
Wakati matukio ya baadhi ya vigogo na wasanii maarufu wanaotuhumiwa
kujihusisha na biashara ya dawa za kulenya hayajapoa, imebainika kuwa
mtambo maalumu wa kuchanganya na kuziongezea thamani dawa hizo upo hapa
nchini.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa mtambo huo ambao awali
ulikuwa unapatikana Mombasa, Kenya, pekee, unatumika kuchanganya dawa za
kulevya na kemikali nyingine ambapo nusu kilo ya heroine huongezwa hadi
kufikia kilo mbili.
Uchunguzi unaonyesha kuwa kuwa mtambo huo ulioingizwa mwaka huu na
kigogo mmoja wa dawa hizo, upo katika nyumba moja iliyopo eneo la Mbezi
Beach.
Mmoja wa watumiaji wa dawa hizo ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa
kuhofia usalama wake, alisema mtambo huo umerahisisha upatikanaji wa
heroine nchini maarufu ‘white sugar’ kama inavyojulikana mitaani.
“Zamani ‘white sugar’ ikitoka shamba (nchi inakotengenezwa yaani
Pakistan na nchi nyingine) ilikuwa inapelekwa Mombasa, Kenya, ambako
kuna mtambo wa kuchanganya na dawa nyingine ili iongezeke wingi wake,
lakini kazi hiyo inafanyika hapa hapa nchini kwa sasa,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu uwepo wa mtambo huo hapa nchini, Mkuu wa Kitengo cha
Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema kuwa kuna taarifa
alizonazo ambazo bado anazifanyia kazi.
“Hata kama nikiwa nazo nazifanyia kazi, za kwangu mimi nazifanyia kazi na hata za kwako nazifanyia kazi,” alisema Nzowa.
Hata hivyo, Nzowa akizungumza katika kipindi cha Malumbano ya Hoja
kilichorushwa na Televisheni ya ITV juzi, alisema kuwa katika siku za
hivi karibuni wafanyabiashara wa heroine wamekuwa wakiingiza nchini
malighafi za dawa hizo, tofauti na awali ambapo walikuwa wakiingiza dawa
hizo zikiwa tayari kwa matumizi.
Akitoa mfano alisema kuna raia wa kigeni alikamatwa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, akiwa na malighafi
hizo zilizokuwa zikifanana na sukari na kwamba Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA) na Mkemia Mkuu wa Serikali, ndiyo waliobaini kuwa haikuwa
sukari kama ilivyodhaniwa.
Alisema kutokana na uhaba wa dawa hizo bei ya kete imepanda ambapo hivi
sasa hakuna kete ya gramu 0.11 inayouzwa chini ya Sh 3,000.
Hii ni mara ya pili kubainika kuwepo kwa mtambo wa kutengenezea dawa za
kulevya nchini. Miaka ya hivi karibuni jeshi la polisi lilikamata mtambo
wa kutengenezea dawa za kulevya katika nyumba moja iliyopo eneo la
Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa mbali ya kuwepo mtambo huo kuna
nyumba tano katika eneo la Tandika jijini Dar es Salaam karibu na soko,
ambazo zinatumika kuuza dawa za kulevya huku baadhi ya polisi wa Mkoa wa
Kipolisi wa Temeke, wakiwalinda wauzaji wake kwa kuwapa taarifa ya
mipango inayopangwa na jeshi la kuwatia mbaroni.
Alisema kuna wakati askari huonekana wakirandaranda katika mitaa hiyo,
kitu kinachowafanya wakazi wa maeneo hayo kuamini kuwa wamefika
kukamata, lakini badala yake huishia kuingia katika nyumba hizo kuchukua
hongo na kutoka.
“Hata askari wenyewe wakija kukagua hubaki wakishangaa na kushindwa
kuamini kama kweli nyumba waliyoambiwa inauza unga ndiyo hiyo
waliyoikagua. Ndiyo ‘madili’ hayo watu wanavyoishi mjini hapa,” alisema.
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Temeke, Engelbert
Kiondo alisema hawezi kusema ndiyo au hapana kwa kuwa jambo hilo
linahusisha vitendo vya rushwa.
“Kuhusu askari kuwalinda wahalifu siwezi kusema ndiyo au hapana kwa
sababu hili ni suala la rushwa,” alisema Kiondo na kuongeza kuwa:
“Lakini kuhusu kuwakamata vijana wanaojihusisha na dawa za kulevya hao
tunawakamata kila siku, wengi wameshafikishwa mahakamani kesi zao zipo
katika hatua tofauti.”
Kwa upande wake Nzowa, alisema kwamba Jumatano wiki hii walifanikiwa
kuwakamata watu watatu wakijihusisha na dawa hizo, akiwamo mwanafunzi wa
kike na kwamba wote walifikishwa mahakamani.
Taarifa zaidi ziliendelea kueleza kuwa dawa aina ya heroin au ‘white
sugar’ ndiyo inayopatikana kwa wingi nchini huku ikifuatiwa na ‘cleck’
inayojulikana mitaani kama ‘pele’ kwa kuwa inatoka nchini Brazil.
“Bei ya unga hutegemea aina na kiwango mteja anachokihitaji kwani kipo
kipimo cha Sh 1,000 na Sh 2,000 huku kipimo maarufu kama pointi kikiuzwa
kati ya Sh3,000 na Sh3,500. Lakini pele huuzwa bei kubwa zaidi, kwani
ukubwa wa punje ya mtama tunanunua kwa Sh10, 000,” alifafanua.
-Mwananchi
إرسال تعليق