Na Othman Khamis Ame, OMPR
Uongozi wa Benki ya
NMB una wajibu wa kufanya utafiti wa kina katika muelekeo wa kuongeza
Matawi yake katika sehemu tofauti nchini wakilenga zaidi maeneo ya
Vijijini ili kuwapa fursa Wananachi walio wengi wa maeneo hayo kupata
huduma za kifedha.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo mara baada ya futari ya
pamoja iliyoandaliwa na Benki hiyo na kuhudhuriwa na watu mbali mbali
wakiwemo wateja wa benki hiyo futari ambayo ilifanyika katika Hoteli ya
Zanzibar Ocean View iliyopo Migombani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema
hivi sasa vipo Vijiji vingi vya kisasa ndani ya Visiwa vya Zanzibar
ambavyo vinahitaji kupatiwa huduma za Kibenki jambo ambalo endapo
watapatiwa Matawi ya Benki linaweza kuwaondoshea usumbufu wa msongamano
wanaoupata wakati wanapofuata huduma hizo Mjini.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar akivitolea mfano baadhi ya Vijiji hivyo kuwa ni pamoja na
Nungwi, Kiwengwa na ukanda wa Mkoa wa Kusini Unguja maeneo ambayo hivi
sasa yamesheheni Hoteli kadhaa ya Kitalii zinayohitaji huduma hizo.
Aliupongeza Uongozi na
Wafanyakazi wa Benki ya NMB kwa kusaidia huduma na kufanya kazi kubwa
ya kutatua kero za Jamii kitendo ambacho kimesababisha Benki hiyo
kupendwa na Wananchi kwa vile bado inaendelea kutoa huduma zaidi
vijijini.
Aliwaomba Wananchi
kujiunga na NMB kutokana na huduma inazotoa Benki hiyo katika kipindi
kifupi tokea kuanzishwa kwake na kufikia hatua ya kuungwa mkono hata na
Serikali kutokana na mfumo wake wa kufika katika maeneo ya Wananchi wa
kawaida.
“ NMB imekuwa mstari
wa mbele kusaidia vikalio katika Maskuli mbali mbali hapa Zanzibar.
Ukweli ni moja kati ya Benki zinazopendwa hapa Zanzibar. Hata ile mikopo
ya JK na AK iliyoandaliwa kuwafikiwa wananachi ili kupunguza umaskini
pia ilipitishwa katika Benki hiyo ya NMB “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar aliuomba Uongozi wa NMB kufanya kazi ya ziada katika
kuhakikisha misururu ya wateja wao hasa wale watumishi wa Serikali ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wanaochukulia mishahara yao katika
Benki hiyo inaondoka.
“ Unafikia hatua ya
kuwaonea huruma wateja wa Benki yenu hasa ndugu zetu wa JWTZ, Polisi na
Taasisi nyengine za Muungano wanaochukulia mishahara yao wanalazimika
kupanga misururu mirefu ya kusubiri mishahara yao na kujikuta wakipoteza
muda mrefu “. Akafafanua Balozi Seif.
Mapema Meneja wa Benki
ya NMB Abdulmajid Mussa Nsekela alisema katika kukabiliana na usumbufu
unaowapata wateja wao Uongozi wa Benki hiyo umejikita kuongeza Tawi
jengine la NMB Mwezi ujao katika eneo la Mwanakwerekwe pamoja na huduma
za ATM Tano katika Maeneo ya Vikosi ya Jeshini na Ziwani.
Abdumajid Mussa
alisema hatua hiyo imelenga kupunguza msongamano uliopo wa wateja wao
hatua ambayo pia itakwenda sambamba na huduma za kifedha kupitia
mitandao ya simu za mkononi mara baada ya kukamilika kwa mawasiliano
kati ya Uongozi wa Benki hiyo na Makampuni ya Simu.
Post a Comment