BARAZA LA USHINDANI (FAIR COMPETITION TRIBUNAL – FCT)
MADA
KUHUSU BARAZA LA USHINDANI ILIYOWASILISHWA KWA WAANDISHI WA HABARI
TAREHE 6 AGOSTI 2013, KATIKA UKUMBI WA HABARI MAELEZO, DAR ES SALAAM
Utangulizi
Ndugu
Waandishi wa Habari, mada yetu inahusu Baraza la Ushindani. Katika mada
hii tunatarajia kuliezea Baraza la Ushindani kuwa ni chombo cha namna
gani, majukumu yake na uwezo wake kisheria. Hivyo,
ili kuweza kuwapa maelezo yatakayoweza kuwasidia kuandika makala zenu
vizuri mada hii imejengwa katika sehemu tatu kuu kama ifuatavyo:
- Chimbuko la Baraza la Ushindani;
- Baraza la Ushindani ni nini
- Majukumu na Uwezo wa Baraza.
Chimbuko la Baraza la Ushindani
Bila shaka mtakumbuka kwamba katika jitihada za kuboresha na kuimarisha uchumi mwaka 1986,
Serikali ya Tanzania iliamua kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa uchumi
kutoka kwenye mfumo wa uchumi hodhi (planned economy) na kufuata mfumo
wa uchumi wa soko (Market Economy). Kwa kifupi katika Mfumo wa
uendeshaji wa uchumi hodhi maamuzi yote makubwa yanayohusisha uendeshaji
wa uchumi hufanywa na Serikali, wakati katika mfumo wa uchumi wa soko,
maamuzi yote makubwa hufanywa kwa kutegemea mwelekeo na nguvu ya soko. Aidha,
mfumo wa uchumi wa soko unashirikisha kwa kiasi kikubwa sekta binafsi.
Katika mfumo huu huduma na bidhaa sokoni hutolewa na kuuzwa kwa
ushindani. Uzoefu duniani umeonesha kuwa bila kuwa na usimamizi mzuri wa
ushindani sokoni migongano na mivutano ya kimasilahi hutokea na
kusababisha kutofikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuanzishwa mfumo wa
uchumi wa soko.
Kwa
hiyo ili kupata matunda yaliyokusudiwa kutoka kwenye mfumo wa uchumi wa
soko, Serikali iliazimia kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa ushindani
sokoni pamoja na udhibiti kwenye sekta za miundombinu, huduma za maji,
nishati na mawasiliano. Utekelezaji wa azma hiyo ya Serikali ukasababisha kuanzishwa kwa vyombo vya udhibiti katika sekta hizo. Vyombo hivyo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA),
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA), na Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Aidha,
Serikali kupitia Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 iliunda vyombo
vitatu muhimu ambavyo ni Tume ya Ushindani (FCC), Baraza la Ushindani
(FCT) na Baraza la Taifa la Utetezi wa Mlaji (NCAC). Nia
ya uanzishaji wa vyombo hivi vyote ni kusimamia biashara zizifanyike
kiholela, kuhakikisha panakuwepo na ustawi wa mlaji na pia kuona kwamba
kunakuwa na ufanisi katika utumiaji wa rasilimali zilizopo, soko na
uchumi kwa ujumla. Kwa hiyo Baraza la Ushindani ni chombo kimojawapo kilichoanzishwa kufuatia mabadiliko hayo ya kichumi.
Baraza la Ushindani ni nini na madhumuni yake ni nini
Baraza
la Ushindani au kwa lugha ya Kiingereza “Fair Competition Tribunal” na
kwa kifupi “FCT” ni chombo huru cha kimahakama kilichoanzishwa na
Serikali chini ya Sheria ya Ushindani Namba 8 ya mwaka 2003 (Fair
Competition Act, No. 8/2003). Madhumuni ya kuanzishwa Baraza hili ni
kuwa chombo maalumu cha kimahakama kitakachopokea, kusikiliza na kuamua
kwa haraka rufaa zitokanazo na maamuzi au amri za Tume ya Ushindani na
Mamlaka nne za udhibiti kwenye sekta za miundombinu na matumizi ya
mawasiliano zilizotajwa kwenye aya zilizotangulia.
Majukumu na Uwezo wa Baraza
Jukumu
kuu la Baraza la Ushindani ni kupokea, kusikiliza na kuamua kesi za
rufaa zinazotokana na maamuzi ya Tume ya Ushindani (Fair Competition
Commission – FCC) pamoja na mamlaka za udhibiti zifuatazo:
- Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA);
- Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri na Usalama wa Anga (TCAA);
- Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA); na
- Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano na Utangazaji (TCRA).
Uwezo wa Baraza la
Ushindani umeainishwa kwenye Sheria ya Ushindani Na 8 ya mwaka 2003
pamoja na Kanuni za Baraza (The Fair Competition Tribunal Rules 2012)
Tangazo la Serikali Na. 2019 la tarehe 22 Juni 2012.
Katika kutekeleza majukumu yake, Baraza la Ushindani linaweza kufanya, kwenye shauri la rufaa, lolote kati ya haya yafuatayo:-
1. Kuthibitisha, kugeuza au kubadilisha uamuzi wa Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika;
2. Kurejesha shauri kwenye Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika pamoja na maelekezo litakayoona yanafaa kutolewa;
3. Kuamuru Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika kuendesha shauri upya; na
4. Kutoa amri yoyote muhimu kufuatia uamuzi wake.
Kimsingi,
kila mtu anaruhusiwa kuleta maombi ya rufaa kwenye Baraza la Ushindani,
hii ni awe mtu binafsi ama ni kampuni ya Biashara au taasisi. Hata hivyo kwa kuwa Baraza la ushindani ni Mamlaka ya
Rufaa, kama ilivyo katika Mahakama za kawaida, ili mtu binafsi, Kampuni
au Taasisi yoyote iweze kuleta maombi ya rufaa kwenye Baraza la
ushindani, ni lazima mtu, Kampuni au Taasisi hiyo iwe ni mdaawa (Party)
katika mgogoro uliozaa uamuzi unaoombewa rufaa. Lakini pia mtu, Kampuni
au Taasisi inaweza kuomba kuunganishwa kwenye rufaa kama muathirika wa
uamuzi unaoombewa rufaa hata kama haikuwa mdaa katika shauri hilo.
Hivyo ndugu waandishi wa Habari kwa kifupi tumeweza kuona kuwa Baraza
la Ushindani ni chombo cha kimahakama kilichoanzishwa na Serikali chini
ya Sheria ya Ushindani Namba 8 ya mwaka 2003 kuwa chombo maalumu cha
Rufaa kitakachopokea, kusikiliza na kuamua rufaa zitokanazo na maamuzi
au amri za Tume ya Ushindani na Mamlaka nne za udhibiti kwenye sekta za
miundombinu na matumizi ya mawasiliano zilizotajwa. Chimbuko
la kuanzishwa Baraza la Ushindani ni mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji
wa uchumi, pia tumeeleza kuhusu majukumu ya Baraza na kwamba katika
kutekeleza majukumu yake, Baraza linaweza kuthibitisha, kugeuza au
kubadilisha uamuzi wa Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika;
Kurejesha shauri kwenye Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika
pamoja na maelekezo litakayoona yanafaa kutolewa; Kuamuru Tume ya
Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika kuendesha shauri upya; na Kutoa
amri yoyote muhimu kufuatia uamuzi wake.
Aidha kimsingi, mtu anayeleta maombi
ya rufaa kwenye Baraza la Ushindani anahitaji kufuata taratibu kama
zilivyoainishwa katika Kanuni (Rules) za Baraza zilizotajwa hapo juu.
Nzinyangwa E. Mchany
MKUU WA KITENGO CHA MASUALA YA UCHUMI
Simu 0754 720007


إرسال تعليق