Gazeti la kila siku la Telegraph la hapa Uingereza linaripoti kuwa
baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislam visiwani Zanzibar wanaamini kuwa
shambulio la tindikali dhidi ya mabinti wawili wa Kiingereza, Kirstie
Trup na Katie Gee lilifanywa na wafuasi wa kikundi cha UAMSHO, ambacho
kinataka Zanzibar ijitenge na Tanzania Bara na kisha kuanzisha sheria
kali za Kiislam.
Huko nyuma kumeshatokea mashambulizi dhidi ya viongozi wa dini ya
Kiislam na Kikristo, ikiwa ni pamoja na mashambulio ya tindikali na
mauaji.
"Ofkoz, itakuwa kazi ya Uamsho," alinukuliwa Sheikh Fadhil Soraga,
aliyeshambuliwa kwa tindikali Novemba mwaka jana, na anaamini wahusika
katika tukio hilo dhidi yake walikuwa UAMSHO.
Wiki mbili zilizopita, vipeperushi vya vyenye wito mkali wa uchochezi
dhidi ya Wakristo vilisambazwa sehemu mbalimbali huo Zanzibar, tukio
linalohusishwa na harakati za UAMSHO.
"Siku 10 tu zilizopita, walikuwa wanasema wanaandaa kitu kikubwa. Tukio
hili, ambalo Waislamu wote twapaswa kulilaani, ni kazi ya kundi hilo
(UAMSHO)," alisisitiza Sheikh Soraga.
Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Zainzibar, Padri Cosmas Shayo
naye alikuwa na mtizamo kama huo wa Sheikh Soraga. Mtangulizi wa Padri
huyo, Padre Evaristus Mushi, aliuawa kwa kupigwa risasi mwezi Februari,
na hisia zimekuwa kwamba UAMSHO walihusika na tukio hilo.
"Hawa watu wamedhamiria kuzusha vurugu ili kufikia malengo yao," alisema.
"Wanataka kuifanya Zanzibar iwe ya Waislam pekee, na walianza kwa
kuwatisha Wakristo na sasa wanataka kuwatisha watalii ambao wanawaona
kama Wakristo pia."
Kabla ya shambulio hilo la tindikali, mmoja wa mabinti hao, Katie,
alizabwa kibao na mwanamke mmoja mtaani wakati wa mfungo wa Mwezi wa
Ramadhan.
Katie na Kirstie, walikuwa Zanzibar wakifanya kazi kwa kujitolea, baada
ya kumaliza masomo yao ya sekondari. Wote wanatoka katika familia
zinazojiweza kimaisha. Baba ya Katie ni chartered surveyor,moja ya ajira
inayolipa vizuri hapa Uingereza, huku Kirstie alisoma sekondari ambayo
ada yake ni pauni 3,375 (zaidi ya Sh milioni 13) kwa muhula.
Mabinti hao walikuwa Zanzibar kwa mwezi mmoja wakijitolea katika shule
ya chekechea ya Mtakatifu Monica, iliyopo Stone Town, kupitia shirika la
kujitolea la Art in Tanzania.
Siku moja kabla ya shambulio hilo la tindikali, ali-tweet kwa furaha
baada ya kukutana na Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, alipozuru
Zanzibar hivi karibuni kuhamasisha vita dhidi ya malaria kupitia
Clinton Health Access Initiative.
Kwa mujibu wa gazeti la Telegraph, mmoja wa masapota wakubwa wa UAMSHO
ni Sheikh Ponda Issa Ponda, anayedaiwa kutumia wiki tatu zilizopita
kuhamasisha Waislam Zanzibar 'kuamka kama huko Misri.'
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Elieza Feleshi alinukuliwa akisema
kuwa Serikali itafanya kila jitihadakumkamata Sheikh Ponda.
Wakati huo huo, gazeti la kila Jumapili la Sunday Mirror lina habari
ndefu kuhusu Sheikh Ponda, iliyobeba kichwa cha habari: "Shambulio la
tindikali Zanzibar: Mhubiri wa chuki Sheikh Ponda Issa Ponda apigwa
risasi na polisi, akamatwa"
Gazeti hilo limeeleza kuwa polisi walimpiga Ponda risasi ya machozi
begani kabla ya kumkamata, na sasa yupo mahututi hospitalini.
Habari hiyo inaeleza kuwa Ponda alikwenda Zanzibar kuhamasisha
maandamano dhidi ya serikali, na kukiunga mkono kikundi cha UAMSHO, kwa
malengo ya kutimua wageni Zanzibar na kuanzisha sheria za Kiislam
Post a Comment