SIKUMTEUA LOWASSA KIRAFIKI: KIKWETE

RAIS Jakaya Kikwete amesema hakumteua
Edward Lowassa kuwa Waziri Mkuu kwa
sababu ya urafiki wao bali kwa sababu
ya ufanisi wake.
Kikwete ameyasema hayo kupitia kitabu
chake cha JK: A Political Biography,
kitabu kinachoeleza kuhusu maisha yake
ambacho sasa kinapatikana hapa nchini.
Kikwete ameelezwa kutoa maelezo haya
mwaka mmoja baada ya tukio la kujiuzulu
kwa Lowassa kufuatia kashfa ya Richmond
ambayo ililazimu baraza lote la
mawaziri kuvunjwa.
“Sikiliza. Ni kweli kwamba Lowassa ni
rafiki yangu na nimemfahamu kwa muda
mrefu. Lakini pia ninawafahamu watu
wengi zaidi kwa muda mrefu, wanasiasa
na wasiokuwa wanasiasa na sikuwachagua
kuwa Waziri Mkuu.
“Nilikuwa natafuta mtu ambaye atafanya
kazi kwa ufanisi na kutekeleza sera
zangu. Lowassa alijitokeza vizuri kama
mtu anayeweza kutokana na uzoefu wake,”
kitabu hicho kinamnukuu Kikwete.
Hii ni mara ya kwanza ambapo Kikwete
anaeleza wazi wazi mahusiano yake
pamoja na tathmini ya utendaji wa
Lowassa, tangu kuibuka kwa kashfa ya
Richmond.
Sentensi moja katika maelezo ya Kikwete
inaonyesha mtazamo wake kwa waziri mkuu
huyo aliyejiuzulu; “Lowassa alikuwa
mmoja wa mawaziri wakuu wenye ufanisi
mkubwa kabisa nchini.”
Tafsiri ya maelezo haya ya Kikwete
inaonyesha kwamba mwaka mmoja baada ya
kashfa ya Richmond, rais bado alikuwa
na imani na Lowassa.
Wakati Kikwete alipochaguliwa kuwa rais
mwaka 2005, majina mengi yalitajwa
kuchukua nafasi ya uwaziri mkuu ingawa
la Lowassa lilitajwa zaidi kutokana na
ukaribu waliokuwa nao viongozi hao.
Lowassa pia hakuchukua fomu kuwania
urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka
2005, jambo lililotajwa kama kuonyesha
azma yake ya kumuunga mkono mgombea
huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya
kisiasa, walidai kwamba uamuzi wa
Kikwete kumteua Lowassa ungekuwa na
athari kubwa kwake kwa vile ukaribu
wake ungeweza kuingia kwenye kazi.
Mara baada ya uteuzi huo, ndipo
ilipoibuka dhana ya ‘serikali ya
kishkaji’ kutokana na baadhi ya watu
waliotajwa kuwa maswahiba wa Kikwete,
akiwamo Lowassa, kupata nafasi katika
baraza lake la kwanza la mawaziri.
Kikwete na Lowassa walikutana kwa mara
ya kwanza mwaka 1974 wakiwa wanafunzi
katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
wote wakiwa wanachama wa Umoja wa
Vijana wa chama cha TANU ingawa Jakaya
alikuwa katika mwaka wake wa mwisho wa
masomo huku Edward akiwa mwaka wa
kwanza.
Wote kwa pamoja walifanya maamuzi ya
kujiunga na ajira katika chama cha TANU
(sasa CCM) wakati huo mara baada ya
kumaliza masomo yao, na wote walichukua
fomu kuwania urais kupitia CCM mwaka
1995 wakiwa na umri chini ya miaka 50.
Source: Raia Mwema

Post a Comment

Previous Post Next Post