AZAM FC YAIFUMUA 1-0 BARAZANI KWAKE MAMELODI SUNDWONS

Gaudence Mwaikimba akishangilia baada ya kufunga leo. Kushoto ni Seif Abdallah.

BAO pekee la Gaudence Exavery Mwaikimba jioni ya leo, limeipa ushindi wa 1-0 Azam FC ya Dar es Salaam katika mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji Mamelodi Sundwons kwenye Uwanja wa mazoezi wa timu hiyo, uliopo Chloorkop, Johannesrbug mjini hapa.   
Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa Azam FC katika ziara yao ya nchini hapa kujiandaa na msimu baada ya juzi kufungwa mabao 3-0 na Kaizer Chiefs.
Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na wenyeji ndiyo waliotawala zaidi mchezo kipindi hicho, ingawa Azam walifanikiwa kutengeneza nafasi nzuri zaidi ya kufunga.
Khamis Mcha ‘Vialli’ aliingia vizuri ndani kutokea pembeni kushoto hadi ndani ya eneo la hatari na akampa pasi ya ‘hapa kwa hapa’ John Bocco ‘Adebayor’ akiwa anatazamana na lango, lakini akapiga juu ya lango dakika ya 43.   
Kipindi cha pili Azam waliingia kwa ari mpya na kufanikiwa kuuteka mchezo hali ambayo ilisababisha wafanye mashambulizi mengi langoni mwa Mamemlodi.
Almanusra Bocco afunge dakika ya 65 kama si kichwa chake kupaa juu ya lango kufuatia krosi maridadi ya Kipre Herman Tchetche.
Mamelodi walijibu shambulizi hilo dakika ya 70 na shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 19 lililopigwa na Jabu Shongwe liligonga nguzo ya juu ya lango na kurejea uwanjani kabla ya Said Morad ‘Mweda’ kuondosha kwenye hatari. 
Katika dakika ya 74, Mwaikimba aliyeingia uwanjani dakika ya 64 kumpokea Bocco aliunganisha vizuri kwa kichwa krosi ya beki Joackins Atudo kutoka wingi ya kulia, ambaye pia alitokea benchi kipindi cha pili kuipatia Azam bao pekee kwenye mchezo wa leo.
Dakika ya 89 Mwaikimba alikaribia tena kufunga kama si shuti lake kupaa juu ya lango akiwa ndani ya eneo la hatari kufuatia krosi nzuri ya Tchetche.
Baada ya mchezo huo, kocha wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall alifurahia matokeo na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake na pia akasifu ushindani ulioonyeshwa na wapinzani. 
Kwa wake, Pitso Masomane kocha wa Mamelodi alisifu Azam na akasema kwa soka waliyoonyesha hastaajabu kwa nini wameshika nafasi ya pili katika Ligi Kuu.  Katika mchezo huo, kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni/Joackins Atudo dk 46, Waziri Salum/Samih Hajji Nuhu dk 80, Said Morad/David Mwantika dk77, Aggrey Morris, Jabir Azzi/Kipre Balou dk50, Himid Mao/Ibrahim Mwaipopo dk55, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Mudathir Yahya dk75, John Bocco/Gaudence Mwaikimbadk65, Kipre Tchetche na Khamis Mcha/Seif Abdallah dk85.
Sundown; Wayne Shandialands/Glenn dk78, Ramahlwe Mphanhlele, Punch Masenamela, Rashid Sumaila, Emanuel Mathias, Thami Sangweni/Sibusiso Khumalo dk51, Jabu Shongwe/Raymond Monama dk62, Mzikayise Mashaba, Richard Hanyekane, Elias Pelembe dk73, Surprise Moriri/Mphela Katlego dk79 na Katlego Mashego.

Post a Comment

Previous Post Next Post