UFISADI WA KUTISHA KWA MGONGO WA ZIARA ZA MARAIS

Ufisadi ujio wa marais
*Hazina yatumia Shilingi bilioni 8
*‘Wajanja’ watafuna mamilioni
*Vifaa vya Obama vyaokoa jahazi
*Vinyago vyagharimu Sh milioni 30
*Sare, mikoba, vyagharimu mil. 400/-
*Karamu, chupa za kahawa, miavuli mil. 390/-
*Burudani ya muziki yatafuna milioni 195
Na Waandishi Wetu
Mkutano wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya
Wote (Smart Partnership Dialogue), uliomalizika hivi karibuni jijini Dar es
Salaam, umeigharimu Serikali Sh bilioni nane.
Hata hivyo, mamilioni ya fedha hizo yameishia mikononi mwa watumishi
kadhaa wa Serikali kupitia zabuni tata walizotoa kwa kampuni
mbalimbali.
Baadhi ya vifaa vilivyoorodheshwa kwenye zabuni hizo, ama
havikuwasilishwa, au viliwasilishwa shughuli ikiwa imeshamalizika, na
sasa vimetunzwa kwenye maghala. Miongoni mwa vifaa hivyo ni shehena
kubwa ya bendera za Tanzania ambazo zimetunzwa katika chumba ndani
ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Wahusika wakuu kwenye ulaji huu ni maofisa kadhaa wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa waliokuwa waratibu wa ugeni
huo. Katibu wa Bodi ya Zabuni katika Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Onesmo Suka, ni miongoni mwa maofisa
wanaokabiliwa na wakati mgumu kueleza mchanganuo wa zabuni
ulivyokwenda.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umeonyesha kuwa kiasi hicho cha
fedha cha Sh bilioni nane ni mbali kabisa na kile kilichokusanywa kutoka
kampuni na mashirika mbalimbali ya umma.
Imebainika kuwa hadi Juni 5, mwaka huu, fedha taslimu zilizokusanywa
ni Sh milioni 170 kutoka kampuni saba. Wachangaji wa kiasi hicho na
kiwango kikiwa kwenye mabano ni Kampuni ya Simu ya Tigo (Sh milioni
80), PPF (Sh milioni 20), PSPF (Sh milioni 20) na LAPF (Sh milioni 20).
Benki Kuu (BoT) ilitoa Sh milioni 10, Barrick Gold (Sh milioni 15) na Benki
ya Azania (Sh milioni 5).
Kampuni tatu zilikubali kutoa vifaa. Vodacom iliamua kuchangia masuala
ya ICT, Masasi Foods walitoa maji ya kunywa, ilhali Shirika la Hifadhi la
Taifa (TANAPA) lilitoa fulana na zawadi ndogo ndogo.
Hadi Juni 5, mwaka huu, kampuni tano zilikuwa zikisubiri uamuzi wa
Bodi. Kampuni hizo ni Mac Group, CBA Bank, PBZ Bank, Nokia-Siemens
na Shirika la Hifadhi la Taifa (NSSF).
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kampuni nne
zilishindwa kuchangia kwa kile kilichoelezwa kwamba ni uwezo wake
mdogo kifedha. Kampuni hizo ni TanzaniteOne inayochimba tanzanite
Mererani; IBM, Infrotech ba Diamond Trust Bank.
Wafanyabiashara nguli nchini hawakuachwa nyuma kwenye michango
hiyo, ingawa taarifa zinasema wapo waliokataa kutoa. Mwenyekiti wa
Kamati ya Uendeshaji wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa
Manufaa ya Wote, Balozi Ombeni Sefue, aliagiza wafanyabiashara kama
Said Bakhresa na Mohamed Dewji wafuatiliwe kwa karibu ili waweze
kutoa michango.
Hata hivyo, aliyekuwa Mkuu wa Sekretarieti ya Smart Partnership
Dialogue, Victoria Mwakasege, anasema kwamba baadhi ya
wafanyabiashara, wakiwamo kina Dewji, hawakuchangia. Hakutoa sababu
za kushindwa kwao.
Sokomoko la matumizi mabaya ya fedha
Uchunguzi umethibitisha kwamba Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa
Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote,
hakuridhishwa kabisa na namna zabuni zilivyotolewa.
Kwenye kikao cha mwisho, Sefue, kwa maandishi, alisema ingawa yeye
ameshiriki katika Kamati ya Uendeshaji, hakubaliani na bajeti pamoja na
mchanganuo wa zabuni ulivyokosa uwazi.
Sefue amenukuliwa akisema ni jambo gumu kwake kukubaliana na
ununuzi huo kwa vile hapakuwapo mchanganuo wa kuthibitisha namna
mamilioni ya fedha yalivyotengwa kuwalipa wazabuni na bei za vifaa
vilivyohitajika.
Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya kikao kilichofanyika Juni 17, vinasema
Balozi Sefue, aliweka wazi msimamo wake baada ya kuona taratibu za
ununuzi zikiwa zimekiukwa, na kwamba baadhi ya vitu
vilivyoorodheshwa, vilikuwa ni “vichekesho”.
“Mimi sitaki nihusishwe na jambo hili, waliolifanya wanapaswa wenyewe
wabebe msalaba huu, mchanganuo uletwe ili kuonyesha nini
kinanunuliwa kwa kiasi gani badala ya utaratibu huu wa kuorodhesha
vitu na kuweka gharama,” alinukuliwa aking’aka Balozi Sefue.
Kampuni zilizopata zabuni
Mmoja wa maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa wamesema wazi kwamba fununu za kufanyika kwa mkutano wa
Smart Partnership zilipoenea, watu wengi walipigana vikumbo wakitaka
wapewe zabuni.
Kampuni ya Luma International Ltd ilipewa zabuni ya kusambaza vitu
mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 391.1 Baadhi ya vitu hivyo ni
vipeperushi, bendera za Tanzania (kubwa na ndogo), suti kwa watu wa
protoko, sare kwa watu wa mapokezi, mabegi kwa wageni mashuhuri na
wageni wa kawaida, na beji.
Kampuni ya Softel Trading Company Limited ilipewa zabuni ya Sh milioni
392.6 kusambaza picha za mapambo ukumbini, miavuli (1,500), chupa za
kahawa (800), vikombe vya kahawa (800), kalamu za zawadi (2,000) na
vishikio vya funguo (800).
Kampuni hiyo hiyo ilipewa zabuni nyingine ya Sh milioni 48.25 kwa ajili
ya kufanya kazi za usanifu kwa kutumia kompyuta na uchapaji wa
mabango madogo madogo.
Kana kwamba haitoshi, kampuni hiyo hiyo ya Softel Trading Company Ltd
ilipewa zabuni ya thamani ya Sh milioni 254 kwa ajili ya kutengeneza
mabango makubwa 40. Wakati mkutano ukiwa unafanyika Dar es Salaam,
iliamuriwa kwamba mabango hayo yasambazwe katika mikoa ya Dar es
Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Zanzibar.
Kampuni ya Wild Cat Publishing ilishinda zabuni ya Sh 278,409,409,269
kwa ajili ya kuandaa machapisho 1,000 ya mkutano. Yalitakiwa yahusu
masuala ya kiasiasa, kiuchumi, fedha, teknolojia, mawasiliano,
usafirishaji, kilimo, ujenzi, afya na elimu, utalii, n.k.
Kampuni ya tano iliyoshinda zabuni ni ya Big Mama’s Woodworks
ambayo ilipangiwa Sh milioni 29.96 kwa ajili ya kutengeneza zawadi za
vinyago 60 yenye urefu wa sentimita 15 na upana wa sentimita 12 kila
kimoja. Pia ilitakiwa itengeneze vinyango vinne vyanye urefu wa
sentimita 150 na upana wa sentimita 35.
Kwenye masuala ya burudani, kampuni ya Prime Time Promotion
ilijipatia zabuni ya Sh milioni 194.7.
Kwenye orodha ya ugawaji zabuni, kampuni ya True Colour
Entertainment Group ilizawadiwa zabuni ya Sh milioni 50 kwa ajili ya
kuandaa na kuonyesha jarida. Ingawa haikufafanuliwa, hii yawezekana
ndilo lile jarida lililoonyeshwa kwenye Ukumbi Kimataifa wa Mikutano wa
Mwalimu Nyerere, siku ya ufunguzi wa Mkutano wa Smart Partnership.
Lilihusu wanyamapori na vivutio kadhaa vya utalii vinavyopatikana hapa
nchini.
Zabuni ya nane ilitolewa kwa kampuni ya Simply Computers (T) Ltd.
Iligharimu Sh milioni 187.478. Ilitakiwa kusambaza kompyuta kubwa
mbili, idadi kama hiyo kwa kompyuta za ukubwa wa kati na projekta nne.
Kampuni hiyo hiyo ya Simply ilipata zabuni nyingine yenye thamani ya
Sh milioni 210.198 kwa ajili ya kusambaza kompyuta tano za mezani,
laptop (5), laptop za sekretarieti na mkutano (14), mobile computing
equipment (14), black and white printer (2), colored printer (2),
kompyuta za mezani (nyingine 5), colored printer (nyingine 2) na flash
disk (32).
Upungufu uliojitokeza
Pamoja na mamilioni hayo kupitishwa kwa ajili ya mkutano huo lakini
bado kulikuwa na upungufu mkubwa katika utendaji hususani katika
utoaji wa vitambulisho.vitabulisho wa
JAMHURI lilishuhudia baadhi ya wageni wakiwemo mabalozi kutoka katika
mbalimbali Askari wa Jeshi la Polisi usalam wa taifa madereva wa Idara
mbalimbalia za Serikali wakiendelea kusota kwa ajili ya kupata
vitambulisho hivyo .
Kadhia hiyo pia ilimpata Katibu Mkuu Kiongozi, Sefue ambaye alifika
katika Ukumbi wa Kalimjee saa nne asubuhi ambapo wafanyakazi wa
waliokuwa wakihusika na utoaji wa vitambulisho hawakumjali jambo
ambalo liliwasahangaza wengi waliokuwepo hapo.
Wengi wao walihoji uelewa wa wahudumu hao katika utendaji wao na
kama kweli walikuwa hawamjui kiongozi huyo au ilikuwa ni dharau.
Sefue alikaa katika eneo hilo kwa zaidi ya nusu saa na kuondoka katika
ukumbi huo huku akiwa hana kitambulisho hadi anaingia ukumbini wa
Kimataifa wa Walimu Nyerere. Saa kumi jioni.
Wengine waliofika katika ukumbi huo na kupata kadhia hiyo ni Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana na
mwenzake ambaye JAMHURI hailikufanikiwa kupata jina lake
Dk. Bana na mwenzake walifika na kujitambulisha kwa mmoja wahudumu
katika ukumbi huo lakini mhudumu huyo baada ya kutekeleza shida yao,
alianza kueleza matatizo yaliyoikumba idara hiyo ya vitambulisho.
“Jamani idara hii ina matatizo kwani hatukuwa tumejipanga kila mtu
yuko kivyake ndio maana mnaona huduma imesimama kama mnavyoona
hakuna majina hapa, mafaili yako tupu na wahusika hawapo
kinachotakiwa ni kufika hapa na kuhakikisha jina lako na pia unakwenda
kupiga picha pale lakini hadi sasa hatujapata majina je nyinyi
mlijiandisha,” anasema mhudumu huyo.
Hata hivyo kauli hiyo ilimuudhi, Dk. Bana na mwenzake hivyo alimtaka
mhudumu huo kutozungumza upungufu wa idara hiyo mbele ya wageni
waliofika katika ukumbi huo, kwani kufanya hivyo ni aibu na haukuwa
wakati wake kinachotakiwa kutoa vitambulisho.
Mhudumu huyo ambaye JAMHURI halikufanikiwa kupata jina leke
alionekana kukerwa kauli hiyo aliendelea kuzumgumzia upungufu huo
pamoja na Dk. Bana mwenzake kunyamaza. Waliondoka katika eneo hilo
kwa miadi ya kurudi baadae.
Viongozi ‘warushiana mpira’
Utata kuhusu uhalali wa fedha zilizotumika kununua vitu hivyo, usiri
kwenye utoaji zabuni na upungufu mkubwa uliojitokeza kwenye shughuli
nzima ya mkutano huo, ni mambo yanayowasumbua sasa viongozi
serikalini.
Wakati Katibu Mkuu Kiongozi akijitoa kwenye sakata hilo na kumsukumia
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
John Haule; Haule anasema yeye hahusiki. Badala yake anasema
anayepaswa kuulizwa mambo yote yalivyokwenda ni Mkuu wa Sekretarieti
ya Smart Partnership Dialogue, Mwakasege.
Kwa upande wake, Mwakasege anaruka kwa kusema Sekretarieti ambayo
yeye alikuwa Katibu haikuhusika kwa namna yoyote na masuala ya
zabuni. Akasisitiza kwa kusema, “Huyo anasema uniulize mimi (Haule),
mwulize yeye. Mimi nilihusika na logistic, sisi tulipeleka mahitaji,
kwenye zabuni hatukuhusika kabisa. Kilichofanyika ni sisi kukabidhiwa
vitu kulingana na mahitaji. Yeye ndiye mwenye masurufu, ndiye
anayejua hesabu zote za wizara.”
CHANZO: Gazeti JAMHURI

Post a Comment

Previous Post Next Post