WAKE wa
viongozi Jumuiya ya Uamsho Zanzibar, wameiomba serikali kuitazama kesi
inayowakabili viongozi hao kwa jicho la uadilifu, haki na sheria ili
kuonesha dhana ya utawala bora.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika kongamano la wanawake wa
Kiislamu lililofanyika jana msikiti wa Mbuyuni, kinamama hao
wamelalamikia kesi hiyo kuchukua muda mrefu huku ikiwa hakuna hatua
yoyote muhimu inayochukuliwa ili haki itendeke.
Wametaka vyombo vya sheria vifanye kazi kwa maadili, hasa
ikizingatiwa kwamba Zanzibar ni mshiriki wa Muungano wa Tanzania ambayo
ni mwanachama wa taasisi mbalimbali za kulinda na kuheshimu haki za
binadamu ulimwenguni.
“Hatukusudii kuingilia kazi za mahakama, bali tunaeleza hali halisi
ya uvunjwaji wa sheria na katiba ya nchi kwa vyombo vya sheria kufanya
kazi kwa utashi bila ya kuzingatia haki za wanachi mbele ya
sheria”,walidai wanawake hao.
Walidai kuwa, kitendo cha kunyima haki kinaweza kuitia doa kubwa mahakama na serikali mbele ya macho ya kimataifa.
Aidha, walitaja sababu za kuwekwa ndani waume zao kuwa ni harakati za
kuongoza umma wa Wazanzibari kudai haki yao ya msingi juu ya hatima ya
Zanzibar kuwa nchi yenye uhuru wa kujiamulia mambo yake.
Wameeleza kusikitishwa kwao kwa kusema kuwekwa ndani kwa waangalizi
hao wa familia zao, kumewaathiri sana kisaikolojia na kiuchumi.
Pia wamesema mwenendo mzima wa taaluma za Kiislamu ambazo viongozi
hao walikuwa wakifundisha katika madarsa mbalimbali kwenye misikiti na
vyuo, umeathiriwa na kushikiliwa kwa viongozi hao.
Kwa hivyo wamevitaka vyombo vya sheria kufanya haki katika maamuzi
yao ili kudumisha amani na utulivu uliopo pasi na kutia dosari serikali
ya umoja wa kitaifa iliyowalea Wazanzibari pamoja.
Kupitia kongamano hilo, wanawake hao wameviomba vyombo vya
sheria,kuwaruhusu viongozi hao kuonana na wake na ndugu zao wakati
wanapofikishwa mahakamani kwa kusikilizwa kesi yao.
Katika hatua nyengine, kinamama hao wameunda kamati ya kufuatilia na
kuratibu mwenendo wa kesi pamoja na kuonana na watendaji wa haki za
binadamu.
Chanzo: Habari maelezo – Zanzibar
إرسال تعليق