
Kutokana
na matukio ya upitishwaji wa dawa za kulevya kukithiri katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA), Jeshi la Polisi Kikosi cha
Viwanja vya ndege limesema kwa sasa linajipanga kukabiliana na matukio
hayo kwa kuweka na kufunga vitendea kazi vya kisasa.
Mpango huo umetangazwa na Kamanda wa kikosi hicho, Deusdedit Kato
wakati akizungumza na NIPASHE kuhusu mikakati ya jeshi hilo kupambana na
matukio ya upitishwaji kiholela wa dawa za kulevya.
Mpango huo ameutangaza siku chache tangu aueleze umma kwamba Polisi
inashindwa kunasa watuhumiwa wanaosafirisha dawa za kulevya wanaopitia
JNIA, kutokana na kukosekana kwa vitendea kazi vya kisasa.
Akihojiwa katika kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One
juu kwanini JNIA umeonekana kuwa kitovu cha kupitisha dawa za kulevya,
Kato alisema sababu kubwa ni kwamba kuna tofauti kati ya nchi na nchi
katika masuala ya teknolojia katika kubaini dawa za kulevya.
Alisema nchi nyingine zina vifaa vya kisasa zaidi na kwamba wakati sasa
umefika kwa serikali kuwekeza katika kupata vitendea kazi zaidi ili
kufanikisha mapambano ya dawa za kulevya.
Alisema katika kipindi cha miezi sita hadi nane, watu 14 wamekamatwa wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya nchini
Alisema tatizo la upitishwaji wa dawa za kulevya katika viwanja vya
ndege ni tatizo la Dunia nzima hivyo linahitaji ushirikiano na kila mtu.
Alisema kwa sasa jeshi lake limejipanga kuhakikisha linapambana na
matukio hayo kwa kuweka mikakati mbalimbali ikiwamo la kuweka vitendea
kazi vya kisasa.
Kato hakuweza kuelezea mikakati mingine iliyopo kwa kile alichodai ni kuogopa kuwapa mbinu hiyo wahusika wa dawa hizo.
Alisema suala la ukamatwaji wa dawa za kulevya haliwezi kushughulikiwa
na taasisi moja tu, bali linahitaji ushirikiano wa hali ya juu pamoja na
kujipanga.
Alisema siyo jeshi la Polisi peke yao ndiyo wanaopaswa kutupiwa lawama
huku kukiwa na taasisi mbalimbali zinazofanya kazi ya kukagua mizigo
JNIA.
CHANZO: NIPASHE
إرسال تعليق