa. Lakini haya yote kweli ulitunza kumbukumbu mpenzi, unazikumbuka tarehe za matukio haya!!! Mimi binafsi siamini, basi naomba niingie kwenye akili yako pacha wangu, niruhusu katika akili yako katika wakati huu mgumu, niruhusu niwaze badala yako, Betty naamini hautaisahau tarehe ambayo mimi na wewe tulisikia kuwa mwalimu Japhari amekufa, lakini kubwa zaidi ile tarehe ambayo yule daktari alitupa majibu kuwa umeathirika na ugonjwa wa Ukimwi!! Mimi sijaisahau naamini hata wewe hautaisahau kamwe na ndio tarehe ambayo imekufanya uwe kama ulivyo, basi naamini hiki ambacho ninaenda kukifanya sasa!!! Naamini ni kweli…” aliyasema yote haya huku akitetemeka na kububujikwa na machozi!!
Kisha kwa mikono inayotetemeka, alibofya ‘19’ kisha akabofya ‘03’ na mwisho akamalizia ‘02’
Kabla ya kuruhusu muamala uendelee, alitazama kioo cha ile mashine ambacho sasa kilipambwa na alama ‘XXXXXX’ zikiwa zinaficha kile alichokiandika.
“Ilikuwa tarehe kumi na tisa, mwezi wa pili mwaka elfu mbili na mbili…siku hii hatutaisahau” alijikumbusha na kisha akafumba macho, akabofya kitufe cha kuruhusu muamala uendelee.
Wacha weee!! Joyce akaruka juu sana, kisha akageuka na kukutana na uso wa mama aliyeonekana kuwa alingoja muda mrefu, Joyce akajifanya hamuoni.
Huku mikono ikitetemeka akafanya utambuzi na kugundua kuwa Betty alikuwa na kiasi cha shilingi milioni mbili na laki nane katika hifadhi yake.
Joyce akaondoka huku akikiri kuwa ukimkabidhi Mungu matatizo yako anayatatua ilimradi tu ukiamini!! Hakika Mungu alikuwa amemwonyesha muujiza.
Alipofika nyumbani akaanza kujiuliza milioni tatu nyingine ataitoa wapi ili aweze ‘kumnunua’ Betty na kuendelea kuwa naye hai kuliko kukabidhiwa akiwa maiti.
Akiwa na matumaini kiasi aliamua kumpigia simu mtu ambaye alitarajia naweza kumsaidia.
Mwanzoni alimfikiria Isaya, lakini akaona kwa Isaya ni kujichoresha sana akimwomba ile pesa. Alijua tu Isaya ataamini kuwa anamtumia kwa sababu ana shida, Joy akauvaa umaskini jeuri na kuamua kupambana kivingine lakini moyoni akikiri kuwa yu katika wakati mgumu sana!!
*****
SIMU yake ya kiganjani iliita akiwa maeneo ya ‘River side’ akipata supu baada ya kunywa pombe sana usiku uliopita.
Ilikuwa ni simu ambayo aliitegemea sana kuwa itaingia wakati wowote. Alijua tu yatakuwa ni malalamiko mengine! Malalamiko na maswali ambayo hatakuwa tayari kutoa majibu.
“Niambie Kidoti” alisabahi Fonga kwa sauti ya kichovu.
“Hali si shwari ndugu yangu, nahitaji sana kuonana na wewe Fonga kabda unaweza kunisaidia.”
“Kwanza Betty una taarifa zozote juu yake?” Fonga alisaili badala ya kujibu hoja.
“Aaah….yaani sijajua lolote hadi sasa ndo maana nataka tuonane.” Joy akalikumbuka onyo la kutomshirikisha mtu yeyote juu ya jambo hilo.
“Tukutane ‘external’ hapo kama inawezekana. Baada ya saa moja.” Alitoa kauli hiyo huku akilamba ndimu na kukunja uso kwa ukakasi.
BAADA ya saa moja Fonga na Joyce walikuwa katika meza moja wakijadili jambo.
Joyce akajielezea kuwa alikuwa na shida ya shilingi milioni tatu upesi sana ili aweze kuhonga watu fulani wazito waweze kumsaidia katika hiyo kesi ya Betty kutoweka.
Fonga alimsikiliza kwa makini sana, kisha akamtazama katika jicho la huruma sana.
“Kidoti, kitu cha kwanza naomba unisamehe bure maana sijui hata ilikuwaje Betty akatekwa, maana vijana wangu walifika pale ulipotuelekeza na hawakumkuta Betty, sasa ninaduwaa ina maana Betty ana maadui ama wamemteka kwa sababu ya huyo mume wake? Inaumiza sana ujue. Sasa kwenye hiyo pesa dah! Joy mimi kama unionavyo ndo nilivyo, nikipata hamsini natia hapa nikipata kumi natia kinywani. Milioni tatu ndugu yangu….” Fonga alijieleza huku akitikisa kichwa.
Joy alikiri kimyakimya kuwa kweli Fonga hakuwa na uwezo walau wa kupata shilingi laki moja sembuse milioni tatu.
Hapa alikuwa amepotea njia!! Na kwa mtazamo tu akaamini kabisa hata uwezo wa kuteka mtu Fonga hana.
Akashangaa sana mbona Fonga alikuwa akisifiwa kiasi hicho kuwa ana mbinu za kimafia za kuvujisha siri, na kugundua ,mienendo ya watu kwa njia zake matata.
“Watu wanajua kusifia ujinga jamani!!!” alijisemea kichwani huku akimsaili Fonga!!
Fonga akainama chini kwa aibu kana kwamba anasikia kile kinachosemwa na Joyce Keto p.a.k Kidoti!!
Walipoagana Fonga akafanya kituko kingine cha kuruhusu mwaka uendelee, akampiga Joyce ‘kirungu’.
“Niachie hata buku mbili basi Kidoti.” Alisema huku akijilazimisha kutabasamu.
Joyce alikuwa amekereka lakini hakuwa na jinsi akatoa shilingi elfu tano akampatia!!
Wakati anaondoka akapokea ujumbe kuwa, mwalimu wa somo mojawapo katika kozi yake, aliingia na alitoa zoezi. Joy aliwekewa ziro.
Mwanzo wa kuidondosha roho moja!! Elimu!!
Akakuna kichwa na kukiri kuwa mshika tatu zote zitamponyoka!!!
Isaya, Betty na Elimu!!
Zote katika hatihati!!
Hali aliyoikuta kwa Fonga ilimfanya afikirie upya juu ya Isaya!!
Akafikiria kumwendea bwana huyo ili amlilie katika shida yake, nafsi ilimwingia baridi sana kwa jaribio alilotaka kulifanya lakini angefanya nini iwapo mambo yanamuwia magumu kiasi hicho!!
Akaishika simu yake aweze kumpigia Isaya!!
Alisita mara kadhaa, akaghairi na kuamua tena zaidi ya mara tatu. Kisha akabofya na kuanza kusikiliza upande wa pili.
Simu ikaita lakini haikupokelewa!!
Alipojaribu kupiga tena mara simu yake ikaanza kuita akajikuta anapokea upesi akidhani ni Isaya.
“Mambo bro Isaya!!” alisabahi..
“Kituo cha polisi Magomeni Usalama….Joyce Keto. Unahitaji kituoni haraka iwezekanavyo!! Fika upesi bila kukosa, Asante. Ukifika mapokezi utakuta maelezo.”
Simu ikakatwa!!
Ebwana eee!! Joyce alitamani kukimbia, akatamani apae juu na apotee kabisa. Miguu ilikuwa inatetemeka kupita kawaida, mara mkoba mdogo aliokuwanao ukaanguka chini. Akahaha huku na kule katika kuuokota mara pikipiki zikapiga honi.
Hofu hii ilikuwa kubwa zaidi, yaani anaitwa polisi? Kwa jinsi alivyokuwa anayaogopa mambo ya polisi leo hii anaitwa polisi haraka iwezekanavyo!! Weeee!
MSHIKEMSHIKE!!!
***JOYCE KIDOTI katika vita ya aina yake, vita inayoishinda akili yake. BETTY anauzwa, pesa hajapata, hatakiwi kutoa taarifa polisi. POLISI wamempigia simu ANAHITAJIKA MARA MOJA!!!! HARAKA IWEZEKANAVYOOOO!!
**MAONI YAKO, LIKES na SHARE kwa watu wengine!!!
ITAENDELEA KESHO!!
إرسال تعليق