Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema
kikosi cha Taifa Stars sasa kina uwezo wa kushindana katika mashindano
yoyote, kwani tayari kimeiva.
Akizungumza
na wachezaji wa timu hiyo kambini kwao hoteli ya Tansoma, Dar es
Salaam, Rais Tenga aliwaambia kuwa kiwango walichoonesha kwenye mechi
zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast
kimethibitisha hilo.
“Kiwango
mlichoonyesha katika mechi hizo kila Mtanzania anayewafuatilia
amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa mtatuwakilisha vizuri kwenye mechi ya
kesho dhidi ya Uganda,” amesema Rais Tenga na kuwataka kupigana kwa
ajili ya Tanzania.
Taifa
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kesho (Julai 13 mwaka
huu) saa 9 kamili alasiri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itacheza na
Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania
tiketi ya kucheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika
Kusini.
Rais Tenga amesema TFF, mdhamini
Kilimanjaro Premium Lager, Kamati ya Ushindi na Watanzania kwa ujumla
wanawaunga mkono kwani wamekuwa wakiboresha kiwango chao kila
wanavyozidi kucheza mechi tangu wake chini ya Kocha Kim Poulsen, Mei
mwaka jana.
Wakati huo huo, Rais Tenga ameahidi
kumpatia tiketi ya kwenda Uganda kwenye mechi ya marudiano mshabiki
Wiseman Mwakyusa Luvanda anayetembea kwa miguu kutoka Mbeya kuja Dar es
Salaam kushuhudia mechi ya kesho.
“Kama ni kweli anakuja kwa kutembea, huyu
ameonyesha kiwango kikubwa cha uzalendo kwa timu ya Taifa, nitampatia
tiketi ya kwenda Kampala kuishangilia Taifa Stars kwenye mechi ya
marudiano,” amesema Rais Tenga.
…POULSEN, MICHO WATABIRI MECHI KALI
Makocha wa timu hizo Kim Poulsen wa Taifa
Stars na Sredojvic Micho wa The Cranes wamesema mechi ya kesho itakuwa
ngumu kwa vile kila mmoja amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo,
makocha wote waliezea ubora wa wapinzani wao, lakini wakasisitiza kuwa
wanaingia uwanjani kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika mazingira
mazuri kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa Kampala wiki mbili
zijazo.
Kim
alisema Uganda ndiyo inayoongoza kwa ubora wa viwango vya FIFA katika
ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni changamoto kwao ingawa
wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo.
Naye Micho aliyefuatana na nahodha wake
Hassan Wasswa alisema Taifa Stars imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe
chini ya Kim, na itakuwa na wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza
kinachocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia wakati kwa upande wake
atakuwa na wachezaji wawili tu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
إرسال تعليق