Harakati ya
Ikhwaanul Muslimiin ya Misri imetangaza kuwa, kwa akali watu 480
wameuawa, 8,000 kujeruhiwa na wengine 1,500 kutiwa mbaroni kwenye ghasia
na machafuko yaliyodumu kwa wiki tatu nchini humo. Chama cha Uadilifu
na Uhuru, tawi la kisiasa la Ikhwaanul Muslimiin, kimeeleza kuwa katika
kipindi cha wiki tatu zilizopita, watu wasiopungua mia nne na themanini
wameuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa pamoja na kufungwa kanali tisa
za televisheni za harakati hiyo. Taarifa zinasema kuwa, machafuko na
mapigano nchini humo yamesababishwa na hatua ya jeshi ya kumuondoa
madarakani na kumuweka kizuizini Rais Mohammad Morsi wa nchi hiyo.
Wafuasi wa Morsi wamekuwa wakijitokeza barabarani kila siku kumuunga
mkono kiongozi huyo na hivyo kukabiliwa na hatua kali za jeshi.
Waziri wa Lebanon: Hizbullah ni chama cha kisiasa
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Lebanon amesema kuwa, chama cha Hizbullah
ni harakati ya kisiasa inayotambuliwa rasmi nchini Lebanon. Marwan
Sharbil amesisitiza kuwa, Hizbulah ni chama cha kisiasa na kina wabunge
na mawaziri kwenye serikali ya Lebanon. Waziri wa Mambo ya Ndani wa
Lebanon ameelezea kushtushwa kwake na maamuzi ya hivi karibuni ya Umoja
wa Ulaya ya kulijumuisha tawi la kijeshi la Hizbulah kwenye orodha ya
makundi ya kigaidi na kusisitiza kuwa, Hizbullah ni harakati ya muqawama
na kwamba madai yanayotolewa dhidi ya harakati hiyo hayana ukweli
wowote. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Lebanon amesema kuwa, njama za nchi
za Ulaya za kulijumuisha tawi la kijeshi la harakati hiyo kwenye orodha
ya makundi ya kigaidi ni kutaka kudhoofisha mapambano yake ya muqawama
dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Post a Comment