
Katibu
wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa
habari, katika Ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya
CCM, Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam. (Picha na Bashir Nkoromo).
Na. Mwandishi wetu
CHAMA
CHA MAPINDUZI (CCM) kimesema bado kina imani na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba nchini, katika mchakato unaoendelea wa kupata katiba mpya.
Imesema
licha ya CCM kutofautiana kimawazo katika baadhi ya maeneo katika
rasimu ya kwanza ya katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
lakini haina ugomvi na tume hiyo.
Hayo
yamesemwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Sekretarieti, Ofisi
Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam.
”Tunawaheshimu
sana wajumbe wa tume hii, na kwa kweli tunamatumaini nao sana kuwa
watatimiza wajibu wao kwa weledi mkubwa”, alisema Nape.
Nape
alibainisha kwamba pamoja na maeneo mengine ya rasimu ya kwanza ya
katiba , CCM ina mawazo tofauti kwenye suala la Muundo wa Muungano
ambapo wakati rasimu inapendekeza muundo wa serikali tatu, CCM yenyewe
inapendekeza serikali mbili.
“Kama
mnavyoona katika hili, wakati tume inapendekeza muundo wa serikali tatu
sisi CCM tunapendekeza muundo wa serikali mbili, lakini hii haitufanyi
tuwapuuze au tugombane na wale wenye mawazo tofauti na yetu”, alisema
Nape na kuongeza;
“Kumekuwepo
na ripoti na makala kadhaa zinazojaribu kuonyesha kama vile kuna
mvutano kati ya tume na CCM, au CCM na wengine wenye mawazo tofauti na
CCM. Ukweli ni kuwa hali hiyo inayojaribu kujengwa kwa nguvu si ya
kweli. Tuache hoja zishindane kwa hoja na nguvu ya hoja ndio iwe msingi
wa ushindani”.
Nape alitaka ushindani uwe kwenye hoja bila kushutumiana ili jatimaye mawazo ya wengi yasikilizwe na kuzingatiwa.
Alisema,
CCM inasisitiza kuwa itaheshimu mawazo ya Watanzania, kwani katiba
inayotengenezwa ni ya watanzania wote bila ya kujali itikadi zao.
“Naomba
nichukue nafasi hii kuwashukuru wale wote wanaounga mkono baadhi ya
hoja za CCM hasa hoja ya serikali mbili. Tumeshuhudia maoni ya wajumbe
wengi wa mabaraza na wananchi kwa ujumla wakiunga mkono mawazo haya ya
CCM ya muundo wa muungano wa serikali mbili na hoja kadhaa zingine”,
alisema Nape na kuongeza;
“CCM tunapenda kuwashukuru wote. Tujadili kwa kuvumiliana, tukipendana na kuheshimiana. Tanzania yenye neema tele inawezekana”.
إرسال تعليق