- Sheikh Ponda alisafirishwa usiku wa manane kutoka Morogoro baada ya juzi kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni mtutu wa bomu saa 12:25 jioni alipokuwa akisindikizwa na wafuasi wake kwenda katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja mara baada ya kumaliza kutoa mhadhara katika kongamano mjini hapo.
Dar es Salaam/Moro.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi
za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda yupo chini ya ulinzi huku
akitibiwa majeraha katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Sheikh
Ponda alisafirishwa usiku wa manane kutoka Morogoro baada ya juzi
kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni mtutu wa bomu saa 12:25 jioni
alipokuwa akisindikizwa na wafuasi wake kwenda katika Msikiti wa Mungu
Mmoja Dini Moja mara baada ya kumaliza kutoa mhadhara katika kongamano
mjini hapo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Sheikh Idd Mussa Msema, alidai kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi tatu begani.
Taarifa
kutoka ndani ya familia ya Ponda zilisema kwamba baada ya kupata
taarifa za kupigwa risasi, baadhi ya masheikh walifunga safari kwenda
Morogoro na kumrejesha Dar es Salaam usiku huohuo. Kabla ya kurudishwa
Dar es Salaam, imeelezwa kuwa Sheikh Ponda alipelekwa katika Zahanati ya
Islamic Foundation.
Mmoja wa wanafamilia alidokeza kwamba Sheikh
Ponda alifichwa na alikuwa chini ya ulinzi mkali wa wafuasi wake na
hakuna aliyeruhusiwa kumsogelea.
Muhimbili
Hata hivyo,
habari zilizopatikana baadaye jana zilisema kuwa alifikishwa Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Sheikh Ponda
alifikishwa Muhimbili jana saa 7:18 mchana na alipelekwa kwenye chumba
cha wagonjwa wa dharura na baadaye alitolewa na kupelekwa kwenye chumba
cha x-ray kwa ajili ya vipimo. Baadaye alipelekwa chumba cha upasuaji.
Eneo
kubwa la hospitali hiyo lilikuwa na idadi kubwa ya askari na mmoja wa
askari waliokuwa doria hospitalini hapo alisema walitawanywa kwenye
hospitali mbalimbali za Dar es Salaam baada ya kupata taarifa kuwa
angeletwa kwa matibabu.
“Nakuambia tuko hapa tangu saa kumi na
moja asubuhi, tumetawanywa hospitali mbalimbali baada ya kupata taarifa
kuwa analetwa Dar. Bahati nzuri kaletwa hapa Muhimbili... tunasubiri
apate matibabu na tutamtia mbaroni,” alisema askari huyo.
Taarifa ya polisi
Msemaji
wa Polisi, Advera Senso alisema jana katika taarifa yake kuwa Sheikh
Ponda yuko Hospitali ya Muhimbili akitibiwa baada ya kupata majeraha
yaliyotokana na purukushani na polisi wakati wafuasi wake walipokuwa
wanataka kumtorosha.
“Kutokana na tukio hilo, timu inayoshirikisha
wajumbe kutoka Jukwaa la Haki Jinai likiongozwa na Kamishna wa Polisi
Isaya Mungulu imeanza uchunguzi wa tukio hilo na Polisi inawataka
wananchi kuwa watulivu wakati wanashughulikia suala hilo kisheria.”
Polisi Morogoro wapigwa chenga
Wakati akiwa Muhimbili, Polisi mkoani Morogoro, lilisema bado linamtafuta Sheikh Ponda.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema jana kuwa kwa
taarifa zilizopo, bado Sheikh Ponda amefichwa mkoani Morogoro na kwamba
anaendelea kutafutwa.
“Tamko la Serikali mpaka sasa
hatujathibitisha kwamba Sheikh Ponda amejeruhiwa na risasi na tunamtaka
mtu yeyote awe yeye au ndugu yake aje kuthibitisha kwamba amepigwa
risasi,” alisema.
Alikanusha madai kwamba jeshi hilo limehusika
kumpiga risasi akisema hakuna ushahidi kwa kuwa hajaonekana ili
kuonyesha kuwa amepata majeraha sehemu yoyote ya mwili wake.
“Siku zote risasi haifichiki, kama amepigwa angejitokeza ili kupewa kibali cha matibabu,” alisema Shilogile.
Alisema
polisi inawashikilia watu wawili na inawatafuta viongozi watano wa
Umoja wa Waadhiri wa Kiislamu Mkoa wa Morogoro walioandaa kongamano
hilo.
Kamanda Shilogile alisema waandaaji wa kongamano hilo
walipewa kibali na polisi kufanya kongamano kwa masharti ya kutokutoa
matamshi ya uchochezi ikiwa ni pamoja na Sheikh Ponda kutokuhudhuria.
Alisema
hata hivyo, katika kongamano hilo lililofanyika eneo la Kiwanja cha
Ndege kulikuwapo na wageni zaidi ya watano waliohutubia. Kamanda
Shilogile alisema ilipofika saa 12.50 jioni ndipo Sheikh Ponda alipofika
na baadaye kupewa dakika tano kuzungumza na alieleza kuwa yeye si
mzungumzaji kwa siku hiyo na badala yake angezungumza leo katika Viwanja
vya Msikiti wa Jabal Hirra.
Alisema baada ya hapo mkutano
ulifungwa na wafuasi wake wakaanza kusukuma gari alilokuwa amepanda
katika Barabara ya Tumbaku karibu na Kituo cha Mafuta cha El Saedy.
Alisema kuwa, polisi walimfuata kutaka kumtia mbaroni lakini wafuasi
wake walianza kurusha mawe na ndipo askari hao walipofyatua juu risasi
tatu za baridi ili kuwatawanya.
Hata hivyo, alisema polisi
walizidiwa nguvu na wafuasi hao ambao walifanikiwa kumtorosha Sheikh
huyo kwa pikipiki.Alisema kuwa baadaye zilizagaa taarifa kuwa amepigwa
risasi ya begani na kupelekwa Hospitali ya Mkoa kisha kutoroshwa
kusikojulikana.
Wavamia hospitali
Katika
hatua nyingine, watu wanaosadikiwa ni wafuasi wa Sheikh Ponda wamevamia
Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na kufanya uharibifu kwa kuvunja vioo
katika wodi namba sita ya watoto wakishinikiza kuonyeshwa Sheikh huyo
alipo.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa na watoto wao katika wodi
hiyo, Kibua Michael na Cecilia Clemence kwa nyakati tofauti walisema
kwamba wafuasi hao walikusanyana nje ya hospitali hiyo na kurusha mawe
na kusababisha taharuki kwa baadhi ya wagonjwa.
Sheikh Kundecha atoa sharti
Taasisi
na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, imeitaka Serikali kuunda tume huru ya
uchunguzi wa tukio la kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda na majibu yake ndiyo
yatakayoamua uhusiano baina ya Waislamu nchini na Serikali iliyopo
madarakani.
Akitoa tamko la Jumuiya hiyo katika Msikiti wa
Mtambani, Kinondoni, Dar es Salaam jana, Amiri wa Jumuiya hiyo, Sheikh
Yusufu Mussa Kundecha alisema pamoja na mambo mengine, pia wanataka
kuona askari polisi aliyemdhuru Sheikh Ponda anachukuliwa hatua za
kisheria.
Alisema kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda ni mtiririko
wa vitendo vya uonevu na unyanyasaji na aliishangaa Serikali kumtafuta
Sheikh huyo kupitia vyombo vya habari wakati inafahamu hatua za kuchukua
pale wanapokuwa wanamtafuta mtu.
Alisema hata yeye wakati
anatafutwa na polisi alipelekewa barua akitakiwa kuripoti kituoni lakini
si kupitia vyombo vya habari na kitendo hicho kinaonyesha wazi kuwa
Serikali imeshindwa kuwahakikishia raia usalama wao.
“Mbaya zaidi,
wao ambao wanataka watu wasichukue sheria mkononi ndiyo hao wa kwanza
kufanya hivyo jambo ambalo sidhani kama litatufikisha pazuri,” alisema
Kundecha.
Aliitaka Serikali kufuata sheria na kufuata taratibu
husika katika kushughulikia masuala yanayowahusu makundi mbalimbali
katika jamii badala ya inavyofanya sasa akisema hiyo inachangia chuki
kati ya Waislamu na Serikali.
Profesa Lipumba atoa tamko
Mwenyekiti
wa (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Rais Jakaya Kikwete
kuingilia kati suala la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda ili nchi isije
kuingia kwenye machafuko yenye mrengo wa kidini.
Profesa Lipumba
aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake Dar es Salaam kuwa
chama hicho kinalaani vikali tukio hilo na kutaka polisi kuwakamata
waliompiga risasi.
“Nimetoka kumjulia hali muda mfupi uliopita,
nimemkuta akiwa katika hali mbaya japo anaweza kuzungumza na kutambua
watu wanaokwenda kumwona... kwa kweli tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh
Ponda linaweza kusababisha nchi kuingia kwenye machafuko ya kidini kama
hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Tukio la Sheikh Ponda kupigwa risasi tena na watu wanaodhaniwa kuwa ni polisi, limeleta sura mbaya kwa taifa,” alisema Lipumba.
Rufaa ya wafuasi wake leo
Wakati
hayo yakitokea, rufaa ya wafuasi 52 wa Sheikh Ponda waliohukumiwa
kifungo cha mwaka mmoja jela inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Wafuasi hao walihukumiwa kifungo
hicho, Machi 21, mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya
kutiwa hatiani kwa makosa matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakabili.
Walikuwa
wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, kutenda makosa, kukaidi amri ya
polisi kabla na baada ya kufanya maandamano yaliyozuiwa na polisi,
kufanya mikusanyiko haramu na kusababisha uvunjifu wa amani na
uchochezi.
Hata hivyo, kupitia kwa Wakili wao, Mohamed Tibanyendera walikata rufaa wakipinga hukumu na adhabu waliyopewa.
Rufaa hiyo itasikilizwa leo na Jaji Salvatory Bongole.
Kwa
mujibu wa hati ya rufani waliyoiwasilisha mahakamani hapo, wafuasi hao,
pamoja na mambo mengine, wanadai kuwa hakimu alikosea kisheria katika
kuchambua ushahidi wa pande zote uliowasilishwa mahakamani.
Pia
wanadai kuwa katika hukumu hiyo, hakimu alijikanganya kwa kumwachia huru
mmoja wa washtakiwa na kuwatia hatiani washtakiwa wengine.
Watu
hao walikamatwa na Polisi Machi 15, mwaka huu, wakiandamana kwenda Ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa lengo la kumshinikiza kumpa
dhamana Sheikh Ponda na mshtakiwa mwenzake Mukadam Swalehe na Machi 18,
mwaka huu walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka.
Imeandikwa na Lilian Lucas (Morogoro), James Magai, Bakari Kiango, Aziza Masoud, Aidan Mhando na Joseph Zablon (Dar).
Post a Comment